Image

Kamwe usimtikise mtoto mchanga!!

 

SHAKEN BABY SYNDROME (SBS) NI NINI?

Utangulizi:

Umewahi kuwaza kwamba unaweza kumpoteza mwanao mchanga kwasababu ya kumtikisa?

Shaken Baby Syndrome (SBS), au "sindromu ya watoto kutikiswa," ni hali ambayo inajielezea kwenye jina lake. Hali hii hutokea pale mtoto mchanga anapotikiswa kwa nguvu na kusababisha athari katika ubongo wa mtoto, na inaweza kusababisha madhara makubwa katika kimwili na afya afya kwa ujumla.

SBS ni sababu kubwa zaidi ya kifo/ athari ya ubongo inayosababishwa na unyanyasaji wa watoto. 

Kwa jumla 95% ya watoto wachanga walio na jeraha kubwa la kichwani wametikiswa. Asilimia inayobaki husababishwa zaidi na majeraha makubwa ya kichwa kama vile ajali za magari.(Blumenthal, 2002) 

Ni Kitu gani hupelekea mtoto kutikiswa?

SBS mara nyingi hutokea kutokana na hasira au kukata tamaa kwa mzazi au mlezi, hasa wakati mtoto analia kwa muda mrefu. Wakati mwingine ni unyanyasaji wa mtoto(child abuse) kutoka kwa mlezi hupelekea hadi mtoto kutikiswa. Wakati mwingine ni kutokujua kwa mlezi na akafanya shughuli ya mtikisiko kama kurukaruka huku akiwa amembeba mtoto mchanga.

Nini hutokea baada ya mtoto kutikiswa?

 

  1. Kutikiswa kwa nguvu kunaweza kusababisha ubongo wa mtoto kugonga ndani ya fuvu lake, na hivyo kusababisha uharibifu mkubwa wa seli za ubongo.
  2. Mishipa ya damu midogomidogo huweza kupasuka na kusababisha kuvuja damu ndani ya ubongo.
  3. Mabonge makubwa ya damu yanaweza kutengenezwa na kugandamiza ubongo na kusababisha kuvimba.
  4. Misuli ya shingo ya mtoto mchanga haijakomaa hivyo haina nguvu ya kulinda mifupa inayozunguka uti wa mgongo ili isikandamize uti wa mgongo.
  5. Majeraha yanayotokana na mtikisiko huu wa ubongo yanaweza kusababisha ulemavu wa akili,kupooza, upofu, uziwi na hata kifo.

Dalili za SBS

Dalili za sbs zina wigo mpana na zinaweza kua dalili ndogo zisizo na kiashiria dhahiri cha jeraha la ubongo au zinaweza kua dalili kubwa na mbaya zaidi.

a)Dalili za SBS zinaweza kujitokeza papo kwa hapo au zikatokea baada ya muda.

  1. Baadhi ya dalili zisizo na kiashiria dhahiri cha jeraha la ubongo ni kama:
  2. Mtoto anaweza kuwa na shida ya kulala,
  3. Kutapika mara kwa mara
  4. kushindwa kula.
  5. Uchovu na kulegea
  6. Kuwa na usingizi wa kupita kiasi: Mtoto anaweza kuwa na usingizi mwingi zaidi ya kawaida.
  7. Mabadiliko ya tabia: Hali kama vile kukasirika bila sababu au kuwa mpweke.
  8. Kukosa uchangamfu

b)Dalili kubwa zinazoweza kuashiria athari kwenye ubongo na uti wa mgongo:

  1. Degedege (seizure)
  2. Kushindwa kupumua
  3. Kupooza (paralysis)
  4. Kupoteza fahamu (coma) 

Athari za kudumu

Madhara ya SBS yanaweza kuwa makubwa na ya kudumu. Mfano wa madhara haya ni kama:

  1. Ulemavu wa akili (intellectual disability)
  2. Changamoto na uzito katika kujifunza (learning difficulties)
  3. Matatizo ya mihemko (emotional problems)
  4. Kichwa kujaa maji (hydrocephalus)

Kinga na Elimu

Ni muhimu kutoa elimu kwa wazazi na walezi kuhusu madhara ya SBS. Mifano ya njia za kuzuia ni pamoja na:

  1. Kujifunza njia bora za kushughulikia hasira na msongo wa mawazo.
  2. Kutafuta msaada wa kitaalamu wakati wa hali ngumu, msongo wa mawazo, ugonjwa wa akili na sonona wakati wa kujifungua. (post-partum psychosis and post-partum depression)
  3. Wenza na ndugu kumsaidia mzazi mpya kulea na Kuelewa kuwa mtoto anahitaji upendo na uvumilivu.

Hitimisho

Shaken Baby Syndrome ni tatizo kubwa linalohitaji umakini na elimu ya kina. Kwa kuwajulisha wazazi na jamii, tunaweza kusaidia kuzuia hali hii na kulinda watoto wetu. Kila mtoto anastahili kuwa na mazingira salama na yenye upendo. 

Marejeo

  1. Medscape
  2. I Blumenthal, Shaken baby syndrome, Postgraduate Medical Journal, Volume 78, Issue 926, December 2002, Pages 732–735, https://doi.org/10.1136/pmj.78.926.732

 

 

 

Imesomwa mara 136 Imehaririwa Jumanne, 12 Novemba 2024 14:37
Dr Ladina Msigwa

Distinguished medical doctor and acclaimed author with a passion for enhancing healthcare and sharing knowledge through the written word.

Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.