Image

Jinsi gani watoto wanapaswa kuwa na heshima kwa dada wa kazi nyumbani.

Inasikitisha sana unapokuta mtoto anakosa heshima kwa dada anayemlea na kukaa naye nyumbani pale wazazi wanapokuwa kazini. Na mara nyingine mzazi anaona ni sawa tu na wala hamkemei mtoto wake kwa tabia hizo.
Unakuta mtoto anamuona dada wa kazi kama mtu asiye na thamani na wa kudharaulika tu. Akiamka asubuhi wala hamsalimii, anatupatupa vitu ovyo akijua kuna mtu wa kuviokota, akila anaacha vyombo hapo hapo mezani na kumuamuru msichana wa kazi avitoe na anaongea naye kwa lugha ya dharau na kuamrisha.
 
Yaani mtoto mdogo anaweza kumgombeza dada wa kazi kama wamelingana vile, hali hii ikiachwa kuendelea inafika wakati wakiwa na umri mkubwa kidogo wanaanza kuwapiga wadada wa kazi.
Mtoto akiachwa kuendelea na dharau kwa msichana wa kazi ambaye anakaa naye kila siku na kumlea atajenga tabia ya kudharau mtu yeyote aliye chini yake na hii itampelekea kuwa na mahusiano mabaya kuanzia shuleni, kazini hadi kwenye ndoa yake.
Ni vizuri mtoto tangu akiwa na umri mdogo akafahamu kuwa watu wote ni sawa na hakuna mtu bora zaidi ya mwingine. Atambue kuwa dada wa kazi yupo pale kama msaidizi na sio mtumwa.
 
Dharau hii ya mtoto kwa dada wa kazi mara nyingi huchangiwa na jinsi mzazi anavyomtendea msichana wake wa kazi. Onyesha mfano mzuri kwa mtoto wako kwa kukaa vizuri na kwa upendo na msaidizi wa kazi na utamsaidia mtoto wako aweze kujifunza heshima kwa watu wote wanaomzunguka.
Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini.
Share