Image

Kulika kwa Meno - Sehemu ya 2

Wiki iliyopita niliongelea kulika kwa meno kama hali inayotokea wakati sehemu ngumu ya nje ya meno huondoka na kusababisha sehemu ya ndani kuwa wazi.

Nilitaja kuwa ziko aina mbali mbali za kulika kwa meno kulingana na nini kinasababisha tatizo. Aidha kinga au tiba hutegemea nini kinasababisha tatizo hilo. Nikaongelea kwa undani kulika kwa meno kunakosababishwa na meno kusagana yaani attrition.

Leo nitaongelea aina nyingine ya kulika kwa meno

Kuyeyuka kwa meno (tooth erosion)

Huku ni kulika kwa meno kunakosababishwa na kemikali hasa tindikali. Tindikali inayoyeyusha meno haya yaweza kutoka nje au ndani ya mwili wenyewe.

Kuyeyuka kwa meno kunakosababishwa na tindikali toka nje ya mwili: Baadhi ya vyakula na vinywaji tunavyokula na kunywa vina kiwango kikubwa cha tindikali (acid), hivyo vyakula na vinywaji hivyo vikikaa kinywani kwa muda huweza kusababisha meno kuyeyuka.

Kiwango cha uharibifu kinategemea mara ngapi unatumia vyakula/vinywaji hivyo, kiwango cha tindikali katika vinywaji hivyo na muda vinaokaa kinywani. Tindikali nyingine inaweza kupatikana katika hewa hasa maeneo ya viwanda vinavyotengeneza betri. Myeyuko unaotokana na tindikali ya nje huathiri zaidi sehemu za nje za meno (buccal or facial surfaces).  Myeyuko utokanao na vinywaji vya tindikali

Watu walio katika hatari zaidi ya kupata tatizo hili ni wale ambao hunywa vinywaji vyenye kaboni kwa wingi (carbonated drinks), juice ya limau au wale wenye tabia ya kufyonza limau. Tatizo linaongezeka kwa wale wenye tabia ya kuweka juice na kukaa nayo mdomoni kwa muda bila kuimeza (unaisikilizia utamu mpaka kwenye kisogo). Unashauriwa unapokunywa juice hizi kumeza haraka.myeyuko utakanao na vinywaji vyatindikali

Kuyeyuka kwa meno kunakosababishwa na tindikali toka ndani ya mwili

Kuyeyuka huku kunasababishwa na tindikali kutoka kwenye tumbo. Meno yanakwanguka sehemu za ndani (palatal and lingual surfaces) kama picha inavyoonesha hapa kulia.

Watu watu walio katika hatari kubwa ya kupata tatizo hili ni wale ambao wana matatizo ya kutapika mara kwa mara kama ugonjwa sugu na wale ambao hula sana lakini kwa vile wanataka wabaki wembamba (slim), kila wakila baada ya muda hujitapisha ili wasinenepe. Matapishi huja na tindikali iliyoko tumboni (gastric hydrochloric acid).

Wanywa pombe kali sugu nao hawaachwi nyuma, pombe kali hukwangua kuta za tumbo na kusabisha chronic gastritis hali ambayo tindikali huwa inamwagika kwenye tumbo zaidi ya kawaida na wakati mwingine hurudi kinywani kama mvuke na kusababisha madhara haya.

Hali inakuwa mbaya kwa wale wanao tapika mara kwa mara na katika hali ya kurudisha maji mwilini maana wanakuwa na kiu ya mara kwa mara hunywa juice au soda kwa wingi pia ili kukata kiu. Watu wa aina hii meno yao huyeyuka sehemu zote yaani nje na ndani.

Dalili

Katika hali zote eneo lililoathirika huonekana angavu, gumu, la njano kuelekea kahawia na laini (smooth).
Dalili zake ni kama zile za kulika kwa meno kunakotokana na namna nyingine, msisimko (sensitivity) wakati wa kunywa vinywaji baridi, kuvuta hewa na hata maumivu kulingana na kiwango cha uharibifu na uwezo wa mwili kujihami.

Matibabu

Matibabu hulenga kugundua na kutibu kisababishi. Kama ni matatizo ya tumbo tabibu wa meno atakupeleka kwa tabibu wa kawaida (general practitioner/physician). Kwa wale wenye tabia hatarishi, la msingi ni kushauriwa kuacha tabia hizo. Mgonjwa akitengemaa basi sehemu zilizoathirika huweza kupigwa viraka kwa dawa zenye rangi kama ya jino (composite veneer).

Kwa wale walioshindikana meno huvalishwa kofia ngumu (crown) ili kuyakinga na myeyuko zaidi.

Imesomwa mara 7217 Imehaririwa Alhamisi, 20 Desemba 2018 09:11
Dr. Augustine Rukoma

Dr Dr. Augustine Rukoma ni daktari na mtaalamu wa meno, anapenda kutumia muda wake wa ziada kuandika makala na kubadilishana mawazo juu ya afya ya kinywa na Meno.

rukomadentalanswers.blogspot.com | Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.

Makala shabihana