Image

Saratani ya Koo (Cancer of the Esophagus) - Chanzo, Dalili na Tiba

Utangulizi

Saratani ya koo ni miongoni mwa magonjwa ya kutisha. Ingawa baadhi ya wagonjwa wa saratani ya koo wanaweza kutibiwa na kupona kabisa, kuna mjadala miongoni mwa matabibu juu ya tiba sahihi ya ugonjwa huu. Bila kujali ni aina gani inayotumika, karibu aina zote za tiba za saratani hii huwa na madhara kwa mgonjwa na wakati mwingine kusababisha kifo badala ya kuponya.

Muundo wa Koo

Ili tuweze kujadili vizuri ugonjwa huu, ni vema kwanza tuangalie muundo wa koo. Koo ni sehemu mojawapo ya mfumo wa chakula likiwa na urefu wa takribani sentimita 25 kuanzia mdomoni mpaka kwenye mfuko wa tumbo yaani stomach.

Ukuta wa koo unajengwa na tando (layers). Tando hizi zimetengenezwa kwa aina tofauti ya chembe hai au seli ambazo kila moja ina kazi zake maalum. Sehemu ya ndani kabisa ya ukuta wa koo huitwa mucosa ambayo hufanya kazi ya kulowanisha chakula ili kiweze kupita vizuri kuelekea kwenye mfuko wa chakula.

Chini ya utando huu, kuna utando mwingine unaoitwa submucosa ambao umejaa tezi zenye kuzalisha ute unaoitwa mucus ulio na kazi ya kulainisha koo na kulifanya liwe na hali ya umajimaji muda wote. Utando wa tatu unajulikana kama muscle layer. Utando huu umejaa misuli inayosaidia koo kusukuma chakula kuelekea tumboni. Utando wa juu kabisa unaolizunguka koo huitwa outer layer ambao una kazi ya kulinda koo kwa ujumla.

Aina za saratani ya koo

Kuna aina kuu mbili za kansa ya koo, nazo ni Adenocarcinoma na squamous cell carcinoma. Aina hizi hutofautiana kulingana na jinsi seli zake zinavyoonekana kwenye darubini. Hata hivyo, pamoja na tofauti hizi za kimuonekano, utambuzi na matibabu ya aina hizi za saratani ya koo hufanana.

Aina zote hizi mbili huanza kwanza kuathiri seli zilizo katika utando wa ndani wa ukuta wa koo yaani mucosa kabla ya kusambaa maeneo mengine.

Vihatarishi vya kansa ya koo

Ingawa chanzo halisi cha kansa ya koo hakijulikani, mambo yafuatayo yanaweza kusababisha mtu kupata saratani ya koo. Hata hivyo, pamoja na kuwepo vihatarishi hivi, ni vigumu kueleza kwa ufasaha kwa nini mtu au watu fulani wanaweza kupatwa na kansa ya koo na mtu mwingine asipate. Vihatarishi hivi ni

 • Umri: Hatari ya kupata saratani ya koo huongezeka zaidi kwa watu walio na umri wa miaka 65 na kuendelea. Hata hivyo saratani ya koo aina ya adenocarcinoma inaweza kutokea hata kwa wanawake walio na umri kuanzia miaka 40 na kuendelea.
 • Jinsia: Tafiti nyingi zimeonesha kuwa wanaume wana uwezekano wa kupata saratani ya koo mara tatu zaidi ya wanawake.
 • Uvutaji sigara: Wavutaji sigara wapo katika hatari ya kupata saratani ya koo ukilinganisha na wasio wavutaji.
 • Unywaji pombe wa kupindukia: Unywaji wa pombe kwa kiasi cha chupa tatu na zaidi kwa siku unamuweka mnywaji katika hatari ya kupata saratani ya koo ikilinganishwa na mtu asiyekunywa kabisa pombe. Aidha wanywaji wa kupindukia ambao pia ni wavutaji sigara wana hatari kubwa zaidi ya kupata saratani ya koo ikilinganishwa na wanywaji wa pombe wasio wavutaji sigara. Kwa maneno mengine, unywaji pombe pamoja na uvutaji sigara hufanya kazi kwa pamoja kuongeza uwezekano wa mtu kupata saratani ya koo.
 • Lishe: Kuna mjadala kuhusu mchango wa aina fulani za vyakula katika kusababisha saratani ya koo. Wakati watafiti wengine wanasema ulaji wa matunda na mboga mboga husaidia kupunguza uwezekano wa kupata saratani ya koo, watafiti wengine wanapinga kuhusu suala hilo.
 •  Unene kupindukia : Unene wa kupitiliza huongeza uwezekano wa kupata saratani ya koo aina ya adenocarcinoma.
 • Matatizo ya tumbo: Matatizo sugu katika tumbo yanayosababisha tindikali kurudi kwenye koo (acid reflux) kutoka tumboni husababisha madhara katika seli za koo na hatimaye kupelekea saratani ya koo kwa baadhi ya watu.
 • Tatizo sugu la kucheua kwa tindikali: Iwapo tatizo la tindikali kucheuliwa kwenye koo litaendelea kwa muda mrefu mpaka kuwa sugu, sehemu ya chini ya koo yaweza kuathiriwa na kusababisha hali ijulikanayo kitaalamu kama Barrett esophagus. Hali hii huongeza uwezekano wa kutokea kwa saratani ya koo.

Dalili za saratani ya koo

Mgonjwa mwenye saratani ya koo katika hatua za awali anaweza asioneshe dalili zozote zile. Hata hivyo, kadiri saratani inavyozidi kukua na kuenea, mgonjwa anaweza kuwa na dalili zifuatazo:

 • Chakula kukwama kwenye koo
 • Siku za mwanzo mgonjwa anaweza kushindwa kumeza chakula kigumu kisha cha majimaji na baadaye akashindwa kumeza hata mate
 • Maumivu wakati wa kumeza chakula hasa chakula kigumu
 • Maumivu kwenye kifua au mgongoni
 • Kupungua uzito
 • Kiungulia
 • Sauti ya mkwaruzo au kikohozi kikavu cha zaidi ya wiki mbili
 • kupaliwa mara kwa mara

Hata hivyo ifahamike kuwa dalili hizi zinaweza kutokea pia kwa baadhi ya magonjwa mengine tofauti na saratani ya koo. Hivyo ni vizuri kumuona daktari kwa uchunguzi zaidi.

Uchunguzi na vipimo

Ili kujiridhisha kuwa mgonjwa ana saratani ya koo, daktari atasikiliza historia ya mgonjwa kisha atamfanyia uchunguzi wa mwili wake kabla ya kuagiza kufanyika kwa vipimo kuthibitisha zaidi.

Vipimo kwa ajili ya utambuzi wa saratani ya koo ni pamoja na

 • Aina ya X ray iitwayo Barium swallow ambayo huonesha muundo wa koo pamoja na tumbo (stomach).
 • Kipimo cha Endoscopy ambacho husaidia kuchunguza ndani ya koo, tumbo pamoja na eneo lote la utumbo
 • Kuchunguza sehemu ya koo kwenye darubini (biopsy). Kwa sasa, njia hii ndiyo ya uhakika zaidi ya kutambua uwepo wa seli za saratani katika koo.

Iwapo itathibitika kuwepo kwa saratani katika koo, madaktari hupendelea kufahamu hatua ya ugonjwa ilipofikia. Kitendo hiki huitwa staging. Faida ya kufanya staging ni kuwa husaidia kufahamu ukubwa wa tatizo yaani ni kwa kiasi gani seli za koo zimeathiriwa, iwapo saratani imesambaa na kuathiri maeneo ya jirani na kama imesambaa ni viungo gani vilivyo athirika.

Aidha staging husaidia pia kufanya maamuzi ya njia gani ya tiba itumike katika kumtibu mgonjwa. Saratani ya koo huweza kusambaa na kuathiri sehemu kama mifupa, ini na mapafu.

Ili kufahamu kama saratani imesambaa kwenye viungo hivi, vipimo vifuatavyo vyaweza kufanyika:

 • Kipimo kiitwacho endoscopic ultrasound ambacho husaidia kutambua iwapo viungo vilivyo jirani na koo vimeathirika ama la. Pia husaidia kufahamu hali ya tezi (lymph nodes) zilizo karibu na koo. Daktari pia anaweza kuchukua sehemu ya tezi hizo (lymph node biopsy) kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
 • CT Scan husaidia kutambua jinsi koo na sehemu nyingi za mwili zilivyoathirika.
 • MRI ni kipimo kingine kinachosaidia kuonesha iwapo saratani ya koo imesambaa na kuathiri tezi na sehemu nyingine za mwili.
 • PET scan: Nia aina ya kipimo ambacho huonesha kwa uhakika na ubora zaidi ukilinganisha na vipimo vingine uwepo wa saratani ya koo na kama imesambaa sehemu nyingine za mwili. Hata hivyo, kipimo hiki kwa sasa hakipatikani nchini kwetu.
 • Bone scan ni kipimo ambacho huwezesha kutambua iwapo saratani imesambaa mpka kwenye mifupa.

Wakati mwingine madaktari hulazimika kufanya upasuaji ili kuweza kufanya staging kwa uhakika zaidi.

Kwa mujibu wa staging, kuna hatua tano za saratani ya koo:

 • Hatua ya 0: Hatua hii huitwa carcinoma in situ ambapo seli za saratani hupatikana tu kwenye utando wa juu wa koo.
 • Hatua ya I: Saratani husambaa kutoka utando wa juu mpaka kwenye tando nyingine za koo.
 • Hatua ya II: ina tabia mojawapo kati ya hizi zifuatazo:
  • Saratani husambaa kutoka kwenye utando wa juu wa ukuta wa koo mpaka kwenye utando wa chini yake yaani submucosa na kisha kuenea kwenye tezi za karibu, AU
  • Saratani husambaa na kushambulia utando wa misuli wa koo (muscle layer) na baadhi ya seli nyingine za saratani hufika kwenye tezi za jirani, AU
  • Saratani husambaa kutoka katika utando wa ndani mpaka kufikia utando wa nje kabisa (outer layer) wa koo.
 • Hatua ya III: ina tabia mojawapo kati ya hizi:
  • Saratani husambaa kufikia kwenye utando wa nje kabisa wa koo na kisha kusambaa hadi kwenye tezi za jirani, AU
  • Saratani husambaa na kushambulia viungo vya karibu na koo kama vile njia ya hewa. Aidha seli za saratani huwa zimesambaa mpaka kwenye tezi za jirani.
 • Hatua ya IV: Seli za saratani husambaa na kuathiri viungo vingine vilivyo mbali na koo kama vile mapafu, ini na mifupa.

Matibabu ya Saratani ya Koo

Uchaguzi wa aina gani ya tiba itumike hutegemea sana eneo lililoathiriwa na saratani, iwapo saratani imeshambulia viungo vilivyo karibu na koo, iwapo saratani imesambaa mpaka kufikia kwenye tezi au viungo vingine vya mwili, na hali ya mgonjwa kwa ujumla.

Kutokana na hayo, saratani ya koo yaweza kutibiwa kwa kufanya upasuaji, kutumia mionzi, kutumia kemikali maalum, au mchanganyiko wa yote matatu.

Upasuaji

Kuna aina kadhaa za upasuaji kwa ajili ya kutibu saratani ya koo. Kila aina inategemea sehemu saratani ilipo. Daktari wa upasuaji anaweza kuondoa sehemu iliyoathiriwa au kuondoa koo lote. Hata hivyo kabla upasuaji haujafanyika, daktari hujadiliana na mgonjwa wake kumueleza ni aina gani ya upasuaji utakaofanyika, faida na hasara zake, na nini cha kutarajia kutokana na upasuaji huo.

Tiba ya Mionzi

Hii ni aina ya tiba inayotumia mionzi yenye nishati kubwa kuua seli zilizoathiriwa na saratani. Kwa kawaida tiba ya mionzi huathiri seli zilizo katika eneo linalotibiwa tu.

Aidha tiba ya mionzi inaweza pia kutumika kuua seli za saratani zilizobakia mara baada ya kufanyika kwa upasuaji au hata kabla ya upasuaji kufanyika. Mara nyingi tiba ya mionzi hutolewa pamoja na tiba ya kemikali (chemotherapy). Tiba ya mionzi inaweza kutolewa kwa kutumia mashine ya mionzi iliyo nje ya mwili (external radiation therapy) au kwa kuingiza mashine ya mionzi ndani ya koo na kuua seli zenye saratani (internal radiation therapy au brachytherapy).

Tiba ya mionzi inaweza kusababisha, mbali na kuua seli zenye saratani, madhara kama vile maumivu kwenye koo, maumivu kama kiungulia au maumivu kwenye tumbo au utumbo. Aidha wagonjwa wengine wanaweza kuharisha, kujihisi kichefuchefu, kuwa na ngozi kavu, ya moto na nyekundu, na kunyonyoka nywele sehemu iliyopigwa mionzi.

Tiba ya kemikali (Chemotherapy)

Aina hii ya tiba hutumia kemikali kuua seli zenye saratani. Kwa kawaida dawa hizi hutolewa kwa njia ya sindano kupitia kwenye mshipa wa damu wa vein. Aidha matibabu kwa njia hii hutolewa kwa awamu (cycles) huku kila awamu ikifuatiwa na kipindi cha mapumziko bila dawa. Madhara yanayoweza kusababishwa na njia hii ya matibabu hutegemea sana aina ya dawa husika. Baadhi ya madhara hayo ni

 • Kupungua kwa kiwango cha chembe za damu hali ambayo inaweza kusababisha mgonjwa kuwa katika hatari ya kupata maambukizi ya vijidudu kwa urahisi, kupata mikwaruzo na michubuko kirahisi, au kujihisi mchovu kila wakati.
 • Baadhi ya nywele za mwili hunyonyoka.
 • Kuathirika kwa seli zinazounda mfumo wa chakula na hivyo kusababisha mgonjwa kukosa hamu ya kula, kujihisi kichefuchefu, kutapika, kuharisha, na kutoka vidonda mdomoni.
 • Madhara mengine ni kama vile maumivu ya viungo, kuvimba miguu na vidole, kupata ganzi mikononi na vidoleni na matatizo ya kusikia.

Lishe na saratani ya koo

Lishe ni jambo la muhimu sana kwa mgonjwa wa saratani ya koo. Chanzo kikuu cha vifo kwa wagonjwa wa saratani ya koo ni utapiamlo pamoja na upungufu wa kiwango cha sukari mwilini yaani hypoglycemia unaosababishwa na mgonjwa kushindwa kumeza chakula. Hivyo ni muhimu sana kuhakikisha mgonjwa anapata lishe kamili kwa ajili ya mwili.

Iwapo mgonjwa anashindwa kabisa kula, daktari anaweza kutumia njia kadhaa za kuhakikisha mgonjwa anapata chakula. Mojawapo ni ya kutumia bomba maalum la kupitishia chakula (feeding tube) katika koo ambalo husaidia kupitisha chakula mpaka kwenye tumbo.

Imesomwa mara 72710 Imehaririwa Jumapili, 24 Januari 2021 15:35
Dr Fabian P. Mghanga

Daktari bingwa na Mhadhiri katika kitivo cha Afya Chuo Kikuu Kishiriki cha Askofu Jacob, Songea

Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.

Makala shabihana