Image

Dalili za ujauzito hutofautiana kati ya mwanamke mmoja  na mwanamke mwingine, ingawa kuchelewa au kukosa hedhi ni dalili moja muhimu sana ya ujauzito.

Ni muhimu kuzitambua na kuzifahamu dalili hizi kwa sababu zinaweza kusaidia kujua kama kweli umeshika ujauzito au la  pamoja na kuweza kutofautisha matatizo mengine yanayoshahabiana kwa dalili na  ujauzito.

Hebu sasa tuangalie dalili na ishara za ujauzito:

  • Kutokwa damu kidogo ukeni wakati kiumbe kikipandikizwa kwenye mfuko wa uzazi, ingawa siyo wanawake wote hupatwa na dalili hii
  • Kukosa hedhi, hii ni moja ya dalili kubwa ya ujauzito
  • Maumivu kwenye matiti na kuvimba matiti (huweza kutokea kati ya wiki ya 1 hadi ya 2)
  • Uchovu, wanawake wengi huhisi uchovu na  na hali ya kutopenda kufanya lolote.
  • Kupoteza ladha au kuhisi ladha ya chuma mdomoni
  • Kuongezeka kwa hisia ya harufu, kipindi cha ujauzito wanawake wengi huongezeka hisia ya harufu
  • Kichefuchefu na kutapika
  • Maumivu ya kichwa
  • Kizunguzungu
  • Kukojoa mara kwa mara (hasa kati ya wiki 6-8)
  • Kubadilika rangi kwa ngozi inayozunguka chuchu kuwa nyeusi
  • Kutamani baadhi ya vyakula na kuchukia vingine
  • Kupanuka kwa mfuko wa uzazi
  • Tumbo kujaa au kuvimbiwa
  • Kununa na kukasirika haraka
  • Kiungulia au kupata choo kigumu
  • Kolostramu kuanza kutoka kwenye matiti 
  • Kuongezeka uzito
  • Kuweza kupapasa mtoto (palpation of the baby)
  • Kulainika na kuvimba kwa shingo ya uzazi (Hegars sign) - kuanzia wiki ya 6
  • Shingo ya uzazi kubadilika rangi kuwa ya samawati kutokana na msongamano wa damu katika mishipa ya vena. Ishara hii hujulikana kama Chadwick's sign

Dalili nyingine ni pamoja na

  • Mstari wima mweusi hutokea tumboni kuanzia chini ya kitovu (linea nigra)
  • Mama kuhisi mtoto akicheza (kuanzia wiki ya 20)
  • Maumivu ya mgongo hasa mimba ikishakuwa kubwa.
  • Kipimo cha mimba kuwa chanya (positive).
  • Kusikia mapigo ya moyo ya mtoto
  • Mtoto kuonekana kwenye kipimo cha ultrasound

Katika makala itakayofuata tutaangalia vipimo muhimu vya kudhibitisha uwepo wa ujauzito. Usikose...

Imesomwa mara 51699 Imehaririwa Jumanne, 01 Mai 2018 17:50
Dr.Mayala

Dr.Henry A Mayala ni daktari bingwa Wa Tiba ya moyo katika taasisi ya Jakaya Kikwete Cardiac Institute (JKCI), ambaye kwasasa anasomea shahada ya uzamivu (PhD) ya Tiba ya Moyo katika Chuo Kikuu cha Tongji  nchini China.

Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.

Makala shabihana