Image

Sababu zinazomruhusu mama mjamzito kutoa mimba (Induced Abortion)

Sio siri duniani kuna baadhi ya nchi ambazo zimeruhusu mama mjamzito kufanya uamuzi wa kutoa mimba (abortion) bila kuwepo kwa sababu zozote za msingi za kitabibu. Baadhi ya nchi hizo ni Marekani, Canada, Visiwa vya Guyana, Bahrain (isizidi umri wa mimba wa wiki 12),Uturuki, China, Singapore, Ubelgiji, Uswisi, Uholanzi nk. Kwa bara la Afrika ni nchi mbili tu ambazo zimeruhusu mama mjamzito kufanya uamuzi huu ambazo ni Afrika Kusini na Tunisia. Katika nchi hizi mbili za kiafrika, mama mjamzito ataruhusiwa kutoa mimba (abortion) iwapo mimba itakuwa na umri wa chini ya wiki 12 za umri wa mimba.

Suala la utoaji mimba bado haliruhusiwi katika mataifa mengi duniani isipokuwa tu pale panapokuwa na sababu za msingi za kitabibu ambazo zinaruhusu mimba hiyo iharibiwe/itolewe (abortion) pasipo mhusika/mama mjamzito kukumbana na mkono mkali wa sheria. Jamhuri ya muungano wa Tanzania ikiwa ni moja za nchi hizo ambazo haziruhusu mama mjamzito kutoa mimba ila pale tu kuna  sababu za msingi za kitabibu zinazoruhusu mama mjamzito kufanya hivyo.

Kuharibu/kutoa mimba kutokana na sababu za kitabibu ambazo kama mama ataendelea kubeba  ujauzito huo  hadi kipindi cha kujifungua  basi atahatarisha maisha yake mwenyewe au maisha ya kiumbe alichobeba ndio hujulikana kitaalamu kama induced abortion.

Leo tutaangalia sababu zinazompa mama haki ya kutoa mimba bila kukumbana na mkono wa sheria.Sababu hizi zimegawanyika katika makundi mawili

 • Sababu kwa upande wa mama
 • Sababu kwa upande wa mtoto

Kwa upande wa mama sababu  hizi  ni kama zifuatazo

 • Magonjwa ya moyo kama ugonjwa wa presha, ugonjwa wa presha wa mishipa ya palmonari (Pulmonary hypertension), kuwepo kwa historia ya mama kupata ugonjwa wa moyo unaosababishwa na ujauzito (Pregancy induced cardiomyopathy) na Eisenmenger's syndrome.
 • Magonjwa ya jenetikali/asili kama marfan syndrome
 • Ugonjwa wa mfumo wa damu kama Thrombotic thrombocytopenic purpura
 • Magonjwa ya mfumo wa fahamu (Neurological disease)-Kutotibiwa kwa ugonjwa wa mfumo wa damu wa ubongo (Untreated cerebrovascular malformations) kama aneurysm au arteriovenous malformation
 • Ugonjwa wa figo-Kupungua kwa uwezo wa figo kufanya kazi mwanzoni kabisa mwa kipindi cha ujauzito
 • Saratani-Saratani ya shingo ya kizazi (Cervical cancer) au saratani yoyote ile ambapo tiba ya mama inahusu kutumia dawa za saratani (chemotherapy) au kupewa tiba ya mionzi ya saratani (radiotherapy)
 • Magonjwa ya mfumo wa umengenyaji chakula (Metabolic disease)-Proliferative diabetic retinopathy
 • Magonjwa yanayohatarisha uhai wa mama-Saratani zilizopo kwenye hatua ya mwisho kuchukua uhai wa mama (Terminal cancers),hatua ya mwisho ya ugonjwa wa upungufu wa kinga mwilini (End stage AIDS)
 • Matatizo yanayotokana na mimba aliyobeba mama-Maambukizi ya kiumbe kipindi cha ujauzito (Intrauterine infections),kupasuka kwa chupa kabla kutimia kwa umri wa kujifungua kwa mtoto (Rupture of the fetal membranes before fetal viability), kifafa hatarishi cha mimba (Severe pre-eclampsia or eclampsia).
 • Ujauzito ambao unaweza kusababisha madhara makubwa kwenye mfuko wa uzazi -Mapacha walioungana (conjoined twins), historia ya kuchanika kwa kizazi hapo awali (prior history of catastrophic uterine rupture),tatizo la kondo la nyuma la uzazi linalojulikana kama Placenta
 • Ujauzito unaoambatana na saratani-Trophoblastic disease
 • Mimba mfu-Mtoto kufariki ndani ya tumbo (Fetal death in utero), mimba isiyokuwa na kiinitete inayojulikana kama anembryonic pregnancy (“empty sac” or “blighted ovum”), mimba ambayo ina hatari kubwa ya kutoka/kuharibika (Inevitable abortion).
 • Kwa upande wa mtoto sababu hizi ni kama zifuatazo

  • Magonjwa yanayojulikana ya kuzaliwa nayo mtoto (known major fetal malformation)- Kutokukuwa kwa mfumo wa mkojo vizuri (Renal agenesis), kichwa kujaa maji (Severe hydrocephaly), kichwa kidogo (Anencephaly), matatizo katika ukuaji wa moyo (Severe cardiac anomaly), Myelomeningocele nk.
  • Magonjwa ya vina saba (chromosomal abnormalities)-Down's syndrome, other trisomies, Fragile X, X-linked recessive disease kama hemophilia
  • Magonjwa ya kurithi ya mfumo wa umengenyaji chakula (Inherited metabolic defect) - Duchenne muscular dystrophy, Tay-Sachs disease
  • Mama kutumia dawa aina ya Warfarin,Thalidomide, Isotretoin, dawa za aina yoyote ile za saratani nk, hivyo kumuweka mtoto kwenye hatari ya kupata madhara mbalimbali.
  • Mama kupewa tiba ya mionzi ya magonjwa ya saratani- dozi ya 15 rad au zaidi, kutumia tiba ya Radioactive iodine
  • Mama kupata maambukizi kipindi cha ujauzito-Maambukizi ya Rubella, Cytomegalovirus, Toxoplasmosis,virusi hatari vya ugonjwa wa zika (zika virus)

  Mjamzito ambaye atapata dozi ya mionzi ya kiwango cha 5 rad kwenye maeneo ya nyonga au tumbo mwanzoni mwa ujauzito wake anaweza kutoa mimba hiyo (abortion) au kuendelea kulea ujauzito wake mpaka pale atakapojifungua ikiwa yupo tayari kukabiliana na madhara ambayo mtoto wake atapata kutokana na mama kukumbana na kiwango hiki cha mionzi 1 .

  Kiwango hiki cha  mionzi cha 5 rad ndio kiwango cha juu cha mionzi kinachoruhusiwa kukumbana na mjamzito, lakini hii haimanishi ya kwamba mjamzito atakapokumbana na kiwango hiki cha mionzi ( 5 rad) hawezi kupata kupata mtoto aliyeathirika na mionzi, la hasha, hiki kiwango ni tahadhari ambayo mjamzito au daktari wake anapaswa ahakikishe kwamba mama huyu hafiki au kupita kiwango hiki  cha  (5 rad) wakati wa kufanya vipimo vyake vyote kipindi cha ujauzito.Dozi ya mionzi zaidi ya  5 rad ni hatari  sana kwani mama mjamzito anaweza kuzaa mtoto mwenye saratani mbalimbali ambazo ni moja ya madhara ya mionzi  wakati wa ujauzito.

  Ni vyema kwa daktari kumuelimisha mama mjamzito juu ya madhara  ya mionzi kwa wajawazito iwapo kuna ulazima wa kufanya vipimo venye kutoa dozi kubwa ya mionzi.

  Kuomba ushauri wa kitaalamu kutoka kwa wataalamu wa fani ya jenetikali ni jambo la busara kabla ya daktari kufikia uamuzi wa kutoa mimba.Mama mjamzito mwenye tatizo la afya ambalo halina madhara makubwa sana kwake au kwa mtoto na ambalo ni mojawapo za sababu za kitabibu za kuruhusiwa kwake kutoa mimba, anaweza pia kuamua mimba yake itolewe kutokana na hisia zake juu ya ujauzito huo (wasiwasi kwamba atapata mtoto ambae ameathirika kwa madhara ya ugonjwa wake/wasiwasi   kuhusu utayari wake wa  kumlea na kumhudumia mtoto mwenye madhara au  wasiwasi kuhusu ujauzito huo kumsumbua au hata kuhatarisha maisha yake ).

  Vipimo kabla ya kutolewa mimba

  • Urine for pregnancy test (UPT)-Kipimo cha mkojo cha kutambua uwepo wa ujauzito
  • Kipimo cha Ultrasound-Kujua umri wa mimba, uwepo wa mimba, kufahamu iwapo viungo vya ndani vya mama ni kamilifu na havina tatizo lolote lile
  • Kipimo cha X-ray-Kuangalia kama mama mjamzito ana tatizo lolote lile la moyo (kwa wale watakaochagua njia ya upasuaji) kama cardiomyopathy, moyo mkubwa (cardiomegally), tatizo la moyo linalotokana na ugonjwa wa presha
  • Kupima presha (Blood Pressure monitoring) hasa kwa wale watakaochagua njia ya upasuaji
  • Kipimo cha mapigo ya moyo (Pulse rate)

  Kabla ya mimba kutolewa, mama mjamzito atahitaji kufanyiwa vitu vifuatavyo;

  Ushauri nasaha unaolenga

  • Kumpa maelezo yanayotosheleza kuhusu utoaji mimba
  • Kuelimishwa jinsi ya kukabiliana na hisia zake
  • Kumuondolea mama mjamzito wasiwasi
  • Kumjengea ufahamu wa kuepuka mimba zisizohitajika (unplanned pregnancies)
  • Kumshauri njia za uzazi wa mpango
  • Kuelemishwa kuhusu njia za utoaji mimba, faida na madhara yake-Hii humsaidia mjamzito pamoja na daktari wake kushirikiana  kuchagaua njia itayomfaa mama  ya utoaji mimba.

  Kuna aina mbili za utoaji mimba kwa mama mjamzito nazo ni

  • Njia ya kutumia dawa za kutolea mimba (medical abortion)
  • Njia ya upasuaji (Surgical abortion)

  Ni vizuri kumfahamisha mama mjamzito ni kwa muda gani maumivu yatakuwepo baada ya kutolewa mimba pamoja na matibabu yake kwani wengi wao huwa na wasiwasi na uoga juu ya maumivu watakayopata wakati na baada ya utoaji mimba. 

  Mama mjamzito kusaini fomu ya kuruhusu daktari kutoa mimba yake (consent form). Hii itamsaidia mjamzito na daktari wake iwapo kutatokea tatizo lolote lile ambalo halikutarajiwa wakati au baada ya utoaji mimba. Kuhakikishiwa utunzaji wa taarifa zake za utoaji mimba. Kwamba taarifa zake hazitapewa/kutolewa kwa mtu  mwingine yoyote  bila ruhusa yake mama mjamzito (presumption of confidentiality). Hiki ni kipengele muhimu sana katika maadili ya udaktari.  

  Tuangalie njia  hizi za utoaji mimba

  Utoaji mimba kwa kutumia dawa za kutolea mimba (Medical abortion)

  Kuna tofauti ndogo sana ya madhara na usalama wa njia hizi mbili  za kutoa mimba (njia ya kutumia dawa na ya upasuaji)

  Njia ya kutoa mimba kwa kutumia dawa hufanyika ikiwa mama mjamzito

  • Amechagua mwenyewe njia hii
  • Ana mimba yenye umri mdogo sana-Chini ya siku 49 za umri wa mimba
  • Ana uzito uliopitiliza (Basal Metabolic Index kuanzia 30 na zaidi) na hana ugonjwa au tatizo lolote la moyo
  • Hana tatizo lolote kwenye maumbile ya mfuko wa uzazi (uterine malformations)
  • Ana uvimbe kwenye mfuko wa kizazi (fibroid)
  • Aliwahi kufanyiwa upasuaji wa shingo ya kizazi (Cervical surgery)
  • Anataka kuepuka njia ya upasuaji

  Madhara ya utoaji mimba kwa kutumia dawa

  • Kuvuja damu kutoka kwenye tupu ya mwanamke (Hemorrhage)
  • Mimba kutotoka yote (Incomplete abortion)
  • Maambukizi kwenye mfuko wa uzazi au kwenye mirija ya uzazi (uterine/pelvic infection)
  • Kuendelea kwa uhai wa mimba na hivyo kulazimu mjamzito kutolewa mimba kwa njia ya upasuaji
  • Kutotambulika/kugundulika kuwa mimba imetunga nje ya mfuko wa uzazi (ectopic pregnancy)

  Kutoa mimba kwa njia ya upasuaji (Surgical abortion)

  Njia hii hutumiwa iwapo mama mjamzito

  • Amechagua mwenyewe
  • Anapata madhara akitumia dawa za kutolea mimba mfano tatizo la mzio (allergic reactions)
  • Hana muda au anaishi mbali na hospitali hivyo kushindwa  kurudi hospitali  kwani njia ya kutoa mimba kwa kutumia dawa inahitaji mgonjwa kurudi kwa uchunguzi zaidi ili daktari ahakikishe mimba yote imetoka na hakuna mabaki ya mimba hiyo. 

  Madhara ya utoaji mimba kwa upasuaji

  • Kuvuja damu kutoka kwenye tupu ya mwanamke (Hemorrhage)
  • Mimba kutotoka yote (Incomplete abortion)
  • Maambukizi kwenye mfuko wa uzazi au kwenye mirija ya uzazi (uterine/pelvic infection)
  • Kuendelea kwa uhai wa mimba na hivyo kulazimu mjamzito kutolewa mimba kwa njia ya upasuaji
  • Kutotambulika/kugundulika kuwa mimba imetunga nje ya mfuko wa uzazi (ectopic pregnancy)
  • Mabonge ya damu kujikusanya ndani ya mfuko wa uzazi (Hematometra)
  • Kutoboka kwa mfuko wa uzazi (uterine perforation)
  • Kupata madhara kwenye shingo ya kizazi (cervical laceration)
  Imesomwa mara 4732 Imehaririwa Jumatatu, 11 Juni 2018 12:32
  Dr Khamis

  Dr. Khamis H.Bakari (MD PhD) ni daktari bingwa,mhadhiri katika chuo cha afya cha Chuo  Kikuu cha Dodoma,mtaalamu wa Tiba na Uchunguzi kwa kutumia mionzi ya nyuklia (Nuclear medicine).

  Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.