Image

Hali ya tumbo kuuma wakati wa hedhi huitwa dysmenorrhea.

Zipo aina mbili za hali hii.

Aina ya kwanza ni maumivu yanayoanza tangu umri wa kuvunja ungo. Katika aina hii huwa hakuna ugonjwa unaosababisha uwepo wa haya maumivu. Hali hii hupona hata bila matibabu baada ya mizunguko kadhaa ya hedhi au baada ya kujifungua. Aina hii inaitwa primary dysmenorrhea (tuiite maumivu ya awali).

Aina ya pili mara nyingi hutokea miaka kadhaa baada ya kuvunja ungo. Aina hii husababishwa na ugonjwa wa viungo vya uzazi. Iwapo ugonjwa huo utatokea kabla msichana hajavunja ungo basi maumivu yanaweza kuanza kuanzia umri wa kuvunja ungo. Maumivu yaliyosababishwa na uwepo wa ugonjwa hayaponi bila kuutibia ugonjwa ulioyasababisha.

Magonjwa yanayoweza kusababisha maumivu ya hedhi ni fibroids, infection, uvimbe ndani ya kifuko cha uzazi (polyp) na ugonjwa unaoitwa endometriosis na adenomyosis. Ugonjwa wa endometriosis na adenomyosis upo Tanzania lakini hausikiki kwa sababu vituo vingi vya huduma havina vifaa vya kugundua uwepo wake. Nitaufafanua kwa kirefu kwenye topic yake.

Msichana au mwanamke mwenye maumivu ya hedhi anatakiwa kumuona daktari kwa ajili ya vipimo na ushauri wa matibabu.

Matibabu

Zipo njia nyingi ya kutibia maumivu ya hedhi.

Mojawapo ni kuweka chupa au mfuko wenye maji ya moto kwenye sehemu ya chini ya tumbo (isiwe moto mkali wa kuunguza ngozi).


Dawa za kutuliza maumivu kama ibuprofen, mefenamic acid, naproxen.


Matumizi ya vidonge vya uzazi wa mpango pia husaidia kupunguza maumivu ya hedhi. Kama ilivyo kwa dawa nyingine, ni muhimu kupata ushauri wa kitaalam kabla ya kuanza kutumia dawa hizi. 

Iwapo njia hizi hazifanikiwi kutuliza maumivu ya hedhi, vipimo zaidi vinahitajika ili kugundua chanzo cha maumivu hayo.

Miongoni mwa vipimo vinavyohitajika ni vipimo vya magonjwa ya infection ya njia ya uzazi pamoja na upasuaji ili kuona uwepo wa endometriosis na kuiondoa (picha zinaonyesha jinsi upasuaji huo unavyofanyika kwa matundu madogo na kamera bila kafungua tumbo).

Iwapo maumivu ni makali sana na hayatibiki kwa dawa, mgonjwa asiyekuwa na mpango wa kupata mtoto hushauriwa kuondoa kifuko cha uzazi.

  

Imesomwa mara 9266 Imehaririwa Ijumaa, 03 Agosti 2018 09:01
Dr Khamis

Dr. Khamis H.Bakari (MD PhD) ni daktari bingwa,mhadhiri katika chuo cha afya cha Chuo  Kikuu cha Dodoma,mtaalamu wa Tiba na Uchunguzi kwa kutumia mionzi ya nyuklia (Nuclear medicine).

Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.

Makala shabihana