Image

Kuvimba kwa Tezi ya Thyroid (Goiter)

Goita (Goiter) ni hali ya kuvimba kwa tezi ya thyroid. Uvimbe huu hautokani na saratani na kwamba goita si saratani. Tezi ya thyroid ipo sehemu ya mbele ya shingo. Kazi kuu za tezi ya thyroid ni kuzalisha homoni mbalimbali ambazo husaidia mwili kuthibiti na kufanya kazi zake mbalimbali.

Aina za goita na visababishi vyake

Kuna aina kadhaa za goita. Goita ya kawaida (simple goiter) inaweza kutokea bila kuwepo kwa chanzo chochote cha kueleweka. Wakati mwingine, yaweza kutokea wakati tezi ya thyroid inaposhindwa kuzalisha homoni/vichocheo vya kutosha vya thyroid kwa ajili ya mahitaji ya mwili. Ili kuweza kuendana na hali hii, tezi ya thyroid huongezeka ukubwa ili kufidia upungufu wa homoni za thyroid.

Kuna aina mbili za goita ya kawaida, Goita inayowapata wakazi wa eneo fulani (endemic goiter). Aina hii pia huitwa colloid goiter, na Goita inayotokea maeneo tofauti (sporadic goiter). Aina hii pia hujulikana kama nontoxic goiter.

Endemic goiter au colloid goiter huwapata makundi ya watu wanaoishi maeneo yenye udongo wenye upungufu mkubwa wa madini ya Iodine. Maeneo ya aina hii mara nyingi ni yale yaliyo mbali kutoka pwani ya bahari au yaliyo katika nyanda za juu kutoka usawa wa bahari kama vile mikoa ya Mbeya, Iringa na Rukwa. 

Iodine ni madini muhimu yanayohitajika katika utengenezaji wa homoni mbalimbali zinazozalishwa na tezi ya thyroid. Watu wanaoishi kwenye maeneo kama haya wapo katika hatari ya kupata goita kwa vile hawapati madini ya kutosha ya Iodine katika chakula chao.

Matumizi ya chumvi ziliongezwa madini ya Iodine yamesaidia sana kupunguza matatizo ya upungufu wa Iodine miongoni mwa watu wengi nchini Tanzania na duniani kwa ujumla. Hata hivyo, upungufu wa madini ya Iodine bado umeendelea kuzikumba sehemu nyingi za Afrika ya kati, Amerika ya kusini pamoja na Asia ya kati.

Chanzo cha sporadic goiter au nontoxic goiter bado hakifahamiki vema miongoni mwa wagonjwa wengi. Hata hivyo, matumizi ya baadhi ya dawa kama vile lithium pamoja na aminoglutethimide yameelezwa kuwa chanzo kimojawapo cha aina hii ya goita.

Vihatarishi vya goita

Kuna baadhi ya mambo yanayohusiana na kurithi yanayoweza kusababisha mtu kupata goita. Vihatarishi hivi ni pamoja na:
•    Kuwa na umri kuanzia miaka 40 na kuendelea
•    Historia ya ugonjwa wa goita miongoni mwa wanafamilia
•    Hali ya kuwa mwanamke
•    Na, kutopata iodine ya kutosha katika lishe

Dalili za goita

Dalili kuu ya goita ni kuvimba au kuongezeka ukubwa kwa tezi ya thyroid. Ukubwa wa tezi unaweza kuwa kijiuvimbe kidogo katika tezi au uvimbe mkubwa kama nundu sehemu ya mbele ya shingo. Kuvimba kwa tezi ya thyroid kunaweza kusababisha mgandamizo katika njia ya hewa na mrija wa chakula, hali ambayo inaweza kusababisha:
•    Shida katika kupumua
•    Kikohozi
•    Sauti kuwa ya mikwaruzo
•    Shida wakati wa kumeza chakula
•    Wakati mwingine, mishipa ya damu ya shingoni inaweza kuvimba pia na kusababisha mtu kujihisi kizunguzungu pindi anapoinua mikono yake juu

Uchunguzi na vipimo

Ili kuweza kutambua iwapo mgonjwa ana uvimbe kwenye tezi ya thyroid, daktari huchunguza shingo ya mgonjwa pindi anapojaribu kumeza mate yake ili kuona kama kuna uvimbe unaopanda na kushuka wakati mgonjwa anapojaribu kumeza. Daktari pia hupapasa sehemu za mbele za shingo ili kuchunguza iwapo kuna uvimbe wowote maeneo hayo.

Vipimo ni pamoja na:

•    Kupima kiwango cha homoni ya thyroxine (free thyroxine fT4)
•    Kupima kiwango cha homoni inayochochea tezi ya thyroid kuzalisha homoni nyingine yaani Thyroid stimulating hormone (TSH)
•    Ultrasound ya tezi ya thyroid. Ikiwa vivimbe (nodules) vitaonekana wakati wa kufanya ultrasound, mgonjwa hana budi kufanyiwa biopsy (kukata sehemu ya vivimbe hivyo) kwa ajili ya uchunguzi wa kimaabara ili kujiridhisha kuwa mgonjwa hana matatizo ya saratani ya thyroid.
•    Mgonjwa pia anaweza kufanyiwa uchunguzi wa tezi ya thyroid kwa kutumia  teknolojia ya mionzi ya nuklia yaani thyroid scan ambayo, pamoja na mambo mengine husaidia kuonesha jinsi tezi ya thyroid inavyofanya kazi (thyroid uptake)

Matibabu

Goita huitaji matibabu iwapo tu inasababisha dalili zinazomletea mgonjwa usumbufu. Matibabu ya goita hujumuisha:
•    Matumizi ya madini ya mionzi ya iodine (radioactive iodine) yaani I-131 kwa ajili ya kupunguza ukubwa wa tezi ya thyroid hususani iwapo tezi hiyo inazalisha kiasi kikubwa cha homoni
•    Upasuaji wa kuondoa tezi yote yaani (total thyrodectomy) au kuondoa sehemu ya tezi (partial thyrodectomy)
•    Iwapo goita inasababishwa na upungufu wa madini ya Iodine, mgonjwa anaweza kupewa kiasi kidogo cha dawa ya maji aina ya Lugol's iodine au mchanganyiko wa potassium iodine
•    Iwapo goita inasababishwa na tezi ya thyroid inayofanya kazi chini ya uwezo wake, mgonjwa anaweza kupewa homoni za thyroid ili kufidia upungufu wowote

Matarajio

Goita ya kawaida inaweza kuisha yenyewe au inaweza kuendelea kuongezeka ukubwa mpaka kumsababishia mgonjwa usumbufu. Kadiri uharibifu wa tezi ya thyroid unavyoendelea, hufikia wakati tezi hii huacha kabisa kutengeneza homoni hali inayoitwa kwa kitaalamu hypothyroidism. Mara chache, goita inaweza kubadilika na kuanza kuzalisha homoni za thyroid bila kuchochewa na kitu chochote. Hali husababisha kuwepo kwa kiasi kikubwa cha homoni za thyroid, hali inayoitwa kitaalamu kama hyperthyroidism.

Madhara ya goita

•    Shida wakati wa kumeza au kupumua
•    Kiwango cha chini cha homoni za thyroid (Hypothyroidism)
•    Kiwango cha juu cha homoni za thyroid (Hyperthyroidism)
•    Saratani ya tezi ya thyroid (thyroid cancer)
•    Goita yenye vivimbe inayozalisha homoni kwa wingi (toxic nodular goiter)

Kinga

Matumizi ya chumvi ya mezani iliyowekwa madini ya iodine husaidia kuzuia uwezekano wa kupata goita. Aidha inashauriwa kumuona daktari au mtaalamu wa afya pindi unapoona kuna uvimbe wowote sehemu za mbele za shingo.

 

Picha ya Goit kwa hisani ya http://malipeds.blogspot.com/

Imesomwa mara 44427 Imehaririwa Jumamosi, 08 Aprili 2017 14:40
Dr Fabian P. Mghanga

Daktari bingwa na Mhadhiri katika kitivo cha Afya Chuo Kikuu Kishiriki cha Askofu Jacob, Songea

Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.

Makala shabihana