Image

Je kukojoa baada ya tendo la ndoa kunapunguza uwezo wa kupata ujauzito?

Siku hizi, kumekuwa na taarifa nyingi juu ya masuala ya uzazi. Taarifa hizi hutokana na imani tofauti zilizopo kwenye jamii. Na, nyingi ya imani hizi hazina uhakika wa kitaalamu. Moja ya imani ni kutokukojoa kwa mwanamke baada ya tendo la ndoa ili kuzuia mbegu za kiume kutoka.

Kukojoa baada ya kufanya tendo la ndoa ni njia mojawapo inayotumiwa na wengi kusaidia kupunguza uwezekano wa kupata maambukizi ya njia ya mkojo (UTI).  Na inashauriwa sana kukojoa punde baada ya tendo la ndoa ili kujikinga na uwezekano wa kuambukizwa ugonjwa wa UTI kama anavyoelezea Dr. Leah Millheiser . Hivyo, kama na wewe ni mmoja wapo, basi unaweza kuendelea. Kukojoa baada ya tendo la ndoa hakuwezi kupunguza uwezekano wako wa kupata ujauzito.

Wakati wa tendo la ndoa, kuna mbegu kati ya milioni 20 hadi 400 hutotelwa na mwanamume kwenye manii (semen) kwa pamoja , na inakadiriwa kuwa mpaka 65% ya mbegu hufanikiwa kutoka kwenye bao na kuingia kwenye mlango wa uke ikisaidiwa na majimaji ya ukeni yanayotoka wakati wa tendo la ndoa (vaginal discharge) au kwa kitaalamu cervical mucus.

Asilimia kubwa ya mbegu hizi hupenya kwenye lango la uzazi wa mwanamke na kuacha sehemu kubwa ya manii ikiwa na maji maji mengine ambayo yana kiasi kidogo sana cha mbegu za kiume /shahawa (kumbuka manii za mwanamume zinajumuisha vitu vingi vingine zaidi ya shahawa  kama protini , ute wa kusaidia shahawa kuelea au kwa kitaalamu  Seminal fluid nk). Kwenye kila manii (bao) moja la mwanamume (manii yote unayoiona), inakadiriwa  kuwa ni 1% tuu ndiyo shahawa / mbegu za mwanamume, hivyo unapoona kama manii zinamwagika, sehemu kubwa siyo mbegu bali ni majimaji mengine yanayotumika kwenye kuhifadhi mbegu za mwanamume.

Kumbuka: Shahawa(sperms) ni sehemu ya manii (semen ) inayotoka wakati mwanamume akifika kilele. Shahawa huelea kwa kutumia kimiminika kiitwacho Seminal fluid  inayopatikana kwenye manii, Hivyo, siyo maji yote ya kwenye manii ni shahawa.

Kimsingi, mpaka muda anaenda kukojoa, mbegu huwa zimeshafika kwenye lango la uzazi, (cervix) hivyo kiasi kidogo sana cha mbegu zilizoshindwa kutoka kwenye manii ndiyo huendelea kubaki kwenye majimaji ambayo yatatoka dakika au masaa kadhaa baada ya tendo la ndoa.

Imesomwa mara 30294 Imehaririwa Jumatatu, 14 Januari 2019 15:16
Dr Khamis

Dr. Khamis H.Bakari (MD PhD) ni daktari bingwa,mhadhiri katika chuo cha afya cha Chuo  Kikuu cha Dodoma,mtaalamu wa Tiba na Uchunguzi kwa kutumia mionzi ya nyuklia (Nuclear medicine).

Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.