Katika miaka ya hivi karibuni, kama wewe ni daktari, mfanyakazi wa kada ya afya,binti au kijana hasa wa miaka 15-24 ni dhahirikabisa jina la P2 si ngeni masikioni mwako. Dawa hii imejizoelea umaarufu mkubwa miongoni mwa mabinti hasa wa umri tajwa kama ni njia kuu ya kuzuia kupata ujauzito. Ingawa dawa hii inaweza kuwa na manufaa yaliyokusudiwa, lakini matumizi yasiyo sahihi huweza kuleta madhara makubwa ukizingatia wengi wanaotumia hawana uelewa mpana juu yake.
Kwa uzoefu niliopata nikiwa kazini mabinti wengi wanaotumia dawa hii ni wale ambao bado hawapo kwenye ndoa lakini wamekuwa wanashiriki tendo na wenza wao, pia, wapo wanawake wachache ambao wapo kwenye ndoa lakini wanatumia P2 kama ni sehemu ya uzazi wa mpango.
Ukweli ni kuwa, mabinti wengi wanaotumia dawa hii ya P2 hujikuta wakitumia kwa sababu;
- Hupatikana kwa urahisi katika maduka mengi ya dawa baridi, na huuzwa bila ya maswali mengi ya ‘kwanini kwanini’-unalipa- unapewa dawa-unaondoka.
- Kutokana na kuona aibu ya kuonekana wanashiriki tendo kabla ya ndoa, mabinti wengi wanaogopa kuhudhuria vituo vya afya kupata ushauri wa uzazi salama na uzazi wa mpango, wengi wao huwa na hofu ya kunyanyapaliwa au kukutana na ndugu wanaowafahamu hivyo kuzua taharuki kwenye familia- kuwa sasa binti huyu ameanza kujihusisha na mapenzi- kumbuka kuwa watumiaji wengi ni kuanzia miaka 15 mpaka 24 (inawezekana ikawa chini au zaidi ya umri huo pia) wengi wao bado hawapo kwenye ndoa.
P2 ni nini:
P2 ni kifupi cha dawa (Postinor-2) hii ni dawa/kidonge kilicho na vichocheo vya homoni kwa ajili ya kuzuia mimba zisizotarajiwa (emergency contraceptive pills) au wengine huita (morning after pills).
Hii ni kati ya dawa nyingi za namna hii ambazo huzuia mwanamke asipate ujauzito inapotokea amefanya mapenzi wakati wa siku za hatari (fertile days) bila kutumia kinga au alitumia kinga (kondomu) ambayo labda ilipasuka (kuachana mkeka) wakati wa tendo na akawa na hofu ya kupata ujauzito.
Dawa hii hushauriwa kutumika si zaidi ya masaa 72 toka mwanamke aliposhiriki tendo la ndoa. Pakiti moja huwa na vidonge viwili ambapo kimoja kinatakiwa kunywa mara tu na kingine hutumia masaa 12 baada ya kunywa kidonge cha kwanza. Ifahamike kuwa vichocheo vya homini katika dawa hizi ni vya kiwango cha juu sana kulinganisha na vidonge vingine vya homini vya kuzuia mimba vya muda mrefu.
Je P2 hufanyaje kazi:
Vidonge hivi hufanya kazi kwa namna kadhaa:
- Hatua ya kwanza kabisa ni kufanya yai lichelewe kupevuka hivyo kuchelewesha uwezekano wa haraka wa kukutana na mbegu na kurutubishwa.
- Pili hufanya ute ute wa ukeni kuwa mzito hivyo huzifanya mbegu za mwanamume (sperms) kushindwa kuogelea kwa haraka kulifuata yai kwa ajili ya kulipevusha. Unaweza kusoma makala ya jinsi gani yai linavyochavushwa hapa.
- Pia, Homoni zilizotolewa na dawa hii ya P2, huufanya mji wa mimba kutokuwa tayari kwa ajili ya kupokea yai lililorutubishwa hivyo huondoa uwezekano wa yao lililochavushwa kwenda kujishikiza tayari kwa ajili ya ukuaji.
Hivyo basi, dawa hii haiwezi kutumika kama dawa ya kutoa ujauzito (abortion) kwa mtu ambaye tayari ni mjamzito.
Faida
Ikitumiaka kwa namna sahihi inaweza kusaidia kuzuia ujauzito usiotarajiwa.
Madhara:
- Dawa hii inavichocheo vya homoni vya kiwango cha juu hivo havimpasi mtu kutumia mara kwa mara lasivyo inaweza leta madhara ya kuharibu utaratibu wa kifisiolojia wa upevukaji wa mayai kwani mara nyingi mwili wa binadamu hubadilika badilika kulingana mazingira, madhara ya mabadiliko haya ya kifisiolojia ni kama:
- Kuchelewa kupata ujauzito kutokana na mayai kutopevuka kwa wakati
- Kupata hedhi isiyotabirika
- Kupata hedhi nyingi kuliko kawaida
- Kutokupata hedhi kabisa
- Mimba kutunga nje ya kizani (ectopic pregnancy)
Mimba hutunga nje ya uzazi endapo mimba imetungwa nje ya mji wa mimba (uterus), mara nyingi hutokea kwenye mirija ya folopian ambapo uchavushwaji hutokea na yai lililochavushwa likashindwa kusafiri kwenda mji wa Mimba. Hii huchangiwa na mabadiliko ya Homoni ambapo P2 hufanya lakini ni nadra sana kutokea kwa sababu ya P2.
- Kuleta shida zaidi au dawa kutofanya kazi kwa usahihi kama utakuwa na magonjwa kama homa ya ini, moyo,figo,sukari au saratani-unatoka damu bila mpangilio-au kama unatumia dawa za muda mrefu kama vile dawa za kufubisha virusi vya ukimwi au dawa za kifaa hivyo ni salama zaidi kujua afya yako kwa ujumla au kuzungumza na mtaalam wa afya kabla ya kumeza/kutumia vidonge hivi.
Maudhi mengine yanaweza kutokea ni pamoja na kichefuchefu, kizunguzungu nk.
Mambo ya msingi ya kuzingatia:
P2 inatumika kuzuia mimba kwa dharura, hivyo haupaswi kuitumia kama njia ya kudumu au kunywa mara kwa mara kwa ajili ya kuzuia mimba- tafadhali kama unafanya hivyo basi tembelea kituo cha afya cha karibu kwa ushauri zaidi.
Hata kama umetumia P2, bad kuna uwezekano wa kupata ujauzito, hivyo kama umetumia P2 na ukakosa hedhi hedhi basi ni vizuri ukapima ujauzito. Watu wengi wanaotumia P2 na bado wakapata ujauzito huamua kufanya utoaji wa mimba kwa njia wanazozijua wao ambazo ni hatari zaidi. Unapogundua hali hiyo ni vyema kutembelea kituo cha afya kwa ushauri zaidi.
Lakini pia wanawake wengi wanasahau kuwa dawa hizi hazizuii magongwa ya zinaa kama vile HIV, Kisonono, Kaswende- hivyo kuwafanya waangalie upande mmoja wa afya yao na kuacha upande mwingine ambao pia ni hatari zaidi kwa faya yao ya uzazi kwa ujumla- kwa sababu magonjwa haya yasipotibika yanaweza kuleta athari kubwa kwenye via vya uzazi na kuleta madhara ya kutopata ujauzito ambao kwa sasa wanaukimbia.
Hivyo wazazi na walezi ni vizuri kuchukua hatua za makusudi kutenga muda wa kuongea na vijana wetu`kuhusu afya ya uzazi,kuwasikiliza, kutambua na kufuatilia mienendo yao kwa karibu.
Lakini pia serikali kwa kushirikiana na wahudumu wa afya pamoja na wizara ya elimu kuweka mazingira sahihi ili kuwasaidia vijana kuweza kupata elimu Rafiki ya afya ya uzazi pia uwoga au kunyanyapaliwa- wanapokuwa na uelewa sahihi inawasaidia kufanya maamuzi sahihi ambapo ni pamoja kujizuia kufanya tendo la ndoa kabla ya wakati au kijihusisha na mahusiano yanayoweza kuhatarisha afya yao kwa ujumla.
Safari ya kila mtoto kuzaliwa ni ya kipekee sana, lakini safari zote huanzia kwenye muungano wa yai la mwanamke (ovum) na mbegu ya kiume (sperm). Mchakato huu unaendelea kwa miezi tisa ndani ya mwili wa mwanamke, na hatimaye kuzaliwa kwa mtoto. Katika makala hii, tutafuatilia kwa karibu hatua zote muhimu katika safari ya kupevushwa yai na mpaka kuzaliwa kwa mtoto.
Upevukaji wa Yai
Kwa kawaida, mtoto wa kike huzaliwa akiwa na mayai yanayokadiriwa milioni 1 hadi 2. Kwa wakati huu wa utotoni, mayai haya huwa yamesinzia (dormant) hadi kufika kipindi cha kubalehe (kuvunja ungo). Baada ya kubalehe, na endapo hakuna changamoto yoyote katika mfumo wa uzazi, basi kila mwezi mwili wa mwanamke huruhusu mayai kadhaa kepevuka ndani ya mfuko wa mayai (Ovary).
Kwa mazingira ya kawaida (isipokuwa mapacha wasiofanana) yai moja tu lililo bora zaidi kati ya mengi yaliyopevuka ndiyo huruhusiwa kutoka (Ovulation) na yale mengine yaliyopevuka na hayaruhusiwa kutoka huliwa na mwili. Yai hili lililotolewa linapotoka kwenye mfuko wa mayai hupita kwenye mirija ya fallopian na kisha kufika katika mji wa mimba (uterus) tayari kwa ajili ya uchavushwaji (fertilization), yai hili lina uhai wa masaa kati ya 12 hadi 24, na ndio wakati mzuri kwa mbegu ya kiume kuungana nalo ili kutunga ujauzito.
Uchavushaji:
Wakati wa tendo la ndoa, mamilioni ya mbegu za kiume(sperm) huingia kwenye uke wa mwanamke na mbegu hizi huogelea kwa msaada wa kimiminika kilichopo kwenye manii kupitia kizazi hadi kwenye mirija ya fallopian katika kutafuta yai. Kati ya mbegu nyingi zilizofanikiwa kufika kwenye yai, ni mbegu moja tu yenye ubora zaidi ndiyo itafanikiwa kuingia kwenye yai la kike na hapa ndipo uchavushaji (Fertilization) inakuwa imekamilika.
Baada ya mbegu moja kuingia, yai hujifunga na kutoruhusu tena mbegu za kiume kuingia kwenye yai kwa ajili ya uchavushaji. Mchanganyiko huu wa yai na mbegu huunda seli moja inayoitwa zygote. Seli hii ndio mwanzo wa maisha mapya na ina mchanganyiko wa DNA kutoka kwa wazazi wote wawili. Kisayansi, mtoto huchukua 50% ya DNA kutoka kwa kila mzazi. Nusu kutoka kwa baba na nusu kutoka kwa mama.
Ndani ya DNA kuna vitu vinaitwa chromosomes, na kila binadamu ana chromosomes 46 tu, 23 kutoka kwa baba na 23 kutoka kwa mama.Kati ya hizi chromosomes 23, 22 zinafanana kabisa lakini chromosomes ya 23 huitwa Sex chromosome na ndio itakayo amua jinsia ya mtoto.
Endapo kwa sababu zozote zile, hakutokuwa na yai lililochavunshwa, basi ukuta ulioundwa ndani ya uterus kwa ajili ya mapokeo ya zygote huvunjika na ndiyo sababu kila mwezi mwanamke ambaye bado hajakoma siku hupata hedhi.
Upachikanaji:
Zygote huanza kugawanyika na kuunda seli nyingi zaidi huku ikitafuta mahali pakujipachika katika mji wa mimba. Kujipandikiza huku hutokea ndani ya siku 6 hadi 12 baada ya fertilization. Baada ya hatua hii kumalizika kikamilifu Kondo (placenta) huundwa na ndiyo tunaweza kusema kuwa mwanamke ana ujauzito. Mwili wa mwanamke huanza kutengeneza hormone ya HCG (Human Chorionic Gonadotropin) ambayo itaanza kuleta dalili za mimba.
Ukuaji wa Mtoto
Baada ya kujipachika, seli zile huanza kugawanyika na kujipanga ili kuunda viungo vya mtoto.
Katika wiki za mwanzo, mtoto anaitwa embryo. Baada ya wiki ya nane, mtoto anaitwa fetus.Fetus huendelea kukua na kutengeneza viungo vyote vya muhimu. Ujauzito umeganyika katika vipindi vitatu tangu fertilization hadi kujifungua. Vipindi hivi huitwa trimesters.
Trimester ya Kwanza (Wiki 1-12):
- Wiki 1-2: Fertilization hufanyika, na zygote huanza kugawanyika na kufanya implantation.
- Wiki 3-8: Mtoto anaitwa embryo na viungo vyote muhimu huanza kuundwa. Moyo huanza kudunda, ubongo na mfumo wa fahamu huanza kuundwa. Wakati huu ni muhimu sana mama apate madini ya folic acid ili kuhakikisha mifumo hii inaundwa kwa usahihi.
- Wiki 9-12: Mtoto anaitwa fetus sasa. Viungo vyote muhimu vimeundwa, na mtoto anaanza kufanya harakati ndogo ndogo huku viungo vikiendelea kukomaa na kuimarika.
Trimester ya Pili (Wiki 13-27):
- Wiki 13-16: Mtoto anakua kwa kasi, na mama anaweza kuanza kuhisi mtoto akisogea au kucheza tumboni.
- Wiki 17-20: Ngozi ya mtoto inakuwa laini, na nywele za kichwa zinaanza kukua. Wakaiti huu kipimo cha ultrasound kinaweza kuonyesha jinsia ya mtoto.
- Wiki 21-24: Mapafu ya mtoto yanaanza kukomaa, lakini bado hayajakamilika na mtoto akizaliwa wakati huu, hataweza kupumua mwenyewe.
Trimester ya Tatu (Wiki 28-40):
- Wiki 28-32: Mtoto anaendelea kukua na kuongezeka uzito. Mafuta huanza kujilimbikiza chini ya ngozi, lakini bado hayupo tayari kwa maisha nje ya mji wa wimba.
- Wiki 33-37: Viungo vyote vya mtoto vimemaliza kukua. Mpaka wiki ya 34 kukamilika, mapafu nayo yanakua tayari yamekomaa na mtoto anaweza kuzaliwa wakati wowote baada ya hapo na akawa na uwezo mkubwa wa kuendelea kuishi nje ya tumbo la mama.
- Wiki 38-40: Mtoto anazingatiwa kuwa amekomaa kikamilifu na anaweza kuzaliwa wakati wowote. Mtoto akizidi kukaa tumboni zaidi ya hapo ni hatari, na uchungu usipoanza wenyewe, harakati za kuanzisha uchungu zinaweza kuanzishwa ili mama na mtoto wote waweze kuwa salama.
Kuzaliwa:
Baada ya miezi tisa, mtoto atakuwa tayari kuzaliwa. Mchakato wa kuzaliwa huanza na uchungu (contractions), ambao husaidia kufungua njia ya kizazi. Njia inapofika sentimita 10 mama huanza kusukuma na mtoto hutolewa. Kuna sababu kadhaa zinazoweza kuzuia mama kujifungua kwa njia hii na kuhitaji njia mbadala ambayo ni ya upasuaji (Cesarean section). Baada ya mtoto kutoka, kitovu (umbilical cord) hukatwa na kisha kondo kutolewa.
Hitimisho
Uzazi ni safari ya kipekee yenye kustaajabisha, Kutoka kwa mchanganyiko wa yai na mbegu hadi kuzaliwa kwa mtoto mpya, kila hatua ni muhimu katika kuunda maisha mapya. Kwa kuelewa mchakato huu, tunaweza kufahamu zaidi umuhimu wa afya ya uzazi na kuunga mkono wanawake wajawazito katika safari hii ya ujasiri.
Unaweza kutumia TanzMED App kwa ajili ya kufuatilia ujauzito au kupanga ujauzito wako.
Wasiwasi kwa watoto ni jambo la kawaida na linaweza kujidhihirisha kwa njia nyingi tofauti. Ingawa hofu na wasiwasi ni sehemu ya ukuaji wa mtoto, wakati mwingine inaweza kuwa kali na kuathiri maisha yao ya kila siku. Katika makala hii, tutajadili kwa undani zaidi kuhusu wasiwasi kwa watoto, sababu zake, dalili, na njia za kukabiliana nayo.
Sababu za Wasiwasi kwa Watoto
Sababu za wasiwasi kwa watoto ni nyingi na zinaweza kuwa za kibinafsi, za mazingira, au mchanganyiko wa zote mbili. Baadhi ya sababu zinazosababisha wasiwasi kwa watoto ni pamoja na:
- Kukabiliana Matukio hasi : Matukio kama vile kushuhudia vurugu, kutengana na wazazi, au kubadilisha shule yanaweza kusababisha wasiwasi kwa watoto.
- Kurithi : Watoto ambao wana wazazi au ndugu walio na matatizo ya wasiwasi wana uwezekano mkubwa wa kupata matatizo haya pia.
- Unyanyasaji au Kudhalilishwa: Watoto wanaofanyiwa unyanyasaji wa kimwili, kihisia, au kingono wana uwezekano mkubwa wa kupata wasiwasi na matatizo mengine ya afya ya akili.
- Matatizo ya Kimwili: Matatizo ya kiafya sugu kama vile mzio (allergy) , pumu, au maumivu ya muda mrefu yanaweza kuchangia katika wasiwasi.
Dalili za Wasiwasi kwa Watoto
Dalili za wasiwasi kwa watoto zinaweza kutofautiana kulingana na umri na aina ya wasiwasi. Baadhi ya dalili za kawaida ni pamoja na:
- Dalili za Kimwili: Maumivu ya tumbo, kichwa, au misuli; matatizo ya kulala; na mabadiliko ya hamu ya kula
- Dalili za Kihisia: Kutokuwa na utulivu, kukasirika kwa urahisi, kulia mara kwa mara, na kujisikia kuwa na hofu kila wakati.
- Dalili za Tabia: Kuepuka shule au shughuli za kijamii, kuzingatia sana mambo mabaya, na kuwa na shida kuzingatia.
Aina za Wasiwasi kwa Watoto
Kuna aina nyingi za wasiwasi kwa watoto, lakini baadhi ya aina za kawaida ni pamoja na:
- Wasiwasi wa Kutengana (separation anxiety disorder): Hofu ya kutengana na wazazi au walezi.
- Phobia Mbali mbali: Hofu kali ya vitu au hali maalum kama vile wanyama, giza, au urefu.
- Wasiwasi wa Jamii: Hofu ya kukataliwa au kuhukumiwa (judged) na wengine katika hali za kijamii.
- Wasiwasi wa Jumla: Wasiwasi wa mara kwa mara kuhusu mambo mbalimbali.
- Mashambulizi ya Hofu: (panic attack) Vipindi vifupi vya hofu kali na dalili za kimwili kama vile kupumua kwa kasi na kutetemeka.
Njia za Kukabiliana na Wasiwasi kwa Watoto
Kuna njia nyingi za kukabiliana na wasiwasi kwa watoto, na matibabu bora itategemea sababu na ukali wa tatizo. Baadhi ya njia za kawaida ni pamoja na:
- Cognitive behaviour therapy: Hii ni aina ya tiba inayomfundisha mtoto jinsi ya kutambua na kubadilisha mawazo na tabia zinazosababisha wasiwasi.
- Dawa: Katika baadhi ya hali, dawa zinaweza kutumika pamoja na tiba ili kudhibiti dalili za wasiwasi.
- Msaada wa Familia: Wazazi na walezi wana jukumu muhimu katika kusaidia mtoto kukabiliana na wasiwasi kwa kujenga mazingira ya usalama na upendo.
- Mabadiliko ya Maisha: Mabadiliko katika mtindo wa maisha (lifestyle), kama vile kulala vya kutosha, kula chakula chenye afya, na kufanya mazoezi ya kawaida, yanaweza kusaidia kupunguza wasiwasi.
Hitimisho:
Ni muhimu kutambua kwamba wasiwasi kwa watoto ni tatizo linaloweza kutibiwa. Ikiwa unashuku kuwa mtoto wako ana tatizo la wasiwasi, ni muhimu kumpeleka kwa mtaalamu wa afya ya akili kwa uchunguzi na matibabu.
Utangulizi:
Umewahi kujiuliza kwa nini mara nyingine watoto wachanga hufa ghafla bila sababu za kueleweka? Jibu la swali hili lipo katika uelewa wa janga la sudden infant death syndrome (SIDS).
SIDS ni kifo cha ghafla cha mtoto mchanga mara nyingi chini ya mwaka mmoja na mwenye kuonekana na afya njema ambacho hakina sababu za kueleweka hata baada ya uchunguzi wa kina wa kitabibu. Vifo hivi vimekuwa chanzo cha majonzi kwa wazazi wengi, na bado havijapata tiba kamili.
SIDS HUSABABISHWA NA NINI?
Ingawa sababu halisi za SIDS hazijulikani kabisa, kuna baadhi ya mambo ambayo yanaweza kuongeza hatari ya kutokea kwake:
-
Unywaji wa Pombe na Uvutaji Sigara: Wazazi wanaotumia pombe au sigara wanaongeza hatari kwa mtoto wao.
-
Kulala Kifudifudi: Kumlaza mtoto kifudifudi kabla hajawa na uwezo wa kujigeuza mwenyewe kunaongeza hatari ya SIDS. Ni vyema mtoto alazwe chali chali au awe na muda maalumu wa kulala kifudifudi wenye uangalizi maalumu (supervised tummy time).
-
Unyonyeshaji: Kuna njia sahihi ambazo zinatakiwa kufuatwa ili kuzuia mtoto kupaliwa au kuziba njia ya hewa.
-
Mazingira ya Kulala: Mahali anapolala mtoto panapaswa pawe tambarare (flat surface) pagumu (sio godoro la kubonyea), panapaswa kuwa salama bila vitu vingi kama vile mito, midoli au blanketi nyingi. Pia ni hatari kwa mzazi/mlezi kulala kitanda kimoja na mtoto mchanga!!
-
Matatizo ya Afya ya Mtoto: Baadhi ya matatizo ya afya ya mtoto, kama vile matatizo ya kupumua au matatizo ya moyo, ubongo na viungo vingine yanaweza kuongeza hatari ya SIDS.
Kuzuia SIDS
Ingawa hakuna njia ya kuzuia kabisa SIDS, kuna hatua ambazo wazazi wanaweza kuchukua ili kupunguza hadhari:
- Kulala Mtoto Chali: Siku zote mlaze mtoto wako chali.
- Epuka Vitu Vingine Vitandani: Epuka kuweka vitu vingi kama mito, blanketi, au vitu vya kuchezea kitandani.
- Unyonyeshaji: Nyonyesha mtoto wako kwa muda mrefu iwezekanavyo kwa kutumia njia salama.
- Mazingira ya Kulala: Hakikisha chumba cha kulala cha mtoto ni chenye joto la wastani na mzunguko mzuri wa hewa.
- Usiweke Mtoto Katika Kitanda cha Wazazi: Epuka kulala na mtoto kitandani.
- Mahudhurio mazuri ya Kliniki: Wazazi wanapaswa kuhakikisha kuwa mama na mtoto wanahudhuria kliniki kila appointment bila kukosa. Hii itasaidia kuzuia matatizo ya afya ya mtoto ambayo yanaweza kuongeza hatari ya SIDS.
Umuhimu na Uchunguzi wa Kitaalamu
Ikiwa mtoto wako atafariki ghafla, ni muhimu sana kufanya uchunguzi wa kina wa kitabibu ili kubaini sababu halisi ya kifo. Hii itasaidia kuzuia matukio kama haya katika siku za baadaye.
Hitimisho:
Kwa kuzingatia hatua za kuzuia SIDS, tunaweza kupunguza idadi ya vifo vya watoto wachanga na kuhakikisha kwamba kila mtoto ana nafasi ya kuishi maisha yenye afya na furaha.
References:
- World Health Organization. (2023). Sudden infant death syndrome. https://platform.who.int/mortality/themes/theme-details/topics/topic-details/MDB/sudden-infant-death-syndrome
- American Academy of Pediatrics. (2023). Reducing the Risk of Sudden Infant Death Syndrome (SIDS). https://www.aap.org/en/patient-care/safe-sleep/
Note: Kwa maelezo zaidi na ushauri, wasiliana na daktari wa watoto.
SHAKEN BABY SYNDROME (SBS) NI NINI?
Utangulizi:
Umewahi kuwaza kwamba unaweza kumpoteza mwanao mchanga kwasababu ya kumtikisa?
Shaken Baby Syndrome (SBS), au "sindromu ya watoto kutikiswa," ni hali ambayo inajielezea kwenye jina lake. Hali hii hutokea pale mtoto mchanga anapotikiswa kwa nguvu na kusababisha athari katika ubongo wa mtoto, na inaweza kusababisha madhara makubwa katika kimwili na afya afya kwa ujumla.
SBS ni sababu kubwa zaidi ya kifo/ athari ya ubongo inayosababishwa na unyanyasaji wa watoto.
Kwa jumla 95% ya watoto wachanga walio na jeraha kubwa la kichwani wametikiswa. Asilimia inayobaki husababishwa zaidi na majeraha makubwa ya kichwa kama vile ajali za magari.(Blumenthal, 2002)
Ni Kitu gani hupelekea mtoto kutikiswa?
SBS mara nyingi hutokea kutokana na hasira au kukata tamaa kwa mzazi au mlezi, hasa wakati mtoto analia kwa muda mrefu. Wakati mwingine ni unyanyasaji wa mtoto(child abuse) kutoka kwa mlezi hupelekea hadi mtoto kutikiswa. Wakati mwingine ni kutokujua kwa mlezi na akafanya shughuli ya mtikisiko kama kurukaruka huku akiwa amembeba mtoto mchanga.
Nini hutokea baada ya mtoto kutikiswa?