Ukubwa wa tatizo
Ifahamike kuwa si kila mwenye kisukari anaweza kupata ugonjwa wa figo. Inasemekana, kwa baadhi ya watu, hali hii ina uhusiano mkubwa na historia ya kisukari katika familia.
Wagonjwa wa kisukari ambao pia ni wavutaji wa sigara, na wale wenye aina ya kwanza ya kisukari (type 1 Diabetes Mellitus) kilichoanza kabla hawajafika miaka 20, wana hatari kubwa ya kupata matatizo ya figo.
Dalili
Kwa kawaida, mtu mwenye tatizo hili anaweza asioneshe dalili zozote katika miaka ya mwanzo ya ugonjwa. Mara nyingi dalili huanza kujitokeza miaka 5 mpaka 10 baada ya figo kuathirika. Dalili huanza taratibu kabla ya kuwa dhahiri.
Dalili kwa watu waliopata madhara makubwa katika figo hujumuisha kukosa hamu ya kula, kujihisi uchovu na kwa ujumla kutojihisi vizuri. Dalili nyingine ni pamoja na kuumwa kichwa, kichefuchefu na kutapika, kuvimba miguu pamoja na dalili nyingine kama zilivyoainishwa katika ugonjwa sugu wa figo.
Vipimo na uchunguzi
Kwa watu wenye kisukari, ni vema kufanya uchunguzi wa figo zao walau mara moja kwa mwaka. Daktari wako kwanza atakuchunguza kama una dalili zozote zinazoashiria matatizo ya figo. Kipimo mojawapo ni kuchunguza mkojo kwa ajili ya kuchunguza kiwango cha protini aiitwayo albumin au microalbuminuria.
Kuwepo kwa kiasi kingi cha protini katika mkojo ni mojawapo ya dalili za kuwepo kwa tatizo katika figo.
Vipimo vingine ni pamoja na kiasi cha Urea Nitrogen katika damu (BUN), kiwango cha creatine katika damu (serum creatinine), kiasi cha protini katika mkojo wa saa 24 (24-hour urine protein), kiasi cha madini ya phosphorus, calcium, bicarbonate, PTH, na potassium katika damu, kiasi cha wingi wa damu (Hemoglobin), na wakati fulani kufanya biopsy ya figo kwa ajili ya uthibitisho wa tatizo.
Matibabu
Lengo kuu la matibabu ni kufanya figo zisiendelee kuathirika. Mojawapo ya njia bora kabisa za kusaidia hilo ni kuthibiti kiwango cha shinikizo la damu kuwa chini ya 130/80 mmHg.
Dawa za jamii ya Angiotensin Converting Enzyme inhibitors kama vile Captopril pamoja na zile za angiotensin receptor blockers zimeonekana kuwa na uwezo mkubwa wa kushusha shinikizo la damu wakati huo huo kuthibiti kasi ya kuharibika kwa figo kutokana na kisukari.
Kula lishe yenye kiwango kidogo cha mafuta, matumizi ya dawa za kuthibiti kiasi cha mafuta mwilini, na kufanya mazoezi mara kwa mara pia husaidia sana kuzuia au kupunguza kasi ya kuathirika kwa figo.
Aidha uthibiti wa kiwango cha sukari kwa kubadilisha aina ya chakula unachokula, kutumia dawa za kisukari kama inavyoshauriwa na daktari wako, na kuchunguza kiwango chako cha sukari mara kwa mara, husaidia pia katika kuzuia tatizo hili. Kwa mtu mwenye uambukizi katika njia ya mkojo (UTI) ni vema kutibiwa kwa kutumia antibiotics.
Matarajio
Ugonjwa wa figo unaotokana na kisukari ni mojawapo ya vyanzo vikuu vya kuugua na kifo kwa wagonjwa wa kisukari.
Hata hivyo, iwapo tatizo litagunduliwa katika hatua zake za awali, kuna uwezekano mkubwa wa kuzuia na kuthibiti uharibifu wa figo. Mara baada ya protini kuonekana katika kojo, uharibu wa figo huanza kuwa mkubwa na wa kutisha kiasi cha kuhitaji kufanyiwa dialysis au kubadilishwa kwa figo.
Hali kadhalika, watu wenye ugonjwa wa figo unaotokana na kisukari huwa wana magonjwa mengine kama vile shinikizo la juu la damu, magonjwa ya moyo pamoja na magonjwa ya macho.