Image

Maambukizi ya Fangasi Sehemu ya Pili

Katika sehemu ya kwanza ya makala hii ya maambukizi ya fangasi, tuliangalia aina za fangasi, watu waliopo kwenye hatari ya kupata maambukizi ya fangasi na aina ya maambukizi ya fangasi. Katika sehemu hii ya pili na  ya  mwisho katika muendelezo wa makala hii, tutaangalia maambukizi ya fangasi kwenye damu yaani systemic mycoses.

Systemic Mycoses

Ni maambukizi ya fangasi kwenye damu ambayo huanzia kwa fangasi kuvamia mapafu ya mtu.Maambukizi haya yamegawanyika katika sehemu kuu mbili;

 • Maambukizi ya fangasi kutokana na fangasi wa kawaida kwa watu wenye afya njema (Systemic mycoses due to primary pathogens)
 • Maambukizi ya fangasi kwenye damu kutokana na fangasi nyemelezi kwa watu wenye upungufu wa kinga mwilini (Systemic mycoses due to opportunistic pathogens)

Maambukizi ya fangasi kutokana na fangasi wa kawaida kwa watu wenye afya njema (Systemic mycoses due to primary pathogens)

Maambukizi haya ya fangasi huanzia kwenye mapafu na kusambaa kwenye viungo vingine vya mwili.Yafuatayo ni maambukizi ya fangasi kwenye damu yanayoonekana sana kwa wagonjwa nayo ni;

 • Histoplasmosis
 • Blastomycosis
 • Coccidioidomycosis

Histoplasmosis

Husababishwa na fangasi Histoplasma Capsulatum, ambao huishi kwenye mazingira hasa kwenye mchanga na mtu huweza kupata maambukizi ya fangasi hawa kwa kuvuta hewa yenye mazalia ya fangasi (Fungal spores).Watu wenye maambukizi haya huweza kuambukiza watu wengine au hata kuambukiza wanyama. Maambukizi ya histoplasmosis ni hatari sana kwa watu wenye kinga dhaifu mwilini hasa kama yatasambaa kwenye viungo vingine vya mwili.

Dalili na Viashiria ya maambukizi ya Histoplasmosis

 • Homa kali
 • Uchovu
 • Kutetemeka (Chills)
 • Maumivu ya kichwa
 • Maumivu ya kifua
 • Maumivu ya mwili (Body aches) 

Vipimo vya uchunguzi

 • Uchunguzi wa maabara kwa kutumia hadubini
 • Kuotesha fangasi maabara
 • Ugunduzi wa surface markers za fangasi aina ya Histoplasma Capsulatum kwenye mkojo
 • Vipimo vya damu vya kuangalia jinsi kinga za mwili zinavyojitahidi kukabiliana na maambukizi haya (Antibody response to histoplasma)

Tiba ya Histoplasmosis

 • Mara nyingi maambukizi haya hupona yenyewe kwa wale wanaopata maambukizi ya wastani
 • Kwa wale wenye kupata maambukizi hatari, uhitaji matibabu ya dawa za kutibu fangasi

Blastomycosis

Husababishwa na fangasi aina ya Blastomyces dermatitidis.Maambukizi haya huathiri mbwa, binadamu, simba, farasi nk. Blastomycosis huweza kuenezwa kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mtu mwingine au kutoka kwa mnyama kwenda kwa binadamu.

Dalili na Vishiria vya Blastomycosis

 • Homa kali inayoambatana na mtetemo (Chills)
 • Maumivu ya kifua
 • Kukohoa
 • Kushindwa kupumua vizuri
 • Maumivu ya misuli (Muscle aches)
 • Maumivu ya viunganishi vya mifupa (Joint pain)

Vipimo vya Uchunguzi

 • Kuoteshwa kwa fangasi maabara (Culture)
 • Kuchunguza tishu maabara kwa kutumia hadubini
 • Kipimo cha antigen test - Kinaweza kugundua uwepo wa fangasi kwa kupima mkojo au damu (Serum)

Tiba ya Blastomycosis

 • Dawa za kutibu fangasi – Hutumika kwa muda mrefu

Coccidiomycosis

Husababishwa na fangasi aina ya Coccidioides immitis au Coccidioides posadasii.Maambukizi ya fangasi aina hii pia hutokana na mtu kuvuta hewa yenye mazalia ya fangasi (Fungal Spores).Maambukizi haya yamegawanyika katika;

 • Acute Coccidiomycosis – Hutokea tu baada ya mtu kupata maambukizi na kama muathirika hatapata tiba, basi maambukizi haya yataendelea katika hatua inayofuata
 • Chronic Coccidiomycosis – Hufuata hatua ya awali ya acute Coccidiomycosis
 • Disseminated Coccidiomycosis- Hatua hii uhusisha Primary Coccidiomycosis inayoonekana kwa watu wenye upungufu wa kinga mwilini kama wagonjwa wa kisukari, wanaotumia dawa aina ya steroid, au dawa za kutibu saratani, nk.

Dalili na Viashiria vya Primary Coccidiomycosis

Dalili hizi hutokea baada ya wiki au miezi kadhaa nazo ni;

 • Homa ya wastani
 • Kudhoofu mwili (Anorexia)
 • Kupungua uzito
 • Kuchoka mwili (Weakness)

Vipimo vya Uchunguzi

 • Daktari atashuku uwepo wa maambukizi haya baada ya kuchukua historia kamili kutoka kwa mgonjwa
 • Kipimo cha makohozi
 • Kipimo cha maji ya uti wa mgongo (CSF)
 • Vipimo vya kuchunguza nyama maabara (Biopsy)
 • Kipimo cha maabara kwa kutumia hadubini
 • Kipimo cha kuotesha fangasi maabara
 • Vipimo vya damu kwa kutumia Immuno diffusion kit (Kuangalia IgG na IgM antibodies) na Complement Fixation (Kwa kuangalia IgG antibodies) ni muhimu sana.

Tiba ya  Coccidiomycosis

 • Kawaida maambukizi haya hupona yenyewe ndani ya wiki kadhaa
 • Hata hivyo baadhi ya wagonjwa watahitaji dawa za kutibu fangasi 

Maambukizi ya fangasi kwenye damu kutokana na fangasi nyemelezi  kwa watu wenye upungufu wa kinga mwilini (Systemic mycoses due to opportunistic pathogens)

Maambukizi haya hutokea kwa watu wenye kinga dhaifu ya mwili kama;

 • Wagonjwa wa ukimwi
 • Wanaotumia dawa aina ya steroid, dawa za kutibu za saratani na immunosuppressive drugs,
 • Wale wanaotumia dawa za antibayotiki pasipo kufuata masharti ya daktari,
 • Wenye kutibiwa kwa mionzi,
 • Watu waliofanyiwa upasuaji wa moyo (Open heart surgery),
 • Wagonjwa waliowekewa mpira wa kupitisha mkojo (indwelling catheter),
 • Wagonjwa waliowekewa milango kwenye mioyo  yao (Artificial heart valves)

Maambukizi yanayotokana na fangasi hawa nyemelezi ni pamoja na;

 • Candidiasis,
 • Cryptococcosis
 • Aspergillosis

Candidiasis

Husababishwa na fangasi aina ya Candida.Kuna aina 20 za fangasi aina candida wanaojulikana kusababisha maambukizi mara kwa mara.Sehemu ambazo hupata maambukizi ya candidiasis ni kwenye ngozi, kucha za vidole vya mikononi au miguuni,kwenye mdomo, mrija wa kupitisha chakula, kwenye tupu ya mwanamke au kwenye uume, kwenye mfumo wa chakula (Gastro-intestinal tract), mfumo wa mkojo (Urinary tract)  na mfumo wa upumuaji (Respiratory tract).

Asilimia 20 ya wagonjwa wanaotumia dawa za saratani na wagonjwa wa ukimwi ndio hupata maambukizi haya1.

Unaweza kusoma makala ya Maambukizi ya Fangasi katika Sehemu za Siri (Vaginal Candidiasis) hapa

Maambukizi ya candidiasis mdomoni hujulikana kama oral thrush na huonekana sana kwa watoto wenye umri chini ya mwezi mmoja, kwa wazee na kwa watu wenye upungufu wa kinga mwilini.Asilimia 6 ya watoto wenye umri wa chini ya mwezi mmoja ndio hupata maambukizi haya ya candidiasis kwenye mdomo1. Oral thrush husababisha;

 • Mabaka meupe kwenye ulimi, kwenye koo na sehemu nyingine za kinywa
 • Vidonda kutokea mdomoni na hivyo mgonjwa kupata taabu wakati wa kumeza chakula 

Dalili na Viashiria

Dalili na viashiria vya candidiasis hutofautiana kulingana na sehemu iliyoathirika.Maambukizi ya candidiasis husababisha;

 • Sehemu husika kuwa nyekundu
 • Kuwashwa katika sehemu iliyoathirika
 • Maudhi yanayotokana na maambukizi haya (discomfort)

Oesophageal Candidiasis

Huonekana kwa wagonjwa wenye upungufu wa kinga mwilini kuliko watu wenye afya njema na maambukizi haya yana hatari ya kusambaa kwenye damu kama hayatadhibitiwa mapema.

Dalili na Viashiria vya Oesephageal Candidiasis

 • Kupata tabu wakati wa kumeza chakula
 • Maumivu wakati wa kumeza chakula
 • Kichefuchefu
 • Kutapika

Gastrointestinal candidiasis-Maambukizi ya candidiasis kwenye mfumo wa chakula husababisha

 • Kuwashwa sehemu ya haja kubwa (Anal itching)
 • Kubeua (belching)
 • Kuvimbiwa tumbo (Bloating)
 • Kushindwa kumengenya chakula vizuri (Indigestion)
 • Kichefuchefu
 • Kuharisha
 • Tumbo kujaa gesi
 • Maumivu makali ya tumbo
 • Kutapika na
 • Vidonda vya tumbo (Gastric ulcers) 2,3 and 4.

Vipimo vya uchunguzi kwa maambukizi ya candidiasis kwa ujumla

 • Kuangalia uwepo wa fangasi maabara kwa kutumia hadubini
 • Kuotesha fangasi maabara
 • Kipimo cha endoscopy kwa maambukizi ya fangasi kwenye mfumo wa chakula na kwenye mfumo wa upumuaji pamoja na kwenye mrija wa kupitisha chakula
 • Fangasi kwenye mfumo wa chakula pia huweza kufanyiwa culture kwa kuchukua majimaji kutoka sehemu ya utumbo inayojulikana kama duodenum 

Tiba ya candidiasis

 • Dawa za kutibu fangasi (candida) kulingana na sehemu husika
 • Dawa za IV drugs za kutibu fangasi kwa wagonjwa wenye upungufu wa kinga mwilini 

Kinga dhidi ya Maambukizi ya Fangasi

 • Kuhakikisha unakula mlo wenye virutubisho sahihi (balanced diet)
 • Kudhibiti kiwango cha sukari mwilini kwa wagonjwa wa kisukari
 • Kuvaa nguo za ndani zilizotengenezwa kwa pamba
 • Kuepuka kuvaa nguo nzito kwa wale wanaoishi sehemu zenye joto kali
 • Kuepuka kuvaa nguo za kubana sana kwa wanaoishi sehemu zenye joto kali
 • Kuepuka kuvaa nguo zenye unyenyevu kwa muda mrefu
 • Kusafisha kinywa vizuri angalau mara mbili kwa siku
 • Kutunza usafi wa kinywa kwa wagonjwa wenye upungufu wa kinga mwilini
 • Kusukutua kinywa kwa kutumia chlorhexidine mouthwash kwa wagonjwa wenye saratani
 • Kusafisha kinywa kwa kutumia maji au mouthwash baada tu ya kutumia inhaler kwa wagonjwa wanaotumia inhaler
 • Kukausha miguu yako kabla ya kuvaa viatu
 • Kufua nguo za mazoezi baada tu ya kumaliza kufanya mazoezi

Marejeo

 1. Oral Candidiasis Statistics". cdc.gov. February 13, 2014. Retrieved 28 December 2014.
 2. Martins N, Ferreira IC, Barros L, Silva S, Henriques M (June 2014). "Candidiasis: predisposing factors, prevention, diagnosis and alternative treatment". Mycopathologia. 177 (5-6): 223–240. doi:10.1007/s11046-014-9749-1. PMID 24789109.
 3. Wang ZK, Yang YS, Stefka AT, Sun G, Peng LH (April 2014). "Review article: fungal microbiota and digestive diseases". Aliment. Pharmacol. Ther. 39 (8): 751–766. doi:10.1111/apt.12665. PMID 24612332.
 4. Erdogan A, Rao SS (April 2015). "Small intestinal fungal overgrowth". Curr Gastroenterol Rep. 17 (4): 16. doi:10.1007/s11894-015-0436-2. PMID 25786900. 

 

Imesomwa mara 18261 Imehaririwa Jumamosi, 01 Julai 2017 18:12
Dr Khamis

Dr. Khamis H.Bakari (MD PhD) ni daktari bingwa,mhadhiri katika chuo cha afya cha Chuo  Kikuu cha Dodoma,mtaalamu wa Tiba na Uchunguzi kwa kutumia mionzi ya nyuklia (Nuclear medicine).

Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.

Makala shabihana