Image

Upungufu Wa Damu Mwilini (Anemia)

Upungufu wa damu mwilini au Anemia ni miongoni mwa magonjwa yanayosumbua watu wengi duniani. Anemia humaanisha kupungua kwa kiwango cha chembechembe nyekundu za damu (RBC’s) katika mzunguko wake, au kupungua kwa wingi wa hemoglobin kwenye damu.

Kazi ya hemoglobin ambayo hupatikana ndani ya chembechembe nyekundu za damu ni kubeba gesi ya oksijeni kutoka katika mapafu na kusambaza kwenye tishu. Kwa sababu hiyo upungufu wa damu husababisha ukosefu wa hewa muhimu ya oksijeni katika viungo au hypoxia.

Kwa mujibu wa shirika la Afya duniani (WHO), viwango vya hemoglobini hutofautiana kati ya jinsia moja na nyingine, na kati ya nchi au eneo na eneo. Hata hivyo, iwapo nchi zote zitazingatia viwango hivi vya WHO, kunaweza kutokea mkanganyiko hususani kwa nchi zinazoendelea kama za Afrika hivyo basi ili kuepuka hali hiyo Wizara za afya za nchi husika zimejiwekea viwango vyao kutokana na mazingira ya nchi zao.

Kwa mujibu wa takwimu za WHO, na kulingana na jinsia, mtu aliye na chini ya viwango vifuatavyo huhesabika kuwa na upungufu wa damu, kwa wanaume chini ya 13g/dl, wanawake wasio wajawazito chini ya 12g/dl wakati wanawake wajawazito na watoto ni chini ya 11g/dl.

Upungufu wa damu husababishwa na nini?

Mambo yanayoweza kusababisha upungufu wa damu yanaweza kugawanywa katika makundi makuu matatu, ambayo ni:

 • Kupungua kwa uzalishwaji wa chembe nyekundu za damu yaani impaired production of rbcs kunakoweza kutokea iwapo kuna upungufu wa madini muhimu ya chuma (iron deficiency) hali ambayo husababishwa na mtu kuwa na minyoo aina ya hookworms au mtu kuwa na vidonda vya tumbo; upungufu wa vitamin hasa vitamin B12 pamoja na upungufu wa folic acid; na magonjwa sugu ya figo (chronic renal failure)
 • Kuongezeka uharibifu wa chembe nyekundu za damu kuliko kawaida yaani increased destruction of rbcs. Hali hii huitwa hemolytic anemia ambayo inaweza kutokea iwapo mtu ana kasoro katika umbo la chembe zake nyekundu za damu kwa mfano iwapo ana magonjwa ya hereditary spherocytosis au sickle cell; aliongezewa damu isiyoendana na kundi lake yaani blood transfusion reaction; ana malaria, au saratani ya damu kama vile chronic lymphocytic leukemia.
 • Kupoteza damu yaani blood loss ambayo yaweza kusababishwa na mambo kama ajali; kupoteza damu wakati wa upasuaji; na kupoteza damu kunakotokea kwa wanawake mara baada ya kujifungua au postpartum hemorrhage (PPH).
 • Sababu nyingine zinazoweza kusababisha upungufu wa damu mwilini ni pamoja na kuungua (burns); matumizi ya dawa au kemikali zinazoathiri sehemu laini ya mifupa inayohusika na uzalishaji wa chembe nyekundu za damu (bone marrow); magonjwa yanayosababisha kuharibika kwa chembe nyekundu za damu kabla ya muda wake kama vile thrombocytopenic purpura na hemolytic uremic syndrome

Dalili za Anemia ni zipi?

Kwa ujumla dalili za upungufu wa damu ni pamoja na

 • Mwili kuwa mchovu au mlegevu
 • Kupungua na kukosekana kwa umakini
 • Mgonjwa kushindwa kupumua vizuri hasa baada ya kutoka kufanya kazi nzito au mazoezi
 • Mapigo ya moyo kwenda haraka
 • Kucha kuwa na umbo la kijiko (Koilonchyia) na kukatika kirahisi. Hali hii hutokea kwa wenye upungufu wa madini ya chuma.
 • Kuwa na manjano (jaundice) kwenye macho, ngozi na sehemu nyingine za mwili kutokana na kuongezeka kwa uharibifu wa chembe nyekundu za damu.
 • Wakati mwingine, iwapo anemia ni kali, mgonjwa anaweza pia kuwa na dalili za moyo kushindwa kufanya kazi (heart failure) kama vile kuvimba miguu, au kushindwa kupumua wakati wa kulala bila kuinua kitanda (flat)
 • Baadhi ya wagonjwa wenye anemia inayotokana na upungufu wa madini ya chuma mwilini hupendelea kula vitu kama udongo, chaki, penseli, mchele mbichi, au vipande vya barafu, hali ambayo kitaalamu huitwa PICA.

Vipimo na Uchunguzi:

Vipimo kwa ajili ya tatizo hili vimelenga kutambua iwapo mgonjwa ana upungufu wa damu pamoja na kutambua chanzo chake. Vipimo hivyo ni

 • Kupima damu na viainishi vyake (complete blood count/full blood picture with red cell indices) kama vile MVC, MCH na MCHC.
 • Kuchunguza damu kwenye darubini (peripheral blood smear) ambayo husaidia kugundua iwapo kuna tatizo kwenye umbo la chembe nyekundu za damu.
 • Hemoglobin electrophoresis
 • Sickling test iwapo mgonjwa anahisiwa kuwa na ugonjwa wa sickle cell
 • Kuchunguza choo (stool examination) husaidia kugundua uwepo wa minyoo (hookworms)
 • Kuchunguza mkojo (urine examination)
 • Kucuhunguza uwepo wa vidonda vya tumbo kwa kutumia Endoscopy na vipimo vya barium
 • Kuchunguza sehemu ya mifupa inayozalisha chembe nyekundu za damu (bone marrow examination)

Matibabu ya Upungufu wa damu

Matibabu ya upungufu wa damu hutegemea kiwango cha upungufu (ukubwa wa tatizo) na chanzo chake. Kulingana na chanzo, matibabu yanaweza kujumuisha

 • Lishe yenye virutubisho muhimu kwa ajili ya wenye upungufu wa madini ya chuma, vitamin B12, na folic acid. Vyakula kama mboga za majani, nyama, na matunda hushauriwa sana.
 • Matumizi ya dawa za corticosteroids hasa kwa wagonjwa wenye autoimmune hemolytic anemia
 • Kuacha matumizi ya dawa au kemikali zenye kuathiri sehemu za mifupa zinazohusika na uzalishaji chembe za damu
 • Kuongezewa damu kwa wale walio poteza kiasi kikubwa cha damu au wale wenye dalili za moyo kushindwa kufanya kazi.
 • Kwa wenye minyoo ya hookworms hupewa dawa za kuua na kuondoa minyoo mwilini.
 • Kutibu malaria ipasavyo
 • Kutibu vidonda vya tumbo kwa wenye tatizo hili

Jinsi ya kuzuia upungufu wa damu: Namna ya kuzuia upungufu wa damu ni pamoja na kujitahidi kula mlo kamili wenye mchanganyiko wa nyama, mboga za majani, maziwa na matunda; kutambua dalili na kutibu haraka magonjwa yawezayo kuleta upungu wa damu; pamoja na kuwapa mama wajawazito vidonge vyenye madini ya chuma na folic acid

Imesomwa mara 36078 Imehaririwa Jumatatu, 21 Januari 2019 15:27
Dr.Mayala

Dr.Henry A Mayala ni daktari bingwa Wa Tiba ya moyo katika taasisi ya Jakaya Kikwete Cardiac Institute (JKCI), ambaye kwasasa anasomea shahada ya uzamivu (PhD) ya Tiba ya Moyo katika Chuo Kikuu cha Tongji  nchini China.

Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.

Makala shabihana