Image

Tundu Katika Kuta za Juu za Moyo (Atrial Septal Defect)

Katika muendelezo wa magonjwa ya moyo ya kuzaliwa nayo, leo nitagusia kuhusu Tundu katika kuta za juu za moyo (atrial walls) au kwa kitaalamu Atrial septal defect (ASD).

Wakati kijusi (fetus) kinapo endelea kukua, kuta kati ya atria mbili za moyo nayo hukua (kitaalamu interatrial septum) ili kutenganisha chemba ya kulia na kushoto. Lakini katika kipindi hiki huwa kuna tundu kati ya kuta hizi kitaalamu huitwa foramen ovale.

Tundu hili ni la kawaida kwa kipindi hiki cha kijusi, tundu hili husababisha damu yenye oksijeni  kutoka kwenye kondo la mama (placenta) kutokwenda kwenye mapafu amabayo hayaja komaa na kuelekea sehemu nyingine za mwili hasa kichwani. Kipande cha tishu kinachoitwa kitaalamu septum primum hufanya kazi kama valvu katika tundu hili. Mara tu mtoto anapozaliwa, shinikizo katika mishipa ya damu ya mapafu (pulmonary circulatory system) hushuka na kusababisha tundu hili (foramen ovale) kufunga kabisa.

Tundu hili huwa halifungi kabisa kwenye karibu asilimia ishirini na tano ya watu wazima, hivyo pindi shinikizo likiongezeka katika mishipa ya damu ya mapafu (hali inayoweza kutokea kwa sababu ya kuwepo kwa shinikizo la damu kwenye mapafu (pulmonary hypertension) kutokana na sababu mbalimbali, au kuwa na matatizo ya kikohozi cha muda mrefu), husababisha tundu la foramen ovale kutofunga na kubaki wazi. Hali hii kitaalamu huitwa patent foramen ovale (PFO).

Aina za tundu katika kuta za juu za moyo

Mpaka sasa, zipo aina kuu sita za tundu katika kuta za juu za moyo, ambazo ni

 • Ostium secundum ASD
 • Patent foramen ovale
 • Otium primum ASD
 • Sinus venosus ASD
 • Common or single atrium
 • Mixed ASD

Aina ya kwanza yaani Ostium secundum inaongoza kwa hutokea mara kwa mara, na huchangia kati ya asilimia 6 hadi 10 ya magonjwa yote ya moyo ya kuzaliwa nayo. Mtatatizo haya hutokana na uwazi wa tundu (foramen ovale) kuwa mkubwa, na kutokukua vema kwa kuta inayotenganisha (septum secundum). Hata hivyo karibu asilimia 70 ya watu wenye tatizo hili huweza kufikisha miaka 40 ndipo dalili huanza kujitokeza.

Dalili za tundu katika kuta za juu za moyo

 • Kupumua kwa shida hasa wakati wa mazoezi
 • Maambukizi ya mara kwa mara ya mfumo wa hewa kwa watoto
 • Kuhisi mapigo ya moyo yanaenda haraka
 • Uchovu
 • Kujaa Miguu au kuvimba tumbo
 • Ngozi kuwa ya bluu

Tundu kwenye kuta za juu za moyo

Madhara ya kuwepo kwa tundu kwenye kuta za juu za moyo

 • Shinikizo la damu la mapafu (Pulmonary hypertension)
 • Eisemnenger syndrome ni hali inayotokea pale ambapo uelekeo wa mkondo wa damu kutoka upande wa kushoto wa moyo kwenda upande wa kulia kupitia kwenye tundu zilizo kwenye kuta zinazotenganisha chemba za moyo huongeza mtiririko wa damu katika mishipa ya mapafu na kusababisha ongezeko la shinikizo la damu katika mapafu, hali ambayo hupelekea kuongezeka pia kwa shinikizo la damu katika upande wa kulia wa moyo, na hivyo kusababisha kubadilika kwa uelekeo wa damu kutoka upande wa kulia kwenda kushoto.
 • Upande wa kulia wa moyo kushindwa kufanya kazi vizuri
 • Hatari ya kupata kiharusi

Wanawake wajawazito wenye tundu katika kuta za juu za moyo (ASD) huweza kuvumilia hali hii na kuendelea na ujauzito bila matatizo yoyote lakini kwa wale ambao wameshapata madhara hali huwa wako katika hatari ya kupata madhara zaidi katika ujauzito hivyo, kwa wale ambao wameshapata madhara hushauriwa kuto shika mimba kwasababu huweza kuhatarisha maisha yao.

Vipimo

 • Chest x-ray
 • Echocardiogram – ni kipimo ambacho huweza kuonyesha tatizo, hasa tundu liko wapi.
 • ECG
 • Cardiac catheterization- hutumika kama kipimo na njia ya matibabu vilevile
 • MRI
 • Pulse oximetry- hutumika kuangalia kama damu yenye oksijeni inachanganyika na ile isiyo nayo

Matibabu

Matibabu ya awali ni ya kupunguza dalili ambayo huhusisha dawa zifuatazo

 • Beta blocker-lopressor, inderal
 • Cardiac glycoside- digoxin

Matatibu ya kutatua tatizo ni kati ya moja wapo ya njia hizi

 • Upasuaji (open heart surgery) ili kuziba tundu na huweza kufanyiwa kwa watoto kati miaka 2 hadi 4
 • Transcatheter approach –hapa mrija kitaalamu catheter upitishwa kwenye mshipa wa damu wa femoral hadi kwenye moyo na huwa na patch ambayo hubandikwa katika tundu na kurekebisha tatizo.
Imesomwa mara 10680 Imehaririwa Jumatatu, 15 Mai 2017 13:24
Dr.Mayala

Dr.Henry A Mayala ni daktari bingwa Wa Tiba ya moyo katika taasisi ya Jakaya Kikwete Cardiac Institute (JKCI), ambaye kwasasa anasomea shahada ya uzamivu (PhD) ya Tiba ya Moyo katika Chuo Kikuu cha Tongji  nchini China.

Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.

Makala shabihana