Image

Carissa edulis na 'miujiza' yake

Mchungaji Mstaafu Ambilikile Mwasapile ni jina lililojipatia umaarufu sana katika miezi ya hivi karibuni nchini Tanzania na eneo la nchi za maziwa makuu. Umaarufu wake unatokana na madai kuhusu uwezo wake wa kutibu maradhi sugu mbalimbali  kwa kutumia dawa ya ‘kiimani’ iliyotengenezwa kwa kutumia majani ya mti maarufu sana katika mazingira ya eneo hilo unaojulikana kama mugariga. 

Lakini mugariga ni nini? Tabia zake ni zipi? Je una uwezo wowote wa kutibu maradhi yanayodaiwa kuwa sugu? Ni mti wa kale au umegunduliwa juzi juzi tu?

Mugariga au Carissa edulis kama unavyojulikana kitaalamu au ‘mtanda-mboo’ kwa Kiswahili fasaha si kitu kigeni duniani. Ni mti ambao umekuwepo tangu zama na zama. Kiasili, mti huu unapatikana maeneo mengi sana duniani hasa yale yenye uoto wa kitropiki kama vile Kenya, Tanzania, Sudan, Ethiopia, Thailand, Botswana, Namibia, Myanmar na Afrika ya Kusini (1).

Mti huu upo kwenye familia ya mimea ya Apocynaceae, familia ambayo inajumuisha genera zipatazo 163 za mimea zenye takribani aina 1850 za miti (2). Familia ya Apocynaceae inajumuisha aina kadhaa za miti ambazo zina matumizi mbalimbali kulingana na sehemu zinapopatikana. Kwa mfano kwa mujibu wa utafiti uliofanywa mwaka 1970 na Kokwaro na wenzake huko nchini Kenya (3), ilionekana kuwa aina ijulikanayo kama Acokanthera schimperi imekuwa ikitumiwa kwa miaka mingi na wenyeji wa maeneo ulipofanyika utafiti huo kama sumu kwa kupaka kwenye ncha za mishale na mikuki kwa ajili ya kutumika kama silaha. Hata hivyo, zipo aina kadhaa katika familia hii ya mimea ambazo si sumu na zimekuwa zikitumiwa kwa matumizi mbalimbali yakiwemo chakula.

Matumizi ya mti wa Carissa edulis yanatofautiana kati ya jamii na jamii. Kwa mfano inasemekana baadhi ya jamii nchini Ghana hutumia mti huu kama chachandu ya kuongeza ladha katika chakula, wakati nchini Sudan na Kenya, mti huu hutumika kutengenezea siki au jam. Aidha zipo jamii kadhaa hukohuko Kenya zinazotumia mti huu kama dawa ya kufukuza nyoka kwa kuweka mizizi yake iliyokaushwa juu ya paa la nyumba.

Pamoja na matumizi yaliyoelezwa hapo juu, matumizi makubwa kabisa ya mti ambayo ndiyo msingi mkuu wa makala hii ni katika kutibu magonjwa mbalimbali ya binadamu pamoja na wanyama.

Ili tuweze kufahamu vizuri utendaji wake kazi katika matibabu, hebu kwanza tuangalie kilichomo (ingredients) katika mti huu.

Kemikali zilizomo kwenye mti huu (ingredients)


Vifuatavyo ni viasili vilivyowahi kukutwa katika mti wa
 Carissa edulis baada ya tafiti mbalimbali za wataalamu wa afya pamoja na mitishamba.

 1. Mizizi yake imegundulika kuwa na kiasili cha Sesquiterpene ambacho huzalisha viasili vya carissone, cryptomeridiol, germacarane na β-eudesmane. Kwa ujumla viasili vya sesquiterpenes vinajulikana kuwa na tabia au uwezo wa kutibu magonjwa au hali zote zinazohusiana na mcharuko mwili (anti-inflammatory effects), vimelea (antimicrobial effects) na saratani na uvimbe (antineoplastic effects).
 2. Mbegu za matunda yake zimeonekana kuwa na viasili vya lignans kama vile carissanol, secoisolariciresinol, nortrachelogenin na olivil. Kutokana na umbo lake la kikemikali, viasili hivi hususani carissanol vimeonekana kuwa na tabia au uwezo wa kuua vimelea (antimicrobial effects) na kusaidia kuua seli zisizohitajika mwilini (antioxidant effects) sifa ambayo inaipa uwezo mkubwa wa kupambana na seli za saratani.
 3. Vichipukizi vyake vina viasili vya quebrachytol ambavyo kina tabia za kuimarisha kinga ya mwili kwa kutegemeza tando za seli (membrane stabilization effects) na kuua seli zisizohitajika zikiwemo za saratani (antioxidant effects). Pia zina cardioglycosides ambavyo hufanya kazi kwenye pump ya Na+-K+ na kuweza kuua minyoo.
 4. Shina na majani yameonekana kuwa na aina fulani ya kemikali ya alkaloid
 5. Magamba ya mizizi yake yamegunduliwa kuwa na viasili vya 2-Hydroxy acetophenone ambacho kina uwezo wa kufanya kazi katika mishipa ya damu na kuifanya itanuke (vasodilation effects) na hivyo kuwa na sifa kubwa ya kusaidia kushusha shinikizo la damu na kuongeza nguvu za kiume.

Matumizi katika tiba

Wenyeji wa jamii kadhaa nchini Ghana wamekuwa, kwa miaka kadhaa sasa, wakichanganya magamba ya mizizi na baadhi ya viungo na kutumia kwa ajili ya kutibu maumivu ya mgongo na maumivu ya sehemu nyingine za mwili. Aidha nchini Guinea, jamii zimekuwa na mazoea ya kuchemsha majani ya mti huu na kutumia kutibu maumivu ya meno. Jamii nyingine barani Africa zimekuwa zikitumia sehemu ya juu ya mizizi hii kutibu uvimbe na mcharuko mwili (inflammatory reactions). Hali kadhalika sehemu za mizizi mkuu zimekuwa zikitumika kwa ajili ya kutibu magonjwa ya zinaa kama kaswende na kisonono, kurudisha urijali na kuongeza uwezo wa kuzaa, vidonda vya tumbo au kikohozi.

Jamii nyingine zimekuwa zikitumia mti huu kwa ajili ya kutoa mimba, na kwa hapa Tanzania yapo baadhi ya makabila yanayotumia Carissa edulis kutibu ugonjwa wa malaria.

Utafiti wa hivi karibuni nchini Kenya umeonesha kuwa, mti wa Carissa edulis una uwezo wa kuua vimelea vya virus aina ya Herpes Simplex Virus ingawa haijajulikana hasa ni kwa njia gani.

Kwa mujibu wa mtafiti Lindsay na wenzake, 2000 (3) ukiacha aina (species) hii ya Carissa edulis, aina nyingine zilizo katika jamii moja na mti huu, kama vile Carissa lanceolata, imethibitika kuwa na uwezo wa kutibu bacteria vya aina mbalimbali vikiwemo Staphylococcus aureus, Escherichia coli na Pseudomonas aeruginosa bila kuwa na madhara kwa mtumiaji.

Je mti huu una madhara kwa afya za binadamu?

Mpaka sasa hakuna ushahidi wowote wa kitafiti unaoonesha kuwa matumizi ya dawa za mitishamba zinazotokana na mti wa Carissa edulis zina madhara kwa binadamu.

Je kuna ushahidi wowote wa kitafiti kuthibitisha uwezo wa Carissa edulis?

Tafiti kadhaa zilizofanywa barani Afrika na kwingineko duniani zinathibitisha hilo.

1. Uwezo wa kupambana na virus (Antiviral activities)

Mwaka 2005 , watafiti nchini Kenya (4) walitumia magamba ya mizizi ya Carissa edulis kuchunguza uwezo wa mti huu katika kupambana na virus wa jamii ya Herpes Simplex Virus (HSV) kwa kutumia panya. Matokeo ya utafiti huo yalionesha kuwa, dawa iliyotumika kutokana na mti huo ilikuwa na uwezo wa kuua aina (strains) zote mbili (wild na resistant) za virus hawa wa HSV. Ilionekana pia kuwa, aina sugu ya virus hawa yaani resistant strain ndiyo iliyoathiriwa zaidi ikilinganishwa na aina isiyo sugu (wild strain). Kwa maneno mengine, mti huu ulionekana kuwa na uwezo mkubwa katika kuua na kutokomeza virus walioonekana kuwa sugu zaidi kwa madawa mengine kuliko wale wasio sugu. Hata hivyo watafiti hawakuonesha ni kwa jinsi gani  (mode of mechanism) mti huu uliweza kufanya kazi hiyo na hivyo kupendekeza kufanyika kwa utafiti mwingine utakaofanya kazi hiyo hususani kwa binadamu.

2. Uwezo wa kupambana na virus vya Ukimwi (Antiretroviral effects)

Mpaka sasa hakuna utafiti wowote wa kisayansi uliofanywa kuthibitisha uwezo wa mti wa Carissa edulis katika kupambana na virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Ukimwi. Hivyo bado ni ngumu kuthibitisha uwezo wa mti huu katika kuua na kutokomeza virus vya Ukimwi. Hii inaleta changamoto kubwa kwa wanasayansi kuweza kubainisha hilo.

3. Uwezo wa kutibu kifafa na degedege (Anticonvulsant effects)

Mtafiti Ya’u (5) kutoka idara ya madawa ya chuo kikuu cha Ahmadu Bello, nchini Nigeria akishirikiana na wenzake walifanya utafiti kuchunguza uwezo wa mti wa Carissa eduliskatika kutibu magonjwa ya degedege na kifafa. Katika utafiti wao, walitumia magamba ya mizizi ya mti huu kuchunguza uwezo wake katika kuzuia kutokea kwa degedege kwa wanyama. Watafiti hao walipendekeza kuwa mti wa Carissa edulis una kiasili chenye uwezo wa kuzuia kutokea kwa degedege na hivyo kukubaliana na madai ya baadhi ya jamii zinazotumia mti huu kama dawa ya kutibu tatizo hilo.

4. Uwezo wa kutoa na kupunguza maji mwilini (Antidiuretic effects)

Mtafiti Nadi T (6) wa chuo kikuu cha Addis Ababa, Ethiopia akishirikiana na wenzake walifanya utafiti kuchunguza uwezo wa mti Carissa edulis katika kutoa na kupunguza maji mwilini kwa njia ya mkojo (antidiuretic effects). Katika utafiti wao, wataalamu hao walitumia magamba ya mizizi kuwapa panya na kisha kuchunguza kiasi cha mkojo kilichotolewa na panya hao pamoja na upotevu wa viasili vya Sodium, potassium na Chloride mwilini. Kadiri dozi ya dawa iliyotumika ilipoongezwa, kiwango cha mkojo na upotevu wa viasili hivyo nao pia uliongezeka. Matokeo haya ya utafiti yanaendana na mazoea ya tangu kale ya jamii mbalimbali ambazo zimekuwa zikitumia mti huu kwa ajili ya kusaidia kukojoa hususani kwa watu wenye matatizo ya figo.

5. Uwezo wa kutibu kisukari (Antidiabetic effects)

Watafiti kutoka chuo kikuu cha Alexandria nchini Misri (7), wakitumia panya wa maabara, walifanya utafiti kwa lengo la kuchunguza uwezo wa mti wa Carissa eduliskatika kutibu ugonjwa wa kisukari. Katika utafiti wao, wataalamu hao walifanikiwa kugundua kuwa, majani ya mti wa Carissa edulis yalikuwa na uwezo wa kushusha na kurekebisha kiwango cha sukari kwa panya waliokuwa na kisukari ndani ya muda wa masaa matatu, sawa kabisa na dawa za Metformin na buguanides zinazotumika kutibu ugonjwa huo mahospitalini.

Hitimisho

Ingawa tafiti mbalimbali za kisayansi zimefanyika kujaribu kuonesha uwezo wa mti waCarissa edulis katika kutibu magonjwa kadhaa kwa kutumia wanyama kama panya na kuku, mpaka sasa hakuna utafiti wowote uliowahi kufanyika kwa binadamu kuthibitish hilo, pamoja na kwamba tangu enzi na enzi, watu wa jamii zilizojaliwa kuwa na mti huu wamekuwa na wanaendelea kuutumia katika kujitibu maradhi mbalimbali yanayowakabili. Ni changamoto kwa watafiti na watalaamu kufanya tafiti zaidi za kisayansi ili kutambua jinsi mti huu unavyofanya kazi katika kutibu baadhi ya magonjwa na kuthibitisha pasi shaka uwezo wake katika kutibu ugonjwa wa Ukimwi na maradhi mengine sugu.

Marejeo

 1. www.worldagroforestry.org/treedb2/AFTPDFS/Carissa_edulis.pdf
 2. Leeuwenberg, A.J.M. & Kupicha, F.K. et al. (1985) Apocynaceae FZ 7(2)
 3. Kokwaro, J.O., 1976. Medicinal Plants of East Africa. East African Literature. Bureau, Nairobi, Kenya, pp. 1–8, 25–26.
 4. Lindsay, E.A., Berry, Y., Jamie, J.F., Bremner, J.B., 2000. Antibacterial compounds fromCarissa lanceolata R. Br. Phytochemistry 55, 403–406.
 5. Festus M. Tolo, Geoffrey M. Rukunga, Faith W. Muli, Eliud N.M. Njagi, Wilson Njue, Kazuko Kumon, Geoffrey M. Mungai, Charles N. Muthaura, Joseph M. Muli, Lucia K. Keter, Esau Oishi, Mawuli W. Kofi-Tsekpo, 2005. Anti-viral activity of the extracts of a Kenyan medicinal plant Carissa edulis against herpes simplex virus. Journal of Ethnopharmacology 104 (2006) 92–99. Inapatikana mtandaoni www.sciencedirect.co
 6. Ya’u J, Yaro AH, Abubakar MS, Anuka JA, Hussaini IM., 2008. Anticonvulsant activity of Carissa edulis (Vahl) (Apocynaceae) root bark extract. J Ethnopharmacol. 2008 Nov 20;120(2):255-8. Epub 2008 Sep 4. Inapatikana mtandaoni www.sciencedirect.com
 7. Nedi T, Mekonnen N, Urga K., 2004. Diuretic effect of the crude extracts of Carissa edulis in rats. J Ethnopharmacol. 2004 Nov;95(1):57-61. Inapatikana mtandaoni www.sciencedirect.com
 8. El-Fiky FK, Abou-Karam MA, Afify EA., 1996. Effect of Luffa aegyptiaca (seeds) and Carissa edulis (leaves) extracts on blood glucose level of normal and streptozotocin diabetic rats. J Ethnopharmacol. 1996 Jan;50(1):43-7. Inapatikana mtandaoni http://www.kau.edu.sa
Imesomwa mara 7538 Imehaririwa Alhamisi, 18 Julai 2019 17:08
Dr Fabian P. Mghanga

Daktari bingwa na Mhadhiri katika kitivo cha Afya Chuo Kikuu Kishiriki cha Askofu Jacob, Songea

Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.