Image

Pancake za Unga wa Mchele na Choroko

Leo katika makala hii, chef Issa anawaletea jinsi ya kuandaa chapati (pancake) za unga wa mchele na choroko, namna ya kupamba chakula na kukifanya kuwa cha mvuto kwa mlaji,

jinsi ya kupika viazi vya kukaanga na mchanganyiko wa mboga za majani, na jinsi ya kutengeneza halwa ya karoti.

Habari njema kwa wale wasiotumia nafaka aina ya ngano na wale wasiotumia mayai na wangependa sana kula chapati hizi za maji.

 

 

 

 

 

 

MAHITAJI

180 gram za mchele uliochemshwa

180 gram za mchele uwe wenye mbegu fupi nene

120 gram za choroko zilizotolewa ngozi

1/2 kijiko cha chai Fenugreek seeds (angalia chini hapo katika picha)

1-1/2 kijiko kidogo cha chai chumvi

Jinsi ya kuandaa fuatilia mafunzo hapa chini

 

 

 

 

 

 

Loweka choroko pamoja na fenugreek katika bakuli moja kisha loweka mchele katika bakuli jingine kwa masaa matatu tu.

 

 

 

 

 

 

Na huu ndio muonekano wa mbegu za fenugreek

 

 

 

 

 

 

 

Huu ni muonekano wa choroko

 

 

 

 

 

 

Unaweza tumia blenda au ukalowanisha grinder kusaga mchanganyiko wako. Kama unavyoona katika picha hapo mimi natumia grinder ndogo naiweka juu ya meza na huwa natumia kusagia vitu vingi kwa urahisi zaidi.

Kwa sasa weka mchele na maji kisha washa mashine iendelee kusaga au blenda.

 

 

 

 

 

 

Saga mpaka upate uji mzito. Hata baada ya kusaga kwa muda mrefu unaweza ona chenga chenga usikate tamaa ni kawaida na mchanganyiko wako uko safi kabisa. Mimina mchanganyiko wako katika bakuli pembeni.

 

 

 

 

 

 

Kisha usioshe blenda yako au mashine ya kusagia weka choroko na mbegu za fenugreek katika grinder pamoja na maji kiasi.

 

 

 

 

 

 

Saga tena upate mchanganyiko mzuri na mzito.

 

 

 

 

 

 

Kisha chukua mchanganyiko huo na changanya katika ule mchanganyiko wa mchele uliosagwa pia.

 

 

 

 

 

 

Hakikisha mikono yako ni safi na salama weka chumvi katika mchangayiko na changanya vizuri kwa kutumia mikono yako.

Sio lazima kutumia mikono unaweza tumia mwiko pia, lakini kumbuka joto la kwenye mikono yako linasaidia kufanya unga uchachuke vizuri pale unapouacha usiku mzima kabla ya kupika.

 

 

 

 

 

 

Weka mchangayiko wako katika bakuli safi kwa usiku mzima. Kama unaishi nchi au miji yenye joto unaacha tu nje itaumuka na kuchachuka safi sana ila kama unakaa nchi za baridi basi iwashe oven yako na kisha izime ipoe kiasi chukua unga wako na uweke humo ukae usiku mzima hakikisha oven imezimwa na joto ni dogo sana.

 

 

 

 

 

 

Siku inayofuata, changanya mchanganyiko wako safi. Kisha changanya vizuri tena mchanganyiko wako. Weka kikaango chako katika moto na kisha paka mafuta kiasi.

Huwa natumia kitunguu kilichokatwa kuenezea mafuta katika kikaango hii husaidia mchangayiko wako wa unga usigandie wakati unakaanga.

 

 

 

 

 

 

Chukua upawa na chota mchanganyiko anza kumimina kati kati ya kikaango.

 

 

 

 

 

 

Baada ya kumimina kiasi hakikisha unasambaza kwanza uone kama inatosha au uongeze.

 

 

 

 

 

 

Kiwango ni iwe nyembemba ili iweze kuiva kwa haraka

 

 

 

 

 

 

Acha iive kwa dakika 3 au mpaka uone mwisho mwa chapati kunajikunja na kuacha kikaango na kua na rangi ya kahawia. Hapo itakua rahisi kugeuza na kuivisha upande mwingine.

 

 

 

 

 

 

Geuza na pika tena kwa dakika 2.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Huu ndio muonekano saafi wa chapati yako ya maji na mchanganyiko wa mchele na choroko.

 

 

 

 

 

 

 

Baada ya kuiva ikunje nusu na mpatie mlaji ikiwa ya moto.Inakua na ubora wake endapo utampatia mlaji mara tu baada ya kuiva. Furahia chapati yako na Coconut Chutney, Tomato Chutney, Onion Chutney, Jam ya ladha yeyote au asali.

VIAZI VYA KUKAANGA NA MCHANGANYIKO WA MBOGA MAJANI

Viazi ulaya (Irish potato) oka kwenye oven pamoja na chumvi na mafuta kiasi na kitunguu swaumu.

Pili chukua pili pili hoho pamoja na nyanya mbivu pia oka kwenye oven lakini hakikisha zinaiva wastahi tu zisipondeke au kuiva sana pia kumbuka kuziwekea chumvi na mafuta kabla ya kuzioka.

Kisha kata kata kitunguu maji slice, majani ya kitunguu mabichi changanya katika viazi mchangayiko wote huo wa mboga majani hizi mbichi na zile za kuoka pia.

Kumbuka kuweka pili pili manga na tomato ketchup kidogo.

Hapa mlo kamili unakua umekamilika kwa wale wasio tumia nyama na pia kwa wanaotumia nyama chakula hiki unaweza kula nanyama ya samaki, kuku au mbuzi na ng'ombe pia.

Badilisha muonekano bora wa chakula nyumbani kwako familia ifurahie mapishi bora na chakula kitamu.

JIFUNZE KUPAMBA CHAKULA ILI KUONGEZA MVUTO KWA WALAJI

Muonekano wa chakula ni kivutio tosha kwa mlaji. Jitahidi kupamba chakula katika sahani ili kivutie walaji kwani mtu anaanza kula kwa macho hata kama chakula si kitamu lakini macho yakishapenda mlaji ataridhika na mapishi yako. Kupamba chakula si hotelini tu hata nyumbani unaweza pamba chakula chako na kikavutia sana.

WALI NYAMA, YAI LA KUKAANGA NA SALSA

 

 

 

 

 

 

 

Huu ni muonekano wa chakula safi sana na kwa muonekano wa macho na hata kwa ladha ni safi sana

Pika wali wako saafi kisha kaanga yai kwa pembeni jicho la ng'ombe (fried egg sun side up) kisha tengeneza salsa ya embe, nyanya na kitunguu weka pilipili manga, chumvi, limao na pilipili mbuzi kiasi sio lazima.

Kupamba katika sahani, chukua kibakuli au kikombe cha chupa ya chai kisha weka wali humo na kandamiza vizuri kisha geuza na weka katika sahani pembeni kama picha inavyoonyesha. Kisha weka salsa pembeni na yai la kukaanga.

Juu ya wali weka nyama au, kuku wa mchuzi mzito au samaki kisha juu yake unatupia karanga zilizookwa au korosho.

Chakula hiki kitakua na muonekano safi sana na mlaji atafurahia mchanganyiko wa ladha.

JIFUNZE KUANDAA CARROT HALWA

Kuandaa ni dakika30

Kupika ni dakika 30

Idadi ya watu kula ni 2

MAHITAJI

480 gram ya karoti ya kukwaruzwa (grated)

240 gram ya maziwa

1240 gram ya fresh cream

120 gram ya samli (ghee)

240 gram ya sukari

1 kijiko kidogo cha chai unga wa hiliki (cardamom powder)

1 kijiko kikubwa cha korosho zivunje vunje

Jinsi ya kuandaa fuatilia picha hapa chini

 

 

 

 

 

 

Pasha kikaango katika moto, kisha weka samli iyeyuke na weka karoti, kaanga mpaka upate harufu nzuri ya kuiva (distinct aroma).

 

 

 

 

 

 

Kisha weka maziwa pamoja na cream pika kwa dakika 10 mpaka maziwa na cream yakaukie kwenye karoti (absorbed).

 

 

 

 

 

 

Kisha weka sukari pamoja na hiliki pika mpaka ishikane kabisa.

 

 

 

 

 

 

Kisha chukua chombo chochote au kikombe na weka halwa yako kisha mimina katika sahani juu yake weka zile korosho zilizo kaangwa au kuokwa kama pambo kwa juu na pamoja kuongeza ladha. Pia unaweza tumia zabibu kavu (raisins) na zinapendeza sana.

 

 

 

 

 

 

Huu ni muonekano wa halwa ikiwa katika sahani tayari kwa kuliwa. Watengenezee familia yako wafurahie.

Imehaririwa Jumatano, 13 Juni 2018 16:35
Tagged under
Share
Issa Kapande

As Chef into with excellent qualification and a strong desire to excel in this professional in Hazard Analysis and critical control points (HACCP) which enable me to demonstrate my commitment to food safety and customer satisfaction, as well as continuously meeting the expectations of a changing world.

activechef.blogspot.com

Makala shabihana