Image

Saratani ya ubongo ni uvimbe uliotokana na mkusanyiko wa chembebehai za ubongo zilizotengenezwa kwa wingi bila mpangilio kutokana na kubadilika kwa DNA. Ikiwa chembehai hizo ni za kawaida basi uvimbe hujulikana kama BENIGN, na kinyume chake ni CANCER.

Saratani za ubongo ziko kwenye makundi makuu mawili; yaani PRIMARY ambayo imeanzia kwenye ubongo wenyewe au SECONDARY (METASTASIS) endapo imetokea sehemu nyingine ya mwili mbali na ubongo.

Ukweli kuhusu saratani za ubongo  

 • Kuna aina 120 au Zaidi za saratani ya ubongo.
 • Dalili na madhara yake hutegemeana na aina, ukubwa na mahali ilipo kwenye ubongo.

Vihatarishi vyake

 • Umri na jinsia ya kike.
 • Baadhi ya mionzi au mionzi tiba.
 • Baadhi ya magonjwa ya kinasaba kama vile Neurofibromatosis.
 • Saratani za sehemu nyingine za mwili kama vile tezi la thyroid, mapafu, titi na ini.

Dalili zake

 • Maumivu ya kichwa
 • Kupungua nuru ya macho au upofu.
 • Kupungua usikivu na kupepesuka.
 • Kupoteza kumbukumbu na haiba.
 • Kupooza mkono au mguu vya upande mmoja.
 • Kupata degedege ama kupoteza fahamu.
 • Kushindwa kumeza chakula.

Matibabu Yake

 • Kufanyiwa vipimo vya damu, CT scan ama MRI ya ubongo.
 • Kufanyiwa upasuaji na kupewa dawa

Kichwa kikubwa ni ugonjwa wa watoto wachanga wa kutanuka chemba za maji za kichwani na hivyo kupeleka muonekano wa kichwa kuwa mkubwa. Ugonjwa huu ni matokeo ya kuzalishwa kwa maji mengi kichwani ama kuziba kwa njia za kupitisha/kufyonzwa maji hayo.

Hutokana na sababu za kinasaba, hivyo mtoto kuzaliwa na kichwa kikubwa. Aina hii huambatana na matatizo mengine kama vile mgongo wazi (SPINE BIFIDA) na mguu kifundo (TALIPES). Sababu nyingine ni maambukizi ya mishipa ya fahamu pindi mtoto anapozaliwa au mara tuu baada ya kuzaliwa.

Ukweli kuhusu kichwa kikubwa  

 • Asilimia 50 ya watoto wa kichwa kikubwa huwa na changamoto ya ukuaji.
 • Kuanza matibabu mapema baada ya mtoto kuzaliwa hupunguza changamoto hizi za ukuaji.

Vihatarishi vyake

 • Ukosefu wa virutubisho (vitamins) aina ya folic acid wakati wa ujauzito.
 • Unywaji holela wa baadhi ya dawa za hospitali wakati wa ujauzito.
 • Ajali, hususani kwa watu wazima
 • BAADHI YA WATU WALIOZIDI MIAKA 60 (NORMAL PRESSURE HYDROCEPHALUS)

Dalili zake

Kwa watoto wachanga chini ya umri wa mwaka 1

 • Kulialia hovyo
 • Kushindwa kunyonya au kula vizuri.
 • Kuchelewa kukaza shingo
 • Kuvimba/kujaa utosi

Kwa watoto wakubwa na WATU WAZIMA

 • Kichwa kuuma
 • Kichefuchefu na kutapika
 • Matatizo ya kuona, kutembea, balance
 • Macho kuzama chini kamaa jua linalokuchwa

Matibabu yake

 • Kuwekewa mirija maalum ya kutoa maji (shunt)
 • Njia ya kisasa ya matundu (ETV)

Kipanda uso ni ugonjwa wa kinasaba unaosababisha maumivu makali ya kichwa kwenye paji la mbele la uso zikiambatana na dalili nyingine ambazo zinaathiri kazi za maisha ya kila siku. Kipanda uso husababishwa na shughuli zisizo tarajiwa kwenye ubongo. Shughuli hizi huweza kusababishwa na mambo mengi, hadi sasa bado haijafahamika ni kitu gani hutokea kusababisha shughuli hizi kutokea. Wanasayansi wengi wanaami kuwa kuna uvamizi hutokea kwenye ubongo ambao huusisha njia za fahamu (nerve pathways) na kemikali. Mabadiliko haya husababisha mabadiliko katika utembeaji wa damu kwenye ubongo ta tishu nyingine zinazouzunguka.

Kipanda uso ni ugonjwa unaotambuliwa kwa dalili zake tu (clinical diagnosis), hakuna kipimo cha maabara ama radiolojia ambacho kinaweza kutambua ugonjwa huu.

Ukweli kuhusu kipanda uso

 • Kinawaathiri wanawake kwa mara 3 zaidi ya wanaume kutokana na mvurugiko wa homoni zao.
 • Upo uwezekano wa asilimia 50 mtoto kurithi kutoka kwa mzazi mwenye ugonjwa huu.

Vihatarishi Vyake

 • Mabadiliko ya homoni kwa wanawake wakati wa hedhi, ujauzito au kukoma hedhi.
 • Unywaji kahawa kwa wingi na pombe.
 • Msongo wa mawazo
 • Mabadiliko ya hali ya hewa ama muda wa kulala.
 • Mwanga mkali ama harufu kali za utuli (perfume)
 • Baadhi ya vyakula ama kuruka baadhi ya milo (skipping meals)

Dalili zake

Hazifanani kwa watu wote. Mara nyingi ni kuumwa kichwa kunako ambatana na

 • Kichefuchefu na kutapika
 • Kichwa kuuma zaidi kwenye mazingira mwanga mkali au kelele.
 • Kukakamaa shingo
 • Wahka (mood changes)

Kinga (seeds technique)

 • Kulala kwa wakati kwenye chumba kisicho na mwanga (Sleep well)
 • Mazoezi unayoyapenda (Exercise)
 • Kula na Kunywa chakula vizuri (Eat well)
 • Kupanga ratiba zako vizuri (Diary)
 • Kupunguza mawazo (Stress Management)

Matibabu yake

 • Dawa za kutuliza maumivu ya kichwa
 • Sindano za kutuliza maumivu za kila mwezi

 

Kiharusi ni hali ya kuziba (ischemic) au kupasuka (hemorrhagic) kwa mishipa ya damu ya ubongo na kisha kupelekea ku ‘paralize’ au kifo. Kuna wakati ububu, uziwi, upofu hutokana na kiharusi.

Asilimia 85 ya kiharusi hutokana na kuziba kwa mishipa ya damu (ISCHEMIC STROKE). Aina ya pili ambayo hutokea kwa asilimia 15, hutokana na kupasuka kwa mishipa ya damu ya kwenye ubongo, kitaalamu hujulikana kama (HEMORRHAGIC STROKE); ni mbaya sana na mara nyingi hupelekea kifo.

Vihatarishi vyake

Kiharusi kinaweza kumpata mtu yeyote yule lakini wafuatao wana uwezekano Zaidi wa kupata kiharusi.

 • Mwenye historia ya kiharusi kwenye familia yake
 • Mwenye kisukari ambacho hakijathibitiwa
 • Mwenye shinikizo la damu (BP) ambayo halijathibitiwa
 • Mwenye maradhi ya mishipa ya damu ya ubongo, au maradhi ya moyo
 • Mwenye maradhi ya kukosa usingizi
 • Mwenye cholesterol nyingi, mnene wa kupindukia, Kutofanya mazoezi
 • Uvutaji wa sigara na Unywaji pombe
 • Utumiaji wa madawa ya kulevya

Dalili zake

 • Kushindwa kuongea au kutamka maneno sawasawa
 • Kupinda uso na kushindwa kutumia mkono ama mguu
 • Kizunguzungu na kukosa balance
 • Kutokuona vizuri
 • Kichwa kuuma

Matibabu yake

Kuwahi haraka hospitali kitengo cha dharura ndani ya saa 24 ili kupewa dawa ya kushusha shinikizo la damu na ubongo, na za kuzuiza kifafa; kisha kufanya vipimo vya kichwa yaani CT scan au MRI, na ultrasound.

Madaktari na wauguzi watakushauri kuhusu kuanza matibabu ya haraka ya kuzibua mishipa ya damu (Angiosuite) au kuondoa donge la damu kwa upasuaji (Theathre).

Baada ya kudhibiti hali ya dharura, utashauriwa kuanza mazoezi tiba (physiotherapy) pamoja na kuwaona jopo maalum la madaktari wa kiharusi.

Kifafa ni milipuko na mivurugano ya mfumo wa umeme wa kwenye ubongo kunakoweza kupelekea kupoteza fahamu kwa dakika kadhaa pamoja, kujikolea ama hata kutokwa na haja kubwa. Ugonjwa huu unaweza kufafanishwa na volcano za milima zinavyotokea. Baadhi ya vifafa huambatana na mabadiliko ya kitabia (psychosis).

Kitabibu, kuna aina mbili za Kifafa, aina ya kwanza kinaweza kutokea sehemu moja ya ubongo (focal) ama ubongo mzima (generalized).

UKWELI KUHUSU KIFAFA

 • Hakiambukizi
 • Hakitokani na laana

VIHATARISHI VYAKE

 • Homa kali kwa watoto wadogo
 • Mtu anayetoka kwenye familia yenye maradhi ya kifafa
 • Ajali za ubongo
 • Saratani za ubongo

DALILI ZAKE

Hutegemea sehemu gani ya ubongo ilipoanzia ila mara nyingi ni

 • Kukazia macho sehemu moja ama kuyapepesa haraka haraka kabla halijatokea
 • Kupumbazwa
 • Kutoka mate mdomoni na Kujing’ata ulimi
 • Kukakamaa mikono na/au miguu
 • Kupoteza fahamu na kisha kufuatiwa na Kujikolea na/au kujinyea
 • Kwa wale ambao hawajapoteza fahamu, kupoteza baadhi ya hisia za ladha, harufu na sauti.

 

MAKOSA WAKATI WA KUMHUDUMIA MGONJWA WA KIFAFA

 • Kumfunga Kamba
 • Kumpa kitu mdomoni

MATIBABU YAKE

Kumuacha mgonjwa wa kifafa kwa dakika chache mpaka pale litakaposimama lenyewe kama uko mbali na hospitali na kama haliachi basi kumkimbiza haraka hospitali kwa matibabu zaidi.  

Madaktari na wauguzi watamuanzishia dawa za kuchoma za kusimamisha degedege kisha kukushauri kuhusu kupima vipimo vya damu na EEG.

Baada ya kudhibiti hali ya dharura, ni vizuri ndugu wa karibu kufahamisha kuhusu kuzifahamu dalili za mgonjwa wao na jinsi ya kuishi nae ili kumuepusha na madhara Zaidi.