Pakua TanzMED App?

Hali ya dharura wakati wa ujauzito -1: Placenta abruption

Utangulizi

Miongoni mwa dharura zinazoweza kuwatokea baadhi ya wajawazito, ambayo husababisha mama kupoteza damu nyingi, kufa kwa mtoto na hata mama mwenyewe ni Placenta abruptio. Neno Placenta abruptio humaanisha hali ya kujitenga kwa kondo la nyuma (placenta) kutoka sehemu ilipojishikilia kwenye ukuta wa tumbo la uzazi (uterus) kabla hata ya mtoto kuzaliwa. Kondo la nyuma au placenta ni kiungo kinachofanya kazi ya kumlisha mtoto akiwa tumboni kwa mama yake. Katika hali ya kawaida, kondo la nyuma hujitenga na ukuta wa mfuko wa uzazi mara baada ya mtoto kuzaliwa.

Hali hii husababishwa na nini?

Sababu hasa za hali hii zaweza kuwa ngumu kuzibaini ingawa baadhi ya visababishi hivyo vyaweza kuwa

 • Kuumia eneo la tumbo kunakoweza kusababishwa na ajali za gari, kuangukia tumbo au kupata kipigo kikali
 • Kupoteza kwa kiasi kikubwa cha maji yaliyo katika mfuko wa uzazi (amniotic fluid). Maji haya yanaweza kupotea kwa njia nyingi ikiwemo kupasuka kwa chupa ya uzazi kabla ya wakati wake au mara baada ya pacha mmoja kuzaliwa iwapo mama mjamzito alikuwa na mapacha.

Je kuna vihatarishi vya Placenta abruption?

Ndiyo! Ukiacha visababishi vya hali hii, kuna mambo kadhaa yanayoelezwa kumuweka mjamzito katika hatari ya kupata tatizo hii. Vihatarishi hivi ni pamoja na

 • Tabia ya uvutaji sigara
 • Matumizi ya mihadarati kama vile kokeni.
 • Shinikizo la damu wakati wa ujauzito. Rejea makala http://www.tanzmed.com/?p=1143. Inaelezwa kuwa takribani nusu ya vifo vya watoto wachanga vinavyotokana na abruptio placenta husababishwa na shinikizo la damu wakati wa ujauzito.
 • Kuwa na magonjwa yanayoathiri mfumo wa kuganda kwa damu (thrombophilias)
 • Ugonjwawa kisukari
 • Unywajiwa pombe kupitiliza wakati waujauzito. Inaelezwa kuwa hali huwa mbaya zaidi kwa wajawazito wanaokunywa wstani wa chupa mbili za pombe kwa siku.
 • Kutanuka kwa mfuko wa uzazi kuliko kawaida hali ambayo inaweza kusababishwa na kuwwepo kwa kiasi kikubwa cha maji (amniotic fluid) au mapacha
 • Wale walio na historia ya kupata placenta abruption wana hatari ya kurudiwa rudiwa na tatizo hili
 • Kina mama ambao wamezaa watoto wengi kwa mfano waliowahi kuzaa watoto kuanzia sita na kuendelea
 • Kupata ujauzito ukiwa na umri mkubwa
 • Kupasuka kwa kuta za chupa kabla ya wiki 37 za ujauzito
 • Uwepo wa fibroids

Wajawazito wangapi hupatwa na tatizo hili?

Placental abruption ni tatizo ambalo linaendelea kongezeka sana nchini kwetu na sehemu mbalimbali duniani. Kwa mujibu wa shirika la Afya Duniani (WHO), kwa kila wajawazito 150 wanaojifungua duniani, mmoja hukumbwa na aina fulani ya tatizo hili. Hata hivyo ni mjamzito mmoja tu kati ya wajawazito 800 wanaojifngua, ambao hukumbwa na hali ya hatari zaidi ya tatizo hili, ambayo husababisha kifo cha mtoto na hata mama.

Dalili zake ni zipi?

Dalili za placenta abruption ni pamoja na

 • Maumivu ya tumbo
 • Maumivu ya kiuno na mgongo
 • Kuongezeka kwa maumivu ya uchungu
 • Uchungu wa kufululiza
 • Kutokwa na damu kwenye njia ya uzazi

Vipimo na uchunguzi

Vipimo vinavyoweza kufanywa kwa ajili ya tatizo hili ni pamoja na

 • Ultrasound ya tumbo au uke
 • Kipimo cha damu (Full blood picture) kwa ajili ya kuchunguza wingi wa damu, na mengineyo
 • Uchunguzi wa nyonga
 • Kumchunguza mtoto iwapo bado yu hai

Matibabu

Matibabu hujumuisha kumuongezea mjamzito maji kupitia mishipa ya damu (i.v fluids) au wakati mwingine kumuongezea damu. Mjamzito hana budi kuangaliwa na kufuatiliwa kwa ukaribu ili asipate dalili zozote za shock, wakati huohuo mtoto aliye tumboni naye hufuatiliwa kwa ukaribu ili kutambua uwepo wa dalili zozote zinazoashiria kuchoka (fetal distress) kama vile mapigo ya moyo ya mtoto yasiyo ya kawaida.

Karibu nusu ya watoto wanaozaliwa na mama wenye tatizo hili hupatwa na tatizo la kuchoka (fetal distress) mwanzoni kabisa mwa tatizo hili na takribani nusu ya wale wanaofanikiwa kuzaliwa wakiwa hai hupatwa na madhara mbalimbali mara baada ya kuzaliwa.

Iwapo mtoto amekomaa kiasi cha kutosha, na ikiwa mama ana uwezo wa kujifungua mwenyewe, mtoto anaweza kuzaliwa kwa njia ya kawaida ili mradi daktari ajiridhishe kuwa ni salama kwa mama na mtoto. Kinyume na hapo, mama anaweza kuhitaji kufanyiwa upasuaji wa dharura ili kumtoa mtoto.

Hata hivyo iwapo mtoto bado ni mdogo sana kiasi cha kushindwa kuishi iwapo atazaliwa na ikiwa kondo limejitenga kwa kiasi kidogo sana, mama anaweza kulazwa hospitali kwa muda kwa ajili ya uchunguzi na kufuatiliwa kwa ukaribu zaidi badala ya kumzalisha mtoto kwa upasuaji. Mama anaweza kuruhusiwa kutoka hospitali siku kadhaa baadaye iwapo hali yake itaonekana kutengemaa.

Matarajio

Kwa kawaida, ni nadra kwa mama mjamzito kufa kutokana na hali hii. Hata hivyo hii haimaanishi kuwa hali hii haiwezi kusababisha vifo vya mama wajwazito. Mambo yanayoweza kuchangia vifo vya wajawazito walio na hali hii pamoja na watoto wao ni:

 • Kuchelewa kugundulika kwa tatizo na kulishughulikia ipasavyo
 • Kupoteza damu kwa wingi mpaka mama kupata shock
 • Damu kuvuja ndani kwa ndani kwenye mfuko wa uzazi (uterus) bila kugundulika
 • Kufunga kwa shingo ya uzazi

Madhara

Kupoteza damu kwa wingi husababisha shock na hatimaye kifo kwa mama na/au mtot. Wakati mwingine, iwapo kutoka damu huku hakuwezi kuzuilika kwa njia nyingine yeyote ile, mama anaweza kuhitaji kufanyiwa upasuaji mkubwa ili kuondoa mfuko wa uzazi, hali ambayo itafuta kabisa uweoz wa kupata tena watoto maishani mwake.

Jinsi ya kujikinga na tatizo hili

Inawezekana kuzuia kutokea kwa placenta abruption kwa kuepuka mambo ambayo uhatarisha mama kupata tatizo hili. Mambo hayo ni pamoja na kuepuka uvutaji wa sigara, unywaji wa pombe kipindi cha ujauzito, matumizi ya mihadarati na kuhudhuria kliniki za mama wajawazito mapema.

Aidha kutambua na kutibu magonjwa kama kisukari au shinikizo la damu ni jambo la muhimu sana linalosaidia kupunguza hatari ya kupata placenta abruption.

Imesomwa mara 5329 Imehaririwa Ijumaa, 19 Mai 2017 08:20
Facebook Google Plus Twitter LinkedIn
Dr Fabian P. Mghanga

Daktari bingwa na Mhadhiri katika kitivo cha Afya Chuo Kikuu Kishiriki cha Askofu Jacob, Songea

Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.

Makala shabihana

No Internet Connection