Image

Hali ya dharura wakati wa ujauzito - 2: Placenta previa

Tunaendelea na mfululizo wa makala juu ya hali za dharura kipindi cha ujauzito. Leo tunazungumzia placenta previa. 

Placenta previa ni miongoni mwa hali za hatari na dharura inayowapata baadhi ya mama wajawazito ambapo kondo la nyuma hujipachika katika sehemu ya chini ya mfuko wa uzazi, kukua na kisha kufunika sehemu ndogo au kubwa ya njia ya uzazi inayoelekea kwenye shingo ya uzazi na hivyo kuzuia kabisa uwezekano wa mtoto kuzaliwa kwa njia ya kawaida.

Chanzo chake ni nini?

Wakati wa ujauzito, kondo huongezeka ukubwa na kutanuka kadiri jinsi mfuko wa uzazi unavyotanuka na kukua. Kipindi cha awali cha ujazito, ni jambo la kawaida kwa kondo kuwa maeneo ya chini ya mfuko wa uzazi (low-lying palcenta). Lakini, kadiri mimba inavyokua ndivyo mfuko wa uzazi unavyopaswa pia kulivuta kondo kutoka sehemu za chini na kulipandisha sehemu za juu za kuta zake. Mpaka ifikapo theluthi ya tatu ya ujauzito, kondo linapaswa kuwa karibu kabisa na juu ya mfuko wa uzazi ili kufanya njia ya uzazi kuwa wazi kwa ajili ya kurahisisha utokaji wa mtoto.

Hata hivyo, wakati mwingine hayo yote hushindikana kutokea hivyo kusababisha kondo kubakia sehemu za chini za mfuko wa uzazi, na hivyo kuziba kwa kiasi fulani au kuziba kabisa njia ya uzazi. Hali hii hujulikana kitaalamu kama previa.

Aina za placenta previa

Kuna aina kuu tatu za hali hii, nazo ni

 • Kondo huwa sambamba na shingo ya uzazi ingawa halifuniki njia ya uzazi. Aina hii hujulikana kitaalamu kama marginal placenta previa.
 • Kondo hufunika sehemu ndogo tu ya njia ya uzazi au kwa lugha nyingine huitwa partial placenta previa, na
 • Aina nyingine ni ile ambapo kondo hufunika kabisa njia ya uzazi au complete placenta previa.

Kundi gani la wajawazito hupatwa na tatizo hili?

Kwa mujibu wa takwimu za WHO, kwa kila wajawazito 200, mjamzito mmoja hupatwa na tatizo hili. Miongoni mwa wale wanaopatwa na hali hii, tatizo hili ni maarufu zaidi kwa wajawazito:

 • Wenye matatizo ya kimaumbile kwenye mfuko wa mimba
 • Walio na historia ya kupata mapacha mara nyingi zaidi
 • Wenye mimba za mapacha
 • Wenye makovu katika mfuko wa uzazi yanayotokana na ama kuwahi kufanyiwa upasuaji kipindi cha nyuma au waliowahi kutoa mimba (abortions)
 • Wanaovuta sigara
 • Walio na umri mkubwa

Makundi hayo mawili ya mwisho, yapo katika hatari kubwa zaidi ya kupata tatizo hili ukilinganisha na makundi yaliyotangulia kutajwa.

Placenta previa husababishwa na nini?

Sababu za tatizo hili ni pamoja na

 • Matatizo katika maumbile ya kondo
 • Matatizo ya maumbile ya mfuko wa uzazi
 • Hali ya kondo kuwa kubwa kuliko kawaida
 • Ukuta wa mfuko wa uzazi kuwa na makovu

Dalili zake ni zipi?

Dalili kuu ya tatizo hili ni kutokwa damu sehemu za ukeni kwa ghafla bila kujihisi maumivu yeyote yale. Mara nyingi kutoka damu huku hutokea karibu na mwisho wa theluthi ya pili au mwanzoni mwa theluthi ya tatu ya ujauzito.

Kwa baadhi ya wajawazito damu inaweza kutoka kwa kiasi kikubwa sana. Kutoka huku kwa damu kunaweza kuacha bila hata matibabu ingawa pia kunaweza kujirudia tena baada ya siku chache au hata wiki kadhaa.

Baadhi ya wajawazito hujihisi tumbo kukaza kipindi cha kutokwa damu, wakati wengine hupatwa na maumivu ya uchungu siku kadhaa baada ya damu kuendelea kutoka kwa wingi.

Baadhi ya wajawazito, hata hivyo, huanza kwanza kujihisi maumivu ya uchungu kabla ya kuanza kutokwa na damu.

Vipimo na uchunguzi

Kipimo kinachoweza kuonesha kwa usahihi kabisa kuwepo kwa tatizo hili ni ultrasound. Baadhi ya wajawazito hugundulika kuwa na tatizo hili mapema kabisa kipindi cha ujauzito hususani pale wanapohudhuria klinikli za wajawazito.

Vipimo vingine ni kama vilivyoainishwa kwenye makala iliyotangulia ya placenta abruption.

Matibabu

Matibabu hutegemea mambo kadhaa. Mambo hayo ni pamoja na

 • Kiasi gani cha damu kilichopotea
 • Iwapo mtoto amekomaa kiasi cha kuweza kuishi kama akizaliwa
 • Kiasi gani cha kondo kimefunika njia ya uzazi
 • Mtoto yupo sehemu gani katika mfuko wa uzazi
 • Mama ana watoto wangapi wanaoishi, na
 • Je mama ameshaanza uchungu ama bado

Imetokea mara nyingi sana, kondo hujisogeza lenyewe mbali na njia ya uzazi kabla hata njia ya uazazi haijafunguka. Hata hivyo, kuna nyakati ambapo hali hiyo haitokei.

Iwapo kondo lipo karibu na shingo ya uzazi au linafunika sehemu ndogo tu ya njia ya uzazi, mama hushauriwa kupumzika na wakati mwingine kutumia muda mwingi akiwa kitandani. Aidha daktari anaweza kushauri mama kutojamiiana na mumewe na kuacha kuingiza vitu ukeni kama vile kupitiliza kujisafisha ukeni au kuingiza vidole. Hii husaidia kupumzisha nyonga.

Iwapo damu itaanza kutoka ukeni, mama mjamzito hulazimika kulazwa hospitali kwa ajili ya kufuatiliwa kwa ukaribu zaidi.

Kwa mama aliyepoteza damu nyingi, anaweza kuhitaji kuongezewa damu. Aidha mama anaweza kupewa dawa za kuzuia uchungu kuanza kabla ya muda wake ili kumuwezesha mtoto afikie angalau wiki 36. Baada ya muda huo, mtoto anaweza kuzaliwa.

Daktari pia anaweza kupima madhara ya kuendelea kupoteza damu na madhara ya kuzalisha mtoto kabla ya muda wake na atakushauri kulingana na anavyoona inafaa.

Wajawazito wengi wenye tatizo hili uhitaji kufanyiwa upasuaji wa kutoa mtoto. Upasuaji husaidia kuondoa uwezekano wa mama au mtoto kufa kama mama ataachwa aendelee kupoteza damu au kama ataachwa ajaribu kujifungua mwenyewe. Mara nyingi, upasuaji wa dharura ufanyika iwapo kondo limefunika kabisa njia ya uzazi na damu inatoka kwa wingi kiasi cha kuhatarisha maisha.

Matarajio

Mara nyingi, tatizo hili hugundulika kabla hata mama hajaanza kutokwa na damu. Jambo la muhimu ni mama kuhudhuria kliniki inavyotakiwa. Ufuatiliaji wa karibu wa mama na mtoto wake aliye tumboni huzuia hatari nyingi zinazoweza kumpata mama na mtoto wake.

Hatari kubwa iliyopo ni kuwa, kutopoteza damu kwa kiasi kikubwa kunaweza kusababisha maamuzi ya kuzaliwa kwa mtoto kabla hata hajakomaa sawa sawa na baadhi ya viungo vyake vya muhimu kama vile mapafu kukomaa.

Hata hivyo, matatizo hayo na mengine mengi yanaweza kuepukwa iwapo mama mwenye tatizo hilo na ambaye ameonesha kuwepo kwa dalili zake, atalazwa hospitali na kisha kujifungua kwa upasuaji.

Madhara

Hatari kubwa za tatizo hili kwa mama mjamzito ni pamoja na

 • Kifo
 • Kupoteza damu kwa kiasi kikubwa
 • Kupata shock ambayo ina madhara kadhaa kwa viungo vya mwili ikiwemo kifo

Kuna hatari pia ya mama kupatwa na maambukizi ya bacteria, kuganda damu na pia madhara yanayohusiana na kuongezewa damu.

Mtoto pia anaweza kuzaliwa akiwa njiti (chini ya wiki 36) na hivyo kuongeza uwezekano wa kufariki, au kupoteza damu na kufa iwapo kondo litajitenga kutoka mfuko wa uzazi wa kati mama anapojifungua.

Kinga

Baadhi ya njia za kujikinga na tatizo hili ni pamoja na kujiepusha na mambo yanayoongeza uwezekano wa kutokea kwake. Mambo hayo ni kama kutobeba ujauzito katika umri mkubwa na kuepuka kuvuta sigara wakati wa ujauzito.

Imesomwa mara 15271 Imehaririwa Jumatatu, 18 Februari 2019 16:42
Dr Fabian P. Mghanga

Daktari bingwa na Mhadhiri katika kitivo cha Afya Chuo Kikuu Kishiriki cha Askofu Jacob, Songea

Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.

Makala shabihana