Image

Mafuta ya Nazi yanaweza kutibu Ugonjwa wa kusahau (Alzheimer’s Disease)?

Wiki chache zilizopita tuliandika makala kuhusu madai kuwa mafuta ya nazi yana uwezo wa kutibu ugonjwa wa kusahau unaowapata wazee maarufu kama Alzheimer’s disease. Katika makala hiyo iliyonukuliwa kutoka tovuti ya www.wavuti.com, mwandishi Dada Subi alijaribu kutoa rai kwa wataalamu wetu wa afya kufanya tafiti ili kuthibitisha madai ya uwezo huo wa mafuta ya nazi ili kusaidia kutatua tatizo hili ambalo limewakumba wazee wengi.

Katika kuzungumzia rai ya Dada Subi, msomaji wetu mmoja alituandikia maoni akitaka kufahamu hasa uhusiano kati ya mafuta ya nazi na uwezo wake katika kutibu ugonjwa huu. Ifuatayo ni makala inayojaribu kuzungumzia uhusiano kati ya mafuta ya nazi na jinsi inavyodaiwa kuwa na uwezo wa kutibu ugonjwa wa kusahau wa Alzheimers.........

Kumekuwepo taarifa kuhusu uwezo wa mafuta ya nazi kutibu ugonjwa wa kusahau unaowakumba wazee uitwao Alzheimer’s disease wakati huo huo ikiripotiwa kuwa baadhi ya dawa zilizokuwa zikitumika kutibu ugonjwa huo hapo awali zinaonesha kushindwa kufanya kazi inavyopaswa. Hivi karibuni, makampuni makubwa ya madawa duniani ya Pfizer yalikiri kuwa dawa mpya aina ya dimebon ilionesha kushindwa kutibu ugonjwa huo na huku ikifanya hali za wagonjwa kuzorota zaidi.

Wakati taarifa za kushindwa kwa dawa hizo zikizidi kutolewa, madaktari na watafiti wameendelea kutafuta mbinu nyingine za kukabiliana na ugonjwa huu. Mojawapo ikiwa ni matumizi ya mafuta nazi.

Watafiti wanasemaje?

Hivi karibuni, jarida la kitafiti la European Journal of Internal Medicine limewahi kuchapisha ripoti ya kitafiti inayozungumzia nafasi ya lishe katika kutibu ugonjwa wa kusahau wa Alzheimer’s. Watafiti waligundua kuwepo kwa uhusiano mkubwa kati ya ukinzani dhidi ya utendaji kazi wa homoni ya Insulin katika seli za ubongo na ugonjwa wa Alzheimers katika hatua zake za awali, hali iliyowafanya kufikiria kuwa pengine ugonjwa wa Alzheimers unafanana fanana na kisukari cha ubongo.

Walikwenda mbali zaidi na kudai kuwa hata vyanzo vya awali vya ugonjwa huu yawezekana vikawa na uhusiano mkubwa na mfumo wa usafirishaji wa lehemu (cholesterol) kutoka kwenye damu mpaka kwenye seli za ubongo, na kuna ushahidi kuonesha kuwa matatizo katika mfumo wa umeng’enyaji lehemu kwenye ubongo yanaweza kuchangia kusababisha ugonjwa wa Alzheimers.

Aidha ilionekana pia kuwa wagonjwa wa Alzheimers walikuwa na kiasi kidogo sana cha lehemu kwenye bongo zao. Kuwa na kiwango kikubwa cha lehemu kwenye ubongo kuna uhusiano mkubwa na kuishi muda mrefu kwa wazee wenye umri zaidi ya miaka 80, na wengine wameonekana kuwa na uwezo mzuri wa kukumbuka mambo mbalimbali.

Utafiti mwingine uliofanyika mwishoni mwa miaka ya 80 ukitumia panya wenye mimba waliolishwa chakula chenye mafuta ya nazi na wengine chakula chenye aina nyingine za mafuta (unsaturated oil) ulionesha kuwa vitoto vya panya waliozaliwa na panya waliolishwa chakula chenye mafuta ya nazi walikuwa na maendeleo mazuri katika ukuaji wa bongo zao ukilinganisha na vitoto vilivyozaliwa na panya waliokuwa wakilishwa chakula kilichowekwa aina nyingine za mafuta. Hii imehusishwa na uwezo wa mafuta ya nazi kusaidia utendaji kazi wa tezi ya thyroid ambayo uhusika na ukuaji wa ubongo kwa watoto wadogo.

Mafuta ya nazi yanafanyaje kazi kutibu Ugonjwa wa kusahau?

Uzito wa ubongo ni asilimia 2 tu ya uzito wa mwili mzima, lakini seli zake zinachukua karibu robo ya lehemu yote iliyopo kwenye mwili wa binadamu. Kazi ya lehemu katika ubongo ni kutengeneza viasili vinavyosaidia kuondoa sumu kwenye seli (antioxidants0, kufunika seli za ubongo ili kuzuia kuvuja kwa madini (cellular ions leakage), na pia kuzipa seli umbo linalotakiwa.

Pia husaidia kusafirisha vichocheo (neurotransmitters) vinavyopeleka taarifa kutoka sehemu moja ya ubongo mpaka sehemu nyingine, na kutengeneza na kuimarisha utendaji kazi wa sinapsi (synapses) au sehemu zinapokutana neva mbili kwa ajili ya kubadilishana taarifa.

Tofauti na aina nyingine, mafuta ya nazi yana kiasi kikubwa cha mafuta yajulikanayo kitaalamu kama saturated oils. Tofauti na unsaturated oils, saturated oils hayawezi kuvunjwa vunjwa kirahisi (oxidation) kutengeneza aina/zao nyingine. Mafuta yenye sifa ya namna hii ni muhimu sana kwenye utendaji kazi wa ubongo kwa vile yanakuwa na uwezo wa kudumu muda mrefu bila kubadilishwa kwenda aina nyingine ya mafuta.

Faida nyingine ya mafuta ya nazi ni kuwa na uwezo wa kuupa ubongo chakula maalum kinachofanya seli zake ziweze kujitengenezea nishati. Uharibifu katika seli za ubongo unaotokana na ugonjwa wa Alzheimer’s husababisha seli hizo kushindwa kutumia sukari (glucose) kujitengezea nishati na pia kuziwezesha zifanye kazi zake sawasawa.

Katika mazingira ambapo, glucose huwa kidogo mwilini, kwa mfano mtu unapofunga kula, au kufanya mazoezi makali kupita kiasi au kwa watoto wachanga waliozaliwa, ubongo hutumia vitu vinavyoitwa ketone bodies (ketones) kuzalisha nishati ili kuhuisha seli zake.

Kadhalika mgonjwa wa Alzheimers, seli za ubongo wake nazo hutumia ketones moja kwa moja ili kujitengenezea nishati ya kuziwezesha kuishi kwa muda mrefu zaidi. Mafuta ya nazi yana kiasi kikubwa sana cha viasili vinavyoitwa medium chain triglycerides. Unapokula mafuta ya nazi, mwili huvunja vunja mafuta hayo na kuzalisha ketone bodies kwa wingi, ambazo hatimaye hutumiwa na seli za ubongo.  

Changamoto zilizopo

Pamoja na kwamba kuna tafiti kadhaa zilizofanyika kujaribu kubainisha faida za mafuta ya nazi kiafya hususani ya ubongo, bado hakuna tafiti zilizoshirikisha idadi kubwa ya wagonjwa wa Alzheimers mpaka sasa kuchunguza ufanisi wa mafuta ya nazi kwa wagonjwa wa kusahau. Hata hivyo wanasayansi bado wanaendelea kuchunguza madai ya uwezo huu wa mafuta ya nazi na bila shaka jibu la uhakika litapatikana siku za usoni.

Marejeo

1. http://abcnews.go.com/Health/Alzheimers/pfizers-promising-alzheimers-drug-fails-study/story?id=9998774

2. Seneff S, et al, Nutrition and Alzheimer’s disease: The detrimental role of a high carbohydrate diet, Eur J Intern Med (2011). Inapatikana mtandaoni kupitia linki hii
3. http://www.coconutoil.com/ray_peat_coconutoil.htm
4. Reger MA, Henderson ST, Hale C, Cholerton B, Baker LD, Watson GS, Hyde K, Chapman D, Craft S. Effects of beta-hydroxybutyrate on cognition in memory-impaired adults. Neurobiol Aging, 2004 Mar;25(3):311-4. Inapatikana mtandaoni kupitia link hii

Imesomwa mara 10717 Imehaririwa Jumatatu, 28 Januari 2019 08:59
Dr Fabian P. Mghanga

Daktari bingwa na Mhadhiri katika kitivo cha Afya Chuo Kikuu Kishiriki cha Askofu Jacob, Songea

Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.

Makala shabihana