Utafiti uliofanyika nchini Uingereza kwa kuhusisha wanawake 46,000 umesema ya kwamba matumizi ya dawa za uzazi wa mpango hupunguza hatari ya kupata saratani ya mayai ya mwanamke (ovarian cancer), saratani ya mfuko wa kizazi (uterine cancer) na ya utumbo mpana wa chakula (bowel cancer).Watafiti hao wamesema kinga anayopata mwanamke dhidi ya saratani hizi kutokana na matumizi ya dawa hizi za uzazi wa mpango ni ya muda mrefu mpaka miaka 35 baada ya mwanamke huyo kuacha kutumia dawa hizi za uzazi wa mpango.
Katika utafiti huu, wanawake wa Uingereza walitumia dawa hizi za uzazi wa mpango kwa wastani wa miaka mitatu na nusu wakati wakiwa na umri kati ya miaka 20 mpaka miaka 30.Kinga dhidi ya saratani kwa wanawake hawa waliotumia dawa hizi za uzazi wa mpango kipindi cha ujana wao ilionekana kuwepo mpaka walipotimiza miaka 50, 60 na 70, umri ambao wanawake wanakuwa kwenye hatari kubwa ya kupata saratani.
Watafiti hawa kutoka chuo kikuu cha Aberdeen nchini Uingereza,waliendelea kusema ya kwamba wanawake waliotumia dawa za uzazi wa mpango walikuwa na hatari pungufu ya theluthi moja kupata saratani ya mayai ya mwanamke au saratani ya ukuta wa mfuko wa kizazi cha mwanamke (endometrial cancer).Pia wanawake hawa waligundulika kuwa na hatari pungufu ya moja ya tano kupata saratani zozote zile ikilinganishwa na wanawake ambao hawakutumia dawa hizi za uzazi wa mpango.
Karibia wanawake milioni 3.5 nchini Uingereza hutumia njia hii ya uzazi wa mpango kama njia rahisi kwao. Utafiti huu uliochapishwa katika jarida la American Journal of Obstetrics and Gynaecology utabadilisha mtazamo wa watu kuhusu athari na faida za dawa hizi za uzazi wa mpango.
Mara nyingi wanawake wameambiwa ya kwamba dawa za uzazi wa mpango zinawaweka kwenye hatari ya kupata saratani ya matiti au ya shingo ya kizazi (cervical cancer) lakini utafiti huu umeonyesha hatari hii huondoka kabisa ndani ya miaka mitano baada ya mwanamke kuacha kutumia dawa hizi za uzazi wa mpango.Wakati mwanamke anapotimiza umri wa kukoma kupata hedhi, kipindi ambacho kwa kawaida huongeza hatari ya kupata saratani za aina tofauti tofauti, lakini kwa wale ambao walitumia dawa za uzazi wa mpango hapo awali hawako kwenye hatari yoyote ile ya ziada ya kupata saratani, walisema watafiti hao kutoka nchini Uingereza.
Watafiti hao wanasema ‘’Matokeo haya ni uthibitisho mzito kwamba wanawake wanaotumia dawa za uzazi wa mpango hawajiweki kwenye hatari ya kupata saratani bali kuna uwezekano mkubwa kwamba dawa hizi huwakinga dhidi ya saratani’’.
Matokeo ya utafiti huo yanaonyesha ya kwamba katika kila wanawake 100,000 ambao walitumia dawa za uzazi wa mpango, ni wanawake 22 pekee ambao walipata saratani ya mayai ya mwanamke ikilinganishwa na wanawake 33 waliopata saratani hiyo kutoka kwenye kundi la wanawake wasiotumia (control group) dawa za uzazi wa mpango .
Hata hivyo, wanawake 48 waliotumia dawa za uzazi wa mpango walipata saratani ya utumbo mpana ikilinganishwa na wanawake 59 waliopata saratani ya hiyo kwa wale wale ambao hawakutumia dawa za uzazi wa mpango hapo awali.
Vilevile wanawake 19 walipata saratani ya ukuta wa kizazi (endometrial cancer) kwa wale waliotumia dawa za uzazi wa mpango wakati wanawake 30 walipata saratani hiyo kwa wale ambao hawakutumia dawa za uzazi wa mpango hapo awali.
Dawa za uzazi wa mpango hufanya kazi kwa kuongeza viwango vya vichocheo aina ya oestrogen na progesterone ambavyo huzuia mayai ya mwanamke kuwa kwenye hali ya utungwishwaji mimba.
Tafiti nyingi za nyuma zilijielekeza kwenye ongezeko la kiwango cha oestrogen ambacho uhusishwa na kuongezeka kwa hatari ya kupata saratani ya matiti na ya shingo ya kizazi kwa wanawake.Wanasayansi wanafikiri kwamba zuio la mayai ya mwanamke la kutoingia kwenye utayari wa kushika mimba ndio linalochangia kupungua kwa nusu hatari ya kupata saratani ya mayai ya mwanamke na ya shingo ya kizazi.Hata hivyo watafiti hao hawana uhakika kwa nini hatari ya kupata saratani ya utumbo mpana imepungua kwa wanawake waliotumia dawa za uzazi wa mpango.
Kutokana na utafiti huu ni dhahiri kabisa kuwa matumizi ya dawa za uzazi wa mpango ni salama na humkinga mwanamke kutopata saratani nilizotaja hapo juu, hivyo ni vyema kuepuka fikra potofu juu ya matumizi ya dawa hizi.