Image

Muda gani inafaa kubeba mimba baada ya mimba uliyobeba kuharibika?

Swala hili limekuwa likiwatatiza wamama wengi wanaopatwa na tatizo la mimba kuharibika.

Ni vizuri kwanza kujua vitu vinavyoweza kusababisha mimba kuharibika.

Mimba nyingi huharibika kutokana na makosa ya ukuaji wa mtoto. Sehemu kubwa ya makosa haya huwa ni kwenye vinasaba vyake. Yanaweza kuwa ya kurithi au yasiyo ya kurithi yaliyotokea kwa bahati mbaya kwa mtoto.

Zipo pia sababu nyingine kama vile maumbile ya viuongo vya uzazi, magonjwa ya mama kama vile kisukari, magonjwa ya damu, magonjwa ya vijidudu (infection).

Pamoja na sababu za mimba kuharibika kuwa nyingi, mara nyingi linapotokea tatizo hili huwa sababu iliyosababisha haifahamiki. Hali hii husababisha akinamama wengi na wenza wao kubaki na maswali mengi kwanini imewatokea hivyo na hujiuliza kama inaweza kutokea tena kwenye ujauzito mwingine.

Mara nyingi hali hii hutokea mara moja na haijirudii. Hii ni kwa sababu makosa ya ukuaji yanayotokea bahati mbaya huwa ni jambo lenye uwezekano mdogo sana kujirudia. Hata hivyo iwapo ujauzito umeharibika kwa sababu nyingine kama vile za kimaumbile au magonjwa ya damu, uwezekano wa kujirudia huwa mkubwa iwapo hali hiyo haijagundulika na hatua stahiki kuchukuliwa.

Kujibu swali la msingi ni baada ya muda gani inafaa kubeba mimba nyingine, inategemea kama ni mara ya kwanza ujauzito kubadilika au ni hali iliyojorudia. Kama ni mara ya kwanza, unaweza kubeba ujauzito mwingine mara tuu unapopata siku zako (vizuri zaidi angalau baada ya wiki 6 baada ya ujauzito kuharibika). Kwa kipindi hiki mwili unakuwa tayari kupokea ujauzito mwingine.
Hata hivyo kwa vile swala la ujauzito kuharibika linapokelewa kwa hisia tofauti na linaowakuta, ni vizuri ukabeba ujauzito baada ya kuwa umeshakuwa katika hali ya kawaida kihisia.

Iwapo ujauzito kuharibika sio mara ya kwanza, kuna umuhimu wa kufanyiwa vipimo na daktari ili upewe ushauri juu ya kujiandaa na ujauzito mwingine. Aina ya ushauri inategemea na matokeo ya vipimo atakavyoshauri daktari. Vilevile inategemea kama ujauzito (mtoto) ulioharibika ulikutwa na tatizo lolote linalohitaji muda kulichunguza. Vipimo hivi vinaweza kuwa pamoja na vipimo vya damu, kipimo cha ultrasound na vingine.

Daktari anaweza kushauri utumie dawa za folic acid au vitamin wakati ukijiandaa na ujauzi mwingine.

Wanawake wengi (asilimia 70) waliopata tatizo la ujauzito kuharibika walifanikiwa kupata ujauzito tena na kujifungua watoto wenye afya njema. Kwahiyo usikate tamaa iwapo umekutwa na hali hii.

 

Picha, special thanks to: Ms Lucy Vicent

 
Imesomwa mara 25481 Imehaririwa Alhamisi, 20 Desemba 2018 13:17
Dr Khamis

Dr. Khamis H.Bakari (MD PhD) ni daktari bingwa,mhadhiri katika chuo cha afya cha Chuo  Kikuu cha Dodoma,mtaalamu wa Tiba na Uchunguzi kwa kutumia mionzi ya nyuklia (Nuclear medicine).

Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.

Makala shabihana