Image

Kiwango gani cha pombe ni salama kwa mama mjamzito?

Utangulizi:

Labda umekua ukijiuliza kwanini mwanamke hatakiwi kunywa pombe wakati wa ujauzito, na je pombe kiasi gani inaleta madhara kwa mtoto ambaye yuko tumboni. Madhara hayo kama yapo ni yapi?

Katika makala hii tutaenda kujifunza kuhusu FASD (fetal alcohol spectrum disorder)na FAS (fetal alcohol syndrome) dalili zake , madhara yake na matibabu. Lakini pia tutajibu swali lililo hamasisha makala hii.

FASD

 FASD  ni wigo mpana wa dalili zinzoweza kumuathiri mtoto aliye tumboni baada ya mama kutumia pombe wakati wa ujauzito, Wigo huu huanzia dalili ndogo ndogo hadi dalili kubwa zaidi. Dalili kubwa zaidi ndio hujulikana kama FAS ( Ugonjwa wa pombe kwa mtoto aliye tumboni).

Pombe ni teratojeni inayojulikana wazi na inaweza kusababisha madhara makubwa kwa maendeleo ya mtoto pindi akiwa tumboni, ambayo yanaweza kudumu maisha yote.

FASD ni moja ya sababu kuu ya ulemavu wa akili ambao hauhusiani na urithi wa kijenetiki.

Epidemolojia

“Uchambuzi wa hivi karibuni wa meta ulithamini kwamba kiwango cha ulimwengu cha Ugonjwa wa Pombe kwa Watoto (FASD) katika idadi ya watoto na vijana (miaka 0–16.4) ni 7.7 kwa kila watoto 1000” (Symons and Pedruzzi #).

“Hatari ya mama kuzaa mtoto mwenye FASD ina visababishi vingi”. Hii inamaanisha kwamba hatari anazoweza kukabiliana nazo mama wakati wa ujauzito zinaweza kuwa za aina nyingi na zinaweza kuathiriwa na mambo tofauti. (May & Gossage, 2011, #)

Dalili za FASD

Kasoro za Kimwili

Kasoro za kimwili zinaweza kujumuisha:

  • Sifa za uso wa kipekee kama kuwa na macho madogo, mdomo wa juu mwembamba sana, pua ndogo inayopanda juu na ngozi laini isiyokua na mikunjo kati ya pua na mdomo wa juu,masikio yaliyo shuka chini.
  • Ukuaji wa mwili wa duni wakati wa ujauzito na baada ya kuzaliwa.(kuchelewa kukaza shingo, kukaa,  kutambaa, kusimama, kuongea n.k)
  • Maumbile yasiyo ya kawaida kwenye mikono na vidole.
  • Matatizo ya kuona na kusikia.
  • Kichwa kidogo na/au ubongo mdogo.
  • Kasoro za moyo na matatizo ya mifupa na figo

 

Matatizo ya Ubongo na Mishipa ya fahamu

Matatizo ya ubongo na mishipa ya fahamu yanaweza kujumuisha:

  • Ukosefu uratibu (co-ordination)
  • Kumbukumbu duni
  • Matatizo ya kutulia na kuchakata taarifa
  • Ulemavu wa akili na kuchelewa kwa maendeleo ya ukuaji
  • Ulemavu wa kujifunza
  • Kutoweza kuelewa matokeo ya vitendo
  • Hoja duni na kushindwa kutatua matatizo 

Matatizo ya Tabia

Matatizo ya katika kufanya kazi na kuwasiliana na wengine yanaweza kujumuisha:

  • Ujuzi duni wa kujichanganya katika jamii (poor social skills)
  • Ugumu wa kuungana au kujumuika na wenzao
  • Kushindwa kuzoea mabadiliko
  • Ugumu wa kuzingatia majukumu 

Madhara ya FASD

  • Ulemavu wa kujifunza na matatizo ya akili.
  • Matatizo ya kitabia na kijamii.
  • Matatizo ya afya ya akili kama vile wasiwasi na unyogovu.
  • Matatizo ya mwili, kama vile kasoro za moyo, matatizo ya kusikia na kuona. 

Je, kiwango gani cha pombe ni hatarishi kwa mtoto alieko tumboni?

Hakuna kiwango cha pombe kinachojulikana kuwa ni salama kwa mama mjamzito. Hivyo basi, Inashauriwa kwamba wanawake wajawazito wasitumie pombe kabisa ili kuepuka hatari ya matatizo kama Ugonjwa wa Pombe kwa mtoto alieko tumboni (FASD).

Ili kuwa salama jua kwamba viwango vyote vya pombe ni hatarishi kwa mama mjamzito na mtoto aliye tumboni.

 Utambuzi na Matibabu

    Utambuzi:

Wakati bora wa kugundua Ugonjwa wa Pombe kwa watoto walio tumboni (FAS) au FASD ni wakati wa kuzaliwa, lakini kesi nyingi hazigunduliwi hadi umri wa mtoto kuanza shule. Uchelewaji huu unasababishwa  hasa na wataalamu wa afya kushindwa kukusanya taarifa za matumizi ya pombe kwa mama wakati wa ujauzito kama inavyotakiwa kwasababu ya kukosekana  utayari wa mama mjamzito kukubali au kusema kama alikuwa anatumia pombe wakati wa ujauzito. Hii hufanya  utambuzi kuwa mgumu kipindi mtoto akiwa mchanga.

Zaidi ya hayo, sifa za kipekee za uso zinaweza zisionekane wazi awali ila zikawa dhahiri kadri mtoto anavyoendelea kukua na kufikia ujana.

     Matibabu:

Ingawa hakuna tiba ya FASD na FAS, kuna matibabu yanayoweza kufanyika kusaidia kuboresha maisha ya walioathirika. Matibabu yanaweza kujumlisha:

  • Elimu maalum na msaada wa kujifunza.
  • Tiba ya usemi na lugha. (speech therapy)
  • Tiba ya mwili na kazi. (physiotherapy and occupational therapy)
  • Huduma za afya ya akili na ushauri.

Hitimisho

FASD na FAS inaweza  kuzuilika kabisa kwa kuepuka pombe wakati wa ujauzito!!

Ni muhimu kwa wanawake kuelewa hatari za matumizi ya pombe wakati wa ujauzito na kutafuta msaada wa matibabu ikiwa wanajikuta wakiwa na shida ya kuacha pombe wakati wa kujaribu kupata mtoto au wakati wa ujauzito. 

Marejeleo

  1. Medscape
  2. Journals
  • May PA, Gossage JP. Maternal risk factors for fetal alcohol spectrum disorders: not as simple as it might seem. Alcohol Res Health. 2011;34(1):15-26. PMID: 23580036; PMCID: PMC3860552.
  • Symons, M., Pedruzzi, R.A., Bruce, K. et al. A systematic review of prevention interventions to reduce prenatal alcohol exposure and fetal alcohol spectrum disorder in indigenous communities. BMC Public Health 18, 1227 (2018). https://doi.org/10.1186/s12889-018-6139-5

 

Imesomwa mara 478 Imehaririwa Jumanne, 08 Oktoba 2024 10:05
Dr Ladina Msigwa

Distinguished medical doctor and acclaimed author with a passion for enhancing healthcare and sharing knowledge through the written word.

Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.