Image

Ufahamu Ugonjwa wa Alzheimer's

Utangulizi

Ugonjwa wa Alzheimer's ni miongoni mwa magonjwa ya ubongo yanayoathiri zaidi wazee au watu wa umri wa makamo. Ugonjwa huu ambao huanza polepole na kuchukua muda mrefu kujitokeza kwa kawaida hauoneshi dalili ya kupata nafuu mara unapoanza.

Ugonjwa wa Alzheimers’s ni miongoni mwa makundi ya magonjwa ya akili yanaitwa kitaalamu kama dementia na ambao huathiri zaidi watu wenye miaka 65 au zaidi.

Ugonjwa wa Alzheimer’s unasababishwa na nini?

Mpaka leo hii, chanzo halisi cha ugonjwa wa Alzheimer’s bado hakijajulikana. Hata hivyo, kuna nadharia kadhaa zilizoibuliwa na wanasayansi kuhusiana na baadhi ya visababishi vya ugonjwa huu. Nadharia inayoonekana kukubalika mpaka sasa ni ile ya uhusiano wa kuwepo kwa jamii ya protein inayoitwa amyloid na ugonjwa huu.

Wanasayansi wameonesha kuwa mabadiliko katika vinasaba vinavyodhibiti uzalishwaji wa protini hii ya amyloid ndiyo chanzo kikuu cha ugonjwa huu. Aidha ushahidi uliooneshwa na watafiti hao unasema kuwa mabadiliko haya ya vinasaba yamethibika kwa takribani zaidi ya nusu ya wagonjwa wote waliogunduliwa kuwa na ugonjwa huu.

Katika wagonjwa wote hawa waliofanyiwa utafiti imeonekana kwamba mabadiliko hayo ya vinasaba yamesababisha uzalishwaji uliopitiliza katika ubongo wa aina fulani ya vipande vya protini ijulikanayo kitaalamu kama ABeta (Aβ). Wataalamu wengi wanaamini kuwa, kukosekana kwa udhibiti wa uzalishaji wa aina hii ya protini kunakosababisha protini hii kuwa nyingi mno kwenye ubongo kuliko inavyoweza kuharibiwa ndiko kunakosababisha ugonjwa huu.

Aidha kulundikana kwa aina hii ya protini katika seli za nyuroni za ubongo hunasabisha kufa kwa baadhi ya seli hizo hali ambayo husababisha kukosekana kwa muunganiko katika utendaji kazi wa baadhi ya nyuroni fulani fulani katika ubongo kitu amabcho husabaisha kutokea kwa ugonjwa huu.

Dalili za Ugonjwa wa Alzheimer’s

Dalili za ugonjwa wa Alzheimer’s hutegemea na hatua au ngazi iliyofikiwa na ugonjwa. Kuna hatua kuu saba za ugonjwa huu. Hata hivyo ieleweke kuwa, dalili za ugonjwa huu hutofautina kati ya mgonjwa na mgonjwa na wakati mwingine dalili zinazoweza kujitokeza katika hatua fulani ya ugonjwa kwa mgonjwa mmoja zinaweza zisijitokeze kwa mgonjwa mwingine. Hivyo hatua hizi ni kama muongozo tu uliowekwa kwa ajili ya utafiti na matibabu.

Hatua ya kwanza

mgonjwa haoneshi dalili zozote za ukosefu wa kumbukumbu

Hatua ya pili

mgonjwa anaweza kuwa na matatizo ya kutambua baadhi ya vitu, hali ambayo inaweza kuchukuliwa kuwa ni ya kawaida kulingana na umri wake

Hatua ya tatu

huendana na kupungua kwa kiasi fulani kwa uwezo wa kutambua baadhi ya vitu, watu au mambo fulani fulani

Hatua ya nne

uwezo wake wa kutambua hushuka zaidi na huweza kuonekana hata kwa baadhi ya wanafamilia. Kwa mfano, mgonjwa anaweza kuonesha dalili ya kusahau matukio ya siku za karibuni, anaweza hata kusahau yeye ni nani, anaweza kushindwa kufanya vitu vinavyohitaji umakini kama kupanga bajeti ya familia au hata kushindwa kufanya hesabu ndogo ndogo

Hatua ya tano

mgonjwa wa Alzheimer’s huonesha mapungufu ya waziwazi katika uwezo wake wa kutambua vitu na wakati mwingine huihitaji msaada wa kufanya baadhi ya mambo ambayo hapo mwanzo alikuwa anaweza kuyafanya bila msaada wa mtu. Kwa mfano mgonjwa anaweza kusahau wapi alipo au kushindwa kutambua muda au jina la siku. Pia mgonjwa anaweza hata kuhitaji msaada wa kuchagua mavazi ya kuvaa kuendana na tukio au kusahau baadhi ya wanandugu katika familia yake. Hata hivyo pamoja na dalili zote hizo, katika hatua hii mgonjwa bado ana uwezo wa kujilisha mwenyewe au kwenda haja bila kuhitaji msaada wa mtu

Hatua  ya sita

hali ya utambuzi ya mgonjwa huwa mbaya zaidi. Mgonjwa huweza kusahau hata jina lake mwenyewe, hushindwa kuvaa vizuri bila kusaidiwa, huweza kutofautisha sura za watu anaoishi nao lakini hushindwa kukumbuka majina yao, hupata mabadiliko makubwa katika ratiba zao za kulala, kwa mfano huweza kukesha muda mwingi wa usiku na kulala muda mwingi wa mchana, hushindwa kudhibiti vibofu vyao hivyo kupelekea kujisaidia haja ndogo na wakati fulani haja kubwa bila kujitambua, huonesha mabadiliko makubwa ya kitabia na wakati mwingine huweza kuhisi kuwa baadhi ya watu wanaoishi nao hawana nia njema nao au wanataka kuwadhuru, huonesha tabia za kutangatanga au wakati mwingine huonekana kama mtu aliyepotea na huwa na tabia za kurusharusha mikono bila kutulia

Hatua ya saba

huambatana na dalili za mgonjwa kushindwa kujidhibiti mwenyewe, mgonjwa huitaji msaada kwa karibu kila tendo alifanyalo. Aidha mgonjwa hupoteza kabisa uwezo wa kukabiliana na mazingira yake. Katika hatua hii, mgonjwa anaweza kuhitaji msaada kwa mfano wa kulishwa au kujisaidia kama mtoto. Mgonjwa hawezi kukaa mwenyewe bila kushikiliwa au kuegemea mahali na hushindwa kabisa kuhimili hata vichwa vyao. Mgonjwa hupoteza uwezo wake wa kutabasamu na muda mwingi huonekana mtu aliye na huzuni. Katika hatu za mwisho mwisho kabisa, misuli ya mwili hukakamaa na mwisho mgonjwa hushindwa hata kumeza chakula au maji.

Utambuzi wa Ugonjwa wa Alzheimer’s

Mpaka sasa hakuna kipimo chochote maalum kinachoweza kugundua kwa ufasaha ugonjwa huu. Hivyo basi, ugonjwa huu, hutambuliwa kwa kuangalia dalili za mgonjwa na kwa kupata historia yake kutoka kwa ndugu au watu wanaomtunza. Aidha daktari atamchunguza mgonjwa na kujiridhisha kuwa

  • Mgonjwa ana dalili zote zinazoonesha kupungua kwa uwezo wake wa utambuzi na kiakili
  • Hatua alizopitia mgonjwa na kufikia zinaoendana na kufanana na zile hatua saba zilibainishwa hapo juu
  • Mgonjwa hana ugonjwa mwingine wowote uliosababisha matatizo haya ya akili au utambuzi

Aidha ili kuwa na uhakika kuwa hali hii ya kupoteza kumbukumbu haisababishwi na magonjwa mengine kama kiharusi, uvimbe kwenye ubongo, VVU, kaswende sugu au hata vimelea vya uti wa mgongo, mgonjwa pia hufanyiwa uchunguzi wa hali ya juu ili kuondoa uwezekano wa kuwepo kwa magonjwa haya.

Tiba ya Ugonjwa wa Alzheimer's

Matibabu ya ugonjwa huu yamegawanyika katika sehemu mbili, yale ya kutumia dawa na huduma kwa wagonjwa zinazoweza kutolewa nyumbani na wanafamilia.

Baadhi ya dawa zilizothibitishwa ana ambazo hutumika kutibu ugonjwa huu ni pamoja na donepezil hydrochloride (Aricept), rivastigmine (Exelon), galantamine (Razadyne – ambayo inajulikana pia kama Reminyl), tacrine (Cognex) pamoja na Memantine (Namenda). Wagonjwa wanaoonesha pia dalili ya kuwa na matatizo ya akili hupewa dawa za kutibu au kutuliza matatizo hayo.

Aidha familia pia ina jukumu la kumsaidia mgonjwa ili aweze kupata nafuu. Baadhi ya mambo amabyo familia inaweza kufanya ni pamoja na kumsaidia kutembea, kushirikisha katika mikusanyiko ya kijamii ili mgonjwa asijihisi kutengwa. Matendo kama kumpa mazoezi madogo madogo ya kumsaidia kurejesha kumbukumbu yake yanaweza pia kusaidia. Kwa wagonjwa ambao wamefikia hatua ya kushindwa kula wenyewe, jamii haina budi kuwasaidia kula ili wasipate utapiamlo.

Imesomwa mara 5478 Imehaririwa Ijumaa, 05 Mai 2017 14:46
Dr Fabian P. Mghanga

Daktari bingwa na Mhadhiri katika kitivo cha Afya Chuo Kikuu Kishiriki cha Askofu Jacob, Songea

Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.