Image

Dalili za ujauzito hutofautiana kati ya mwanamke mmoja  na mwanamke mwingine, ingawa kuchelewa au kukosa hedhi ni dalili moja muhimu sana ya ujauzito.

Ni muhimu kuzitambua na kuzifahamu dalili hizi kwa sababu zinaweza kusaidia kujua kama kweli umeshika ujauzito au la  pamoja na kuweza kutofautisha matatizo mengine yanayoshahabiana kwa dalili na  ujauzito.

Hebu sasa tuangalie dalili na ishara za ujauzito:

  • Kutokwa damu kidogo ukeni wakati kiumbe kikipandikizwa kwenye mfuko wa uzazi, ingawa siyo wanawake wote hupatwa na dalili hii
  • Kukosa hedhi, hii ni moja ya dalili kubwa ya ujauzito
  • Maumivu kwenye matiti na kuvimba matiti (huweza kutokea kati ya wiki ya 1 hadi ya 2)
  • Uchovu, wanawake wengi huhisi uchovu na  na hali ya kutopenda kufanya lolote.
  • Kupoteza ladha au kuhisi ladha ya chuma mdomoni
  • Kuongezeka kwa hisia ya harufu, kipindi cha ujauzito wanawake wengi huongezeka hisia ya harufu
  • Kichefuchefu na kutapika
  • Maumivu ya kichwa
  • Kizunguzungu
  • Kukojoa mara kwa mara (hasa kati ya wiki 6-8)
  • Kubadilika rangi kwa ngozi inayozunguka chuchu kuwa nyeusi
  • Kutamani baadhi ya vyakula na kuchukia vingine
  • Kupanuka kwa mfuko wa uzazi
  • Tumbo kujaa au kuvimbiwa
  • Kununa na kukasirika haraka
  • Kiungulia au kupata choo kigumu
  • Kolostramu kuanza kutoka kwenye matiti 
  • Kuongezeka uzito
  • Kuweza kupapasa mtoto (palpation of the baby)
  • Kulainika na kuvimba kwa shingo ya uzazi (Hegars sign) - kuanzia wiki ya 6
  • Shingo ya uzazi kubadilika rangi kuwa ya samawati kutokana na msongamano wa damu katika mishipa ya vena. Ishara hii hujulikana kama Chadwick's sign

 

Surua ni mojawapo ya magonjwa ya kuambukiza yanayotisha  kwa binadamu. Huu ni  ugonjwa ulio na  kiwango cha juu cha karibu asilimia 100 cha mashambulizi  pindi mtu apatapo vimelea vya ugonjwa huu.
Pamoja na kuwepo chanjo ya ugonjwa huu, bado surua ni miongoni mwa magonjwa yanayosababisha vifo vingi vya watoto walio chini ya umri wa miaka 5 katika baadhi ya maeneo  duniani hasa kwa nchi zinazoendelea. Ugonjwa huu ambao ulitoweka katika baadhi ya nchi, umeanza kuonekana tena hivi karibuni miongoni mwa watu ambao hawakupata chanjo katika nchi za Uingereza na nyingine za Ulaya.
 
Surua husababishwa na nini?
Surua huenezwa na aina ya virusi jamii ya paramyxovirus. Jamii hii ya virusi hupatikana katika mfumo wa njia ya hewa. Hukaa katika kamasi na majimaji yaliyopo katika mfumo wa hewa. Kwa sababu hii basi virusi hawa huenezwa kwa njia ya upumuaji.
Virusi hawa wanaweza kuishi hewani kwa muda wa hadi saa moja baada ya kutolewa kwa kupiga chafya au kukohoa au hata mazungumzo na mgonjwa. Hii ina maana kuwa, ili kuambukizwa surua, si lazima mtu akutane uso kwa uso na mgonjwa.
Baada ya kuingia ndani ya mfumo wa hewa virusi hushambulia seli za utando wa nje wa njia ya hewa (respiratory tract epithelium) na kuingia katika mzunguko wa wa limfu na kufika kwenye tezi zilizo karibu. Katika tezi huzaliana zaidi na kusambaa mwilini.
 
Muonekano wa mgonjwa
Kawaida dalili za mwanzo zinaanza kuonekana baada ya siku 8 ya kupata uambukizi. Mgonjwa huwa na mafua mepesi, homa, kukohoa na macho kuwa mekundu.
Baada ya siku 2-4 tangu kuanza kuonekana kwa dalili za awali, ukichunguza mdomo wa  mtoto, na kama utamchunguza pembeni (ndani ya shavu) utaona vidonda vyeupe kwenye utando mwekundu wa ndani ya mdomo. Vidonda hivi huonekana kama chumvi iliyomwagwa kwenye zulia jekundu. Hali hii huitwaKoplik spots. Hii ni dalili tosha ya kuthibitisha uwepo wa surua.
Lakini vilevile mgonjwa anaweza kuwa na vipele vidogo sana ambavyo inaweza kukuwia vigumu kutambua. Vipele hivi huweza kuonekana vizuri siku mbili baadaye. Kwa kawaida, vipele hivi huanzia usoni au nyuma ya sikio na kushuka chini kabla ya kutapakaa mwili mzima siku zinazofuata. Vipele huongezeka na kuwa vingi kadiri siku zinavyopita. Kawaida hali hii ya vipele inaweza kuchukua kati ya wiki 1-2. Vipele hupotea baada ya siku 7 na kuacha ngozi iliyobabuka. Hata hivyo, kukohoa kunaweza kuendelea zaidi ya siku 10.
 
Athari za Surua ni zipi?
Ingawa baadhi ya wagonjwa hupona katika kipindi cha siku 10 mpaka 14, baadhi hupata matatizo zaidi yanayoweza kuwa ya muda mrefu kama;
•Maambukizi njia ya masikio (Otitis media)
•Maambukizi njia ya chini ya mfumo wa hewa kama vile
  1. Uambukizi kwenye mirija ya hewa ya koo (bronchitis) maambukizi kwenye njia ya sauti (laryngitis) na croup. Surua inaweza kusababisha kuvimba katika sehemu ya sauti na kuathiri uwezo wa kutoa sauti lakini vilevile inaweza kusababisha uvimbe  katika kuta za utando wa njia ya hewa.
  2. Homa ya mapafu (pneumonia) ambayo ni sababu kuu inayosababisha vifo vinavyotokana na surua. Mgonjwa wa surua ni rahisi kupata homa ya mapafu kwa sababu kinga ya mwili wake huwa imepungua. Homa hii ya mapafu yaweza kusababishwa na aina nyingine ya virusi kama adenovirus, herpes simplex au bakteria kama Staphylococcus aureus, Streptococcus pneumonia, Haemophillus influenza, Klebsiella pneumonia. Lakini vilevile Kifua kikuu kinaweza kutokea kwa kusababishwa na upungufu huu wa kinga mwilini.
•Surua pia inahusishwa na aina mbalimbali ya mashambulizi kwenye ubongo kama vile
  1. Acute encephalitis ambayo hutokea wakati au ndani ya wiki chache baada ya maambukizi.
  2. Progressive encephalitis ambayo hutokea kwa wagonjwa walio na upungufu wa kinga mwilini unaotokana na sababu yeyote ile ikiwemo wale anaopata tiba ya kemikali (Chemotherapy) au kwa sababu ya VVU. Hali hii hutokea  miezi 6 baada ya maambukizi, na inaweza kusababisha mgonjwa kufa.
  3. Subacute sclerosing panencephalitis (SSPE) ni nadra sana kutokea. Mara nyingi kama likitokea, basi humpata mgonjwa baada ya mwaka mmoja wa ugonjwa wa surua. Sifa mojawapo ya hili tatizo ni kupungukiwa kwa uwezo wa kufikiri na akili kuzorota na hatimaye mgonjwa kufariki dunia.
•Surua inaweza kusababisha utapiamlo kwa sababu ya ukali wake hasa kwa watoto ambao hawapati lishe nzuri. Inahusishwa pia na kuharisha na kutapika na kusababisha upungufu wa maji mwilini.
•Surua husababisha upungufu wa Vitamini A na kusababisha tatizo la kutoona vizuri ambalo hijulikana pia kama Keratitis. Kwa mtoto ambaye ana upungufu wa Vitamini A tatizo la macho huwa kubwa zaidi na kwa kitaalamu hujulikana kama Keratomalaciaambapo sehemu nyeupe ya jicho hutoboka.
•Maambukizi katika misuli ya moyo  (Myocarditis)
•Upungufu wa chembe sahani kwenye damu (Thrombocytopenia)
 
Utambuzi wa surua
Utambuzi wa surua inajumuisha historia ya mgonjwa kuwa na homa kwa angalau siku 3 na kuwepo kwa mojawapo ya dalili za mwanzo za surua ambazo ni kukohoa, kuwa na mafua mepesi, macho kuwa mekundu na upele mwilini. Aidha ikithibitika mgonjwa ana Koplik spotsbaada ya uchunguzi ndani ya mdomo ni utambuzi tosha wa surua.
Vilevile vipimo vya kimaabara ni pamoja na uthibitisho chanya wa antibodi dhidi ya surua(measles IgM antibodies) na uwezekano wa kuwapata virus wa surua kutoka katika mfumo wa hewa, damu au mkojo wa mgonjwa (isolation of measles virus RNA) au kwa njia ya kuoteshwa maabara (culture).
 
                                                                        Matibabu
Hakuna tiba maalum kwa ajili ya surua. Lengo kubwa la matibabu ya surua ni kuhakikisha mgonjwa anapata mapumziko, maji ya kutosha, oksijeni na faraja. Mgonjwa anaweza kupewa dawa za kutuliza homa kama vile paracetamol. Imeonekana kuwa matumizi ya dawa ya virusi wa surua (antivirus) hayana msaada wowote katika kutibu surua.
Aidha dawa kwa ajili ya kuzuia magonjwa yanayosababishwa na bakteria (Prophylactic antimicrobial therapy) isipokuwa tu iwapo itathibitika kuwepo kwa maambukizi ya bakteria. Inasisitizwa sana mgonjwa apatiwe Vitamini A. Vitamini A hupunguza hatari ya kifo na madhara ya surua.
Kwa vile ugonjwa wa surua unaenea kwa njia ya hewa ni vizuri mgonjwa akatengwa na watoto wengine. Muhimu ni kutafuta ushauri wa daktari haraka pale unapoona mtoto ana dalili za surua.
 
Kinga
Surua huzuiwa kwa urahisi kwa njia ya chanjo. Watoto ambao hawajapata chanjo ya surua wapo katika hatari kubwa sana ya kupata surua.
 
Kumbuka
Surua ni ugonjwa hatari. Unaweza kuua au kusababisha madhara ya muda mrefu lakini chanjo dhidi yake inazuia hatari hiyo.  Kwa hiyo pale unapohisi mtoto wako  ana dalili za surua  mpeleke haraka hospitali ili kujithibitisha na kupata matibabu yanayofaa.

Tatizo la mimba kutoka au kutolewa ni jambo ambalo limewakumba kina mama wengi walio katika umri wa kuzaa. Aidha mijadala kuhusu kuhalalishwa au kuendelea kuharamishwa kwa utoaji mimba ni jambo linalochukua nafasi ya mazungumzo ya kila siku katika maisha yetu. 

Kwa baadhi ya nchi, suala la utoaji mimba ni jambo lililohalallshwa kisheria ingawa kwa nchi kama Tanzania, suala hili halijahalalishwa isipokuwa tu pale panapokuwa na sababu za kitabibu zinazolazimisha kufanya hivyo.

Nini maana ya mimba kutoka (abortion)

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), utokaji mimba (abortion) hutokea pale ambapo kiumbe (mimba) kilicho chini ya wiki 22 kinapotoka kwa sababu moja ama nyingine, au kinapotolewa kwa njia yeyote ile. Aidha shirika la Afya limekwenda mbali zaidi na kutoa maana nyingine ya utokaji mimba kuwa ni pale mtoto (kiumbe) anapozaliwa akiwa na uzito wa chini ya gram 500.

Aidha baadhi ya matabibu hupendelea kutumia neno ‘abortion‘ kumaanisha kitendo cha utoaji wa mimba kinachofanywa na mtu mwingine ama kwa njia sahihi au zisizo sahihi na ‘miscarriage‘ kumaanisha kitendo cha mimba kutoka yenyewe kwa sababu nyingine yeyote. Ukiacha tofauti hizi za jinsi ya kuharibika kwa mimba, abortion na miscarriage humanisha kitu kilekile cha mimba kutoka.

Aina za utokaji mimba (Classification of abortion)

Utokaji mimba umeanishwa katika aina zifuatazo

  1. Utokaji wa mimba wa hiyari yaani kitendo cha mimba kutoka yenyewe (spontaneous abortion)
  2. Mimba inayotishia kutoka ingawa bado haijatoka (threatened abortion)
  3. Utokaji wa mimba usioepukika (inevitable abortion)
  4. Utokaji wa mimba ulio kamili (complete abortion)
  5. Utokaji wa mimba usio kamili (incomplete abortion)
  6. Mimba iliyotoka bila kugundulika kuwa imetoka (missed abortion)
  7. Utokaji wa mimba unaojirudia rudia (recurrent abortion)
  8. Utoaji mimba kinyume cha sheria (illegal abortion)
  9. Utoaji mimba kwa sababu za kiafya (therapeutic abortion)

1. Utokaji mimba kwa hiari au kitendo cha mimba kutoka yenyewe (spontaneous abortion)

Hii ni hali inayotokea pale mimba inapoharibika na kutoka bila kuwepo kwa sababu yeyote iliyo dhahiri, kwa maana nyingine mimba uharibika na kujitokea bila kusababishwa na mtu wala kitu chochote. Utokaji mimba wa namna hii umegawanyika katika aina kuu nne ambazo ni

  • Mimba inayotishia kutoka ingawa bado haijatoka (threatened abortion)
  • Mimba isiyoepukika kutoka (Inevitable abortion)
  • Mimba inayotoka yote au kamili (complete abortion), na
  • Utokaji mimba usio kamili (Incomplete abortion)


i. Mimba inayotishia kutoka (threatened Abortion)

Tatizo hili hutokea mapema wakati wa ujauzito. Hali hii hujionesha kwa damu kutoka ukeni wakati njia ya shingo ya uzazi ikiwa bado imefunga. Mara nyingi mimba inayotishia kutoka haina tabia ya kuambatana na maumivu yeyote ya tumbo.

Daktari anapompima mgonjwa hukuta shingo ya kizazi ikiwa imefunga na hakuna dalili zozote za kiumbe kutoka ingawa mgonjwa hutokwa na damu sehemu za siri. Aidha mgonjwa huwa hana maumivu yeyote ya tumbo.

ii. Mimba isiyoepukika kutoka (inevitable abortion)

Hii ni hali inayotokea mapema wakati wa ujauzito pale damu inapotoka ukeni wakati njia ya shingo ya kizazi ikiwa imefunguka au kuwa wazi. Aidha, kwa kawaida, kiasi cha damu kinachotoka ni kingi na mgonjwa hujisikia maumivu makali sana ya tumbo.

Utokaji mimba usioepukika waweza kupelekea

  • Utokaji mimba ulio kamili (complete abortion), au
  • Utokaji mimba usio kamili (incomplete abortion).

iii. Utokaji mimba usio kamili (incomplete abortion)

Utokaji mimba usio kamili huambatana na utokaji damu kwa wingi sehemu za siri za mgonjwa, kufunguka kwa njia ya shingo ya kizazi, kutoka kwa baadhi ya mabaki ya kiumbe (products of conception) ingawa mengine hubakia, na mgonjwa kujisikia maumivu makali ya tumbo hususani sehemu za chini ya kitovu.

iv. Utokaji wa mimba ulio kamili (complete abortion)

Hali hii huambatana na mama kutokwa damu sehemu za siri, kujisikia maumivu makali ya tumbo pamoja na kutoka kwa kiumbe ikiambatana na kondo lake la nyuma. Aidha baada ya muda, mgonjwa hueleza kupotea kwa maumivu ya tumbo, damu kupungua kutoka sehemu za siri na kufunga kwa njia ya njia ya shingo ya kizazi (cervix).

v. Mimba iliyotoka bila kugundulika kuwa imetoka (missed abortion)

Hali hii hutokea pale ambapo, kiumbe kinapokuwa kimekufa bila ya mimba kutoka. Mara nyingi, damu huwa haitoki sehemu za siri, na mgonjwa huwa hajisikii maumivu yeyote ya tumbo. Aidha huwa hakuna dalili zozote za ukuaji wa mimba na hata mapigo ya moyo ya mtoto hayawezi kutambulika hata kama vipimo maalum vitatumika.

vi. Utokaji wa mimba unaojirudia rudia (recurrent abortion)

Hali hii hutokea pale ambapo mama huwa na historia ya mimba kutoka mara tatu au zaidi kwa mfululizo.

vii. Utoaji mimba kinyume cha sheria (illegal abortion)

Utoaji mimba kinyume cha sheria ni usitishwaji wa maisha ya mimba au kutolewa kwa kiumbe kinyume na sheria za nchi husika zinavyoagiza. Katika mazingira kama haya, sababu dhahiri za kitaalamu hukosekana isipokuwa wahusika hutenda kulingana na sababu zao binafsi zikiwemo za kutoitaka mimba au kama ni muhusika ni mwanafunzi huogopa kufukuzwa shule.

viii. Utoaji mimba kisheria kwa sababu za kitabibu (therapeutic abortion)

Utoaji mimba ulioidhinishwa kitabibu ni usitishwaji wa mimba kwa ajili ya kuokoa maisha ya mama. Usitishwaji huu ni hufanywa kitaalamu na daktari. Sababu zinazoweza kufanya mimba ikasitishwa ni pamoja na

  • iwapo kiumbe kina mapungufu mengi ya kimaumbile (fetal anomally) ambayo yatamletea mtoto atakayezaliwa matatizo na hata kusababisha kifo chake
  • iwapo mama mjamzito alipata ujauzito kwa kubakwa na asingependa kuzaa, au
  • iwapo mama mjamzito ana kansa , kwa mfano, kansa ya kiwanda cha mayai ya kike (ovarian cancer), kansa ya damu (leukemia) au kansa ya tezi la goita (thyroid cancer)

Mambo gani hufanya mimba kutoka kwa hiyari?

Kuna sababu kadhaa zinazoweza kupelekea mimba kutoka kwa hiyari (spontaneous abortion). Miongoni mwa sababu hizo ni

  • Matatizo kwenye mfumo wa jenetiki (genetic abnormalities) ambayo husababisha kuharibika na kutoka kwa mimba katika miezi mitatu ya mwanzoni.
  • Matatizo kwenye mfuko wa uzazi (uterine problems): matatizo kama vile kuwepo kwa uvimbe kwenye mfuko wa uzazi wa mwanamke (uterine fibroids), au kulegea kwa milango ya shingo ya kizazi (cervical incompetence) husababisha mimba kutoka katika theluthi ya pili ya ujauzito (second trimester).
  • Sababu nyingine ni pamoja na maradhi wakati wa ujauzito kama malaria, kisukari, shinikizo la damu, kifafa cha mimba, matatizo kwenye tezi ya ‘goita’ (hypothyroidism). Aidha maambukizi kama Rubella, toxoplasmosis na mengineyo nayo pia huweza kusababisha mimba kutoka.
  • Kukosekana kwa ulinganifu katika baadhi ya homoni mwilini (hormonal imbalance)
  • Matumizi ya baadhi madawa kwa mfano zinazotumika katika kutibu msongo wa mawazo kama vile paroxetine au venlafaxine nayo yaweza kusababisha utokaji wa mimba.

Tabia hatarishi zinazoweza kusababisha utokaji wa mimba

  • Unywaji pombe uliopitiliza.
  • Uvutaji sigara
  • Utumiaji madawa ya kulevya kama vile kokeini (cocaine)
  • Utumiaji kwa wingi wa vinywaji vyenye kiasili cha caffeine kama vile kahawa au kakao.

Vipimo na Uchunguzi

Ili kutambua kuwepo kwa hali hii ya mimba kutoka, vipimo vifuatavyo vyaweza kufanywa na tabibu

  • Kipimo cha mimba kwa kutumia mkojo (Urine for hCG)
  • Kupima damu ili kufahamu kiasi cha wingi wa damu (haemoglobin level), kundi la damu (blood group) na muda wa damu kuganda (bleeding and clotting time).
  • Kuchunguza iwapo shingo ya uzazi imefunga au ipo wazi, na pia kuchunguza iwapo kuna dalili ya kiumbe kutoka ama la. Uchunguzi huu huitwa speculum examination.
  • Ultrasound ya nyonga (pelvic utrasound) kwa ajili ya kutambua iwapo kiumbe kipo ama la, na kama kipo je ki hai ama kimekufa.
  • Aidha ni muhimu pia kufanya uchunguzi wa magonjwa mbali ya zinaa ambayo husababisha mimba kutoka.

Matibabu ya utokaji wa mimba

Matibabu ya utokaji wa mimba hutegea sana aina ya utokaji wa mimba. Hata hivyo, ni muhimu kuzingatia vitu vifuatavyo wakati wa kutoa matibabu kwa mtu aliyepoteza mimba
Wahudumu wa afya huzingatia kanuni zote (ABC) za kuokoa maisha ya mgonjwa kama vile

  • kuhakikisha njia ya hewa ya mgonjwa ipo wazi na hewa inaingia na kutoka vizuri kwenye mapafu
  • kuhakikisha mgonjwa anapumua vizuri bila shida
  • kuhakikisha mishipa ya damu ya mgonjwa imewekwa mrija wa veni (intravenous line) na mgonjwa anapewa dripu ya maji ya normal saline.
  • kuhakikisha mgonjwa anaongezwa damu haraka iwapo vipimo vitaonesha kuwa alipoteza damu kwa wingi

Matibabu ya mimba inayotishia kutoka (threatened abortion)

Kwenye hali hii, mgonjwa hutakiwa

  • kupumzika kitandani bila kufanya kazi yeyote (complete bed rest) angalau kwa wiki moja au zaidi mpaka hapo damu itakapoacha kabisa kutoka
  • kumpa ushauri na uhakika mama ili kumfanya atulie kiakili (assurance and proper councelling)
  • Mama pia hupewa dawa za kumtuliza na kumfanya apumzike (sedatives) kama vile phernobabitone
  • Aidha mama hupewa dawa kwa ajili ya kupunguza kusukuma kwa uterus (antispamodics) kama vile salbutamol
  • Kutofanya tendo la ndoa kwa wiki mbili au tatu
  • Aidha mama na mumewe hupewa ushauri juu ya tatizo hilo na jinsi ya kuendelea na matibabu

Matibabu ya mimba iliyotoka kamili (complete abortion)

Mara nyingi mgonjwa huwa haitaji matibabu zaidi ya uangalizi wa karibu kwa vile kiumbe pamoja na kondo lake la nyuma vyote huwa vimetoka kikamilifu. Mara chache sana, kulingana na jinsi daktari atakavyoona, mgonjwa anaweza kupewa antibiotiki kwa ajili ya kuzuia uwezekano wa kupata maambukizi.

Matibabu ya utokaji wa mimba usiokuwa kamili (incomplete abortion)

Matibabu ya aina hii ya utokaji wa mimba uhitaji mgonjwa kusafishwa kwa ajili ya kuondoa mabaki ya kiumbe (products of conception) yaliyobakia. Usafishaji huu huweza kufanywa kwa kutumia njia inayoitwa Manual Vacuum Aspiration (MVA).

Aidha mgonjwa hupewa dawa za antibiotiki kwa ajili ya kuzuia uwezekano wa maambukizi ya vimelea vya bakteria.

Matibabu mimba iliyotoka bila kugundulika kuwa imetoka (missed abortion)

Matibabu ya aina hii ya utokaji wa mimba ni pamoja na mgonjwa kuwekewa maji ya uchungu ili kiumbe kiweze kutoka. Wakati mwingine, daktari anaweza kuamua kusafisha mfuko wa uzazi (uterus) kwa kutumia njia inayoitwa dilatation and curettage. Sambamba na matibabu hayo, mgonjwa pia hupewa dawa za antibiotiki kwa ajili ya kuzuia maambukizi ya vimelea vya bakteria.

Matibabu ya tatizo la utokaji wa mimba unaojirudia (recurrent abortion)

Jambo la msingi katika matibabu ya tatizo la utokaji mimba unaojirudia (recurrent abortion) ni kugundua na kutambua chanzo kinachosababisha tatizo hilo na kisha kukishughulikia ili kuondoa kabisa kujirudia rudia kwa tatizo hili.

Kwa nini watoto wachanga wanalia?

Ni kawaida kwa watoto kulia. Hata watoto wanaozaliwa na afya njema kabisa wanaweza kulia kwa jumla ya wastani wa kati ya saa moja mpaka matatu kwa siku. Kwa vile watoto hawawezi kujifanyia chochote wao wenyewe zaidi ya kutegemea wazazi, walezi ama watu wengine wanaowazunguka katika kuwapatia chakula, joto, na faraja, kilio ni njia ya mtoto ya kuwasilisha moja ya mahitaji hayo.

Kama mzazi mpya, wakati mwingine inakuwa vigumu kutambua mtoto wako anahitaji nini anapolia. Mzazi anaweza kuwa na maswali kadhaa kichwani mwake, je, mtoto ana njaa, anasikia baridi, ana kiu, anaumwa ama amechoka? Katika siku za mwanzo, hali ya namna hii inawawia vigumu wazazi wengi, wasijue nini la kufanya. Hata hivyo, kwa kadiri siku zinavyopita mzazi mpya ataweza kutambua kuwa kilio cha mtoto wake kinamaanisha anahitaji nini kutokana na mfumo wake wa kulia.

Ukurasa 5 ya 5