Haya ni matibabu ambayo hutolewa kwa jino ambalo sehemu ya uhai wake imeharibika kiasi kwamba haliwezi kutibika kwa kuziba tu, kwa maneno mengine hii ndiyo njia mbadala ya kutibu jino bila kung’oa.
Matibabu uhusisha kutoboa jino hadi sehemu ya uhai wa jino yenye mishipa ya damu na ile ya fahamu na chembechembe za meno na kuviondoa nikimaanisha kuondoa mishipa ya fahamu, ya damu na chembe pamoja na ugonjwa na baadae kuijaza sehemu hii na vitu maalumu vinavyokubaliana na mwili (biocompatible).
Aina za matibabu ya mzizi wa jino
Kuna aina kuu mbili za matibabu ya mzizi wa jino
Njia ya kawaida (conventional root canal treatment)
Njia hii ni kama nilivyoeleza hapo juu, kuingia kwenye kiini cha jino na kuondoa kila kitu kilichomo na kisha kujaza uwazi uliobaki na vitu maalumu vinavyokubaliana na mwili
Matibabu ya mzizi wa jino yanayohusisha upasuaji
kwa njia hii mbali na kutumia njia ya kwanza, upasuaji hufanyika pia ili kondoa mfupa uliofunika ncha ya mzizi wa jino kusafisha eneo lililozunguka ncha ya mzizi na baadaye kukata ncha husika kisha kuziba kutokea kwa nyuma (retro grade filling).
Njia hii hutumika pale njia ya kawaida inaposhindwa kuondoa tatizo au inapoonekana kabisa kuwa haitaweza kuondoa tatizo. Huu ni upasuaji mdogo, unaofanyika kwa ganzi ndogo ya eneo husika (local anaesthesia). Mafanikio ya matibabu haya ni makubwa sana.
Ni meno yapi yanahitaji matibabu hayo?
• Meno yaliyooza hadi uoza kufikia kiini cha jino (dental pulp) - sehemu ya uhai wa jino.
• Meno yaliyopata ajali na kupasuka na kuacha kiini cha jino kikiwa wazi (traumatic pulp exposure)
• Meno yaliyopata ajali na kusababisha mishipa ya damu kukatika au kupasuka na kuvunjika ndani ya jino, kitu ambacho hupelekea jino kufa (pulp necrosis) na baadaye kusabisha jipu au kubadilika rangi
• Wakati mwingine japo ni mara chache, ni pale tunapokuwa tunataka kuliweka sawa jino/meno ambalo/ambayo hayapo kwenye mstari sawa ili yaendane na meno mengine.
• Pia wakati mwingine, tunapo lisaga jino ili liweze kubeba meno bandia ya daraja (bridge) huku tukiwa na mashaka na uhai wake.
Nini dalili zinazoashiria jino kuhitaji matibabu haya?
• Jino linalouma - kuuma kwa jino kunashiria ugonjwa kuwa umeingia ndani ya kiini cha jino na au hata kupitiliza na kuingia kwenye mfupa ulioshikilia jino
• Jino lililooza na kusababisha uvimbe, liwe linauma au haliumi
• Jino lililokatika na kupoteza zaidi ya nusu ya kichwa cha jino (crown) kukatika kuwe kwa ajali au kuoza au vyote kwa pamoja
• Jino linalobadilika rangi huku kukiwa na historia ya kuligonga mahali au kuchapwa ngumi usoni, hapa jino linaweza kuanza kubadilika rangi miezi sita tangu siku ya ajali mpaka wakati mwingine hadi miaka ishirini wakati mgonjwa alishasahau hata ajali yenyewe.
Malaria ni ugonjwa unaoathiri watu wengi sana duniani. Malaria husababisha vifo vya watu milioni 2.7 duniani kote, ambapo vifo vingi hutokea barani Afrika. Ugonjwa wa malaria huonekana katika nchi 100 duniani kote.
Kwa Tanzania, mikoa ambayo inaongoza kwa maambukizi ya malaria ni Kagera (41.1%), Lindi (35.5%), Mtwara (36.6%), Mwanza (31.4%), Mara (30.3%). Mikoa ambayo maambukizi ya malaria ni kidogo ni Manyara (1%), Kilimanjaro (1%) na Dar-es-salaam (1.2%). Kwa Zanzibar, maambukizi ya malaria ni kwa asilimia 0.8.
Malaria huonekana sana katika kanda ya Tropiki.Ugonjwa huu wa malaria uligunduliwa mwaka 1880 na Charles Louis Alphonse Laveran, katika hospitali ya jeshi ya Constatine, Algeria, baada ya kuona vimelea vya plasmodium, kutoka kwa mgonjwa aliyefariki kwa ugonjwa huo.
Malaria ni kati ya magonjwa ya maambukizi ambao husababishwa na vimelea vya Plasmodium, ambavyo humfikia binadamu kupitia kung’atwa na mmbu aina ya Anopheles jike.
Kuna aina 5 za vimelea viletavyo malaria:
- Plasmodium falciparum - Hupatikana sana katika nchi zilizopo katika jangwa la sahara. Asilimia 75 ya wagonjwa wote wa malaria barani Afrika husababishwa na vimelea hivi. Mwaka 2006, kati ya watu milioni 247 duniani waliougua malaria, asilimia 91 walisababishwa na vimelea hivi (Afrika 98%) na kusababisha vifo kwa asilimia 90 mwaka huo huo barani Afrika.
- Plasmodium malariae - Pia hupatikana katika nchi zilizopo katika jangwa la sahara, Asia ya Mashariki, Indonesia na katika visiwa vya magharibi mwa Pacific. Kati vya vimelea vyote vya malaria, plasmodium malariae ndio huonekana kwa uchache zaidi.
- Plasmodium ovale - Hupatikana Afrika Magharibi, Ufilipino, Mashariki mwa Indonesia, Papua New Guinea, Cambodia, Bangladesh, India, Thailand na Vietnam.
- Plasmodium vivax - Huonekana katika bara la Marekani, Latin Amerika na baadhi ya sehemu za bara la Afrika.
- Plasmodium knowlesi - Hupatikana katika bara la Asia ya mashariki katika nchi za Bormeo, Myanmar, Malaysia, Ufilipino, Singapore na Thailand. Haipatikani katika bara la Afrika.
Mzunguko wa maisha ya vimelea vya malaria
Mwenyeji wa msingi ya vimelea vya malaria ni mbu aina ya anopheles wa kike, ambae pia ni msambazaji, na binadamu ni mwenyeji wa kati. Mbu anapokuwa anajipatia chakula kwa kunywa damu kwa kuuma binadamu mwenye maambukizi ya vimelea vya malaria, ndio mzunguko wa kwanza huanza, ambapo gametocyte za vimelea vya plasmodium hugawanyika ndani ya mbu na kutengeneza gametocyte za kike na za kiume na baada ya hapo gametocyte hizo za kike na za kiume, hujiunga ndani ya mfumo wa chakula wa mbu na kutengeneza Ookinete ambayo hupenyeza kwenye kuta za mfumo wa chakula na kutengeneza Oocyst nje ya ukuta wa mfumo wa chakula, na hapo hupasuka na kutengeneza Sporozoites na kuhamia kwenye tezi za mate za mbu, na kuwa tayari kuambukiza binadamu mwengine pindi mbu anapojitafutia chakula.
Kwa mbu jike damu ndio lishe yake wakati dume lishe yake ni nekta ya mimea, hivyo mbu dume hasambazi ugonjwa huu. Na mbu jike aina ya anopheles hupenda kujipatia lishe kipindi cha usiku.
Maambukizi ya malaria yanaweza kupatikana kwa kuongezewa damu ingawa ni nadra sana.
Ni pale ambapo kunakuwa na mkusanyiko wa maji kati ya kuta mbili zinazozunguka mapafu. Kujaa huku kwa maji husababisha mgonjwa kupata shida ya kupumua vizuri.
Je mapafu kujaa maji husababishwa na nini?
Sababu za Mapafu kujaa maji zinaweza kuelezewa kutokana na aina ya maji yaliyojaa:
- Transudate – hapa maji huliki kutoka kwenye mishipa ya damu na kuingia kwenye mapafu mfano kwenye magonjwa yafuatayo:
- Moyo kushindwa kufanya kazi kwa ufanisi (congestive cardiac failure)
- Ini kushindwa kufanya kazi kwa ufanisi (liver failure)
- Figo kushindwa kufanya kazi kwa ufanisi (renal failure)
- Exudate – hapa maji hujaa kutokana na kuta zinazonguka mapafu kitaalamu pleura zinapovimba au kutokana na magonjwa ya mapafu mfano:
- Kansa ya pafu au ya titi
- Lymphoma
- Kifua kikuu
- Vichomi
- SLE
- Figo kushindwa kufanya kazi kwa ufanisi
- Asbestosis
- Majipu ndani tumbo
Hutokea pale vimelea (bakteria) wanapovamia kuta za ndani za moyo (endocardium), zikiwepo valve na kusababisha maambukizi.
Hakuna mishipa ya damu ambayo ni mahususi kwa ajili ya kupeleka damu safi moja kwa moja kwenye valve za moyo, hivyo chembe chembe nyeupe za damu (ambazo ni mahususi kwa ajili ya kinga ya maambukizi) hufika kwa shida sana kwenye valve za moyo. Hali hii husababisha chembe chembe nyeupe kuwa butu pale vimelea (bakteria) wanapotengeneza uoto (vegetations) kwenye valve za moyo. Na kwa sababu ya hakuna mishipa ya damu ambayo ni mahususi kwa ajili ya kupeleka damu moja kwa moja kwenye valve za moyo, matibabu yake husumbua sana kwakuwa ni vigumu dawa kufika kwenye eneo husika.
Maambukizi katika kuta za ndani za moyo yamegawanyika katika sehemu kuu mbili kutokana na jinsi ugonjwa ulivyo-anza (onset):
Maambukizi ya kuta za ndani za moyo ya papo kwa hapo kitaalamu acute bacteria endocarditis
huanza kati ya siku kadhaa hadi wiki kadhaa, na mgonjwa huwa maututi; na maambukizi katika kuta za ndani za moyo ndogo ya papo kwa hapo kitaalamu sub acute bacteria endocarditis- huanza kati ya wiki kadhaa hadi miezi kadhaa, na dalili hutokea pole pole
Na vile vile maambukizi haya yanaweza kugawanywa kama ifuatavyo
- Maambukizi katika kuta za ndani za moyo ya Valve asili au kitaalamu native valve endocarditis
- Maambukizi katika kuta za ndani za moyo ya Valve za bandia au kitaalamu prosthetic valve endocarditis
- Maambukizi katika kuta za ndani za moyo kutokana na matumizi ya madawa ya kulevya kwa njia ya mshipa kitaalamu intravenous drug abuse endocarditis
Maambukizi ya tezi dume bila uwepo wa bakteria (Chronic non-bacterial prostatitis)
Kama jina lake linavyoeleza, maambukizi ya aina hii kwenye tezi dume husababishwa na msongo wa mawazo, matatizo katika vichocheo vya mwili (homoni) na hata matatizo katika mfumo mzima wa neva.Pia kumekuwepo na dhana ya kwamba maambukizi ya aina hii huchangiwa na kuwepo kwa maumivu ya kibofu cha mkojo yanayotokana na maambukizi katika kibofu hicho (Cystitis) au hali ya hewa hususan baridi ambayo huongeza maumivu ya tezi dume na hali ya joto ambayo hupunguza maumivu hayo. Baridi pia huchangia kujirudia kwa dalili na viashria vya maambukizi haya. Katika utafiti uliofanyika kaskazini mwa nchi ya Finland (nchi ambayo ina majira ya baridi kali sana),umeonyesha ya kuwepo kwa maambukizi ya aina hii yanayoambatana na dalili na viashiria vyake kali sana kuliko sehemu yoyote duniani.
Maambukizi haya ya tezi dume bila uwepo wa bakteria hutokea kwa wanaume walio katika umri wa miaka 35-45 na inakisiwa kutokea kwa asilimia 90-95 ya maambukizi yote ya tezi dume .
Dengue ni ugonjwa unaosababishwa na virusi viitavyo Dengue vinavyosambazwa na mbu aina ya Aedes . Mbu huyu anayeambukiza homa ya dengue hupendelea kuishi karibu na makazi ya watu na huweza kuuma binadamu mchana na usiku. Ugonjwa huu huathiri sana nchi za tropiko kama Amerika ya kusini na Africa. Ni moja kati ya homa kali inayodhoofisha na kuambatana na maumivu makali. Kwa sasa, hakuna kinga ya homa ya dengue, njia pekee ya kuepuka ugonjwa huu ni kuzuia kuumwa na mbu anayesambaza homa ya dengue.
Je ni wapi homa hii upatikana zaidi duniani?
•India
•China
•Visiwa vya pasifiki
•Mexico
•Afrika
Dalili za homa ya dengue
•Homa kali ya ghafla
•Maumivu makali ya kichwa
•Macho kuuma
•Maumivu ya viungo
•Kichefuchefu
•Kutapika
•Vipele ambavyo hutokea siku nne baada ya homa kuanza
•Kutoka damu puani, kwenye fizi na kuchubuka kirahisi
Mara nyingi dalili huwa sio kali na wengi hudhania ni homa ya mafua au maambikizi mengine ya virusi. Dalili hizi huanza kutokea baada ya wiki mbili, lakini kwa wengi huchukua wiki moja ya kwanza na tayari utaanza kuona dalili za dengue.
Usonji ni tatizo linalojitokeza mapema utotoni, ambapo mtoto huwa na mapungufu kwa kupenda kujitenga na kutotaka kuwa karibu na watu (Impaired social interaction), hupata matatizo ya lugha na shida ya mawasiliano (impaired language and communication skills) na huwa na tabia ya kurudia rudia kitu anachokifanya mara nyingi (restrictive repetitive behaviour).
Mara nyingi wazazi hugundua watoto wao wana tatizo hili katika kipindi cha miaka miwili ya umri wa mtoto.Chanzo halisi cha tatizo hili la usonji hakijulikani ingawa matatizo ya kijenetiki (Neurodevelopmental disorder) ndio uhusishwa na tatizo la usonji.Maaambukizi ya Rubella au matumizi ya pombe na madawa ya kulevya aina ya coccaine wakati wa ujauzito na hata sababu za kimazingira, yote haya uhusishwa na tatizo hili la usonji.
Watoto wa kiume huathirika sana ikilinganishwa na watoto wa kike. Kwa kila watoto watatu wa kiume wenye kupata usonji ni mtoto mmoja tu wa kike anaepata usonji.
Jarida la The Lancent la mwaka 2013, linasema watu wapatao milioni 21.7 wameathirika kwa tatizo hili la usonji ulimwenguni kote 1. Tabia za kujirudia rudia kwa mtoto aliyeathirika na tatizo la usonji zimegawanyika katika makundi yafuatayo;
- Tabia zilizozoeleka - Kama kupiga piga mikono, kutikisa tikisa kichwa mara kwa mara na kujibiringisha mwili
- Tabia ambazo huchukua sana muda kama za kupanga panga vitu kwa mpangilio maalum au kuosha mikono mara kwa mara
- Tabia ya kung’ang’ania vitu visihamishwe kwa mfano viti au kutokubali kukatizwa katizwa
Ugunduzi (Diagnosis)
Ugunduzi wa tatizo hili la usonji hufanyika kwa
- Daktari wa watoto (Pediatrician) kumpima vipimo vya kawaida pamoja na kuchukua historia ya ukuaji wa mtoto husika (Developmental milestones)
- Daktari bingwa wa watoto aliyebobea kwenye matatizo ya kisaikolojia ya watoto (Pediatric neuropsychologists) kumpima ili kuangalia tabia za mtoto huyu na uwezo wake wa kiakili (Cognitive skills)
- Vipimo vya kijenitikia (genetics testing) kama high-resolution chromosome and fragile X testing. Hufanyika baada ya kugundulika kwamba chanzo cha tatizo la usonji ni matatizo ya kijenetiki
Kadri mtoto anavyoendelea kukuwa ndio usonji unavyoweza kutambulika kwa urahisi zaidi kwani madhara yake yanaonekana kwa urahisi wakati wa ukuaji wa kiakili wa mtoto.
Uchunguzi
Mchunguze mtoto wako kwa viashiria vya tatizo la usonji mapema zaidi kwani kumchelewesha mtoto mwenye usonji kupimwa na kupewa tiba mapema huchangia tatizo hili kuwa kubwa zaidi na hivyo kuathiri matokeo ya matibabu ya tatizo hili. Nusu ya wazazi hugundua watoto wao wana tabia zisizo za kawaida ndani ya miezi 18 ya umri wa mtoto, na moja ya tano ya wazazi hugundua ya kwamba watoto wao wana tabia zisizo za kawaida ndani ya kipindi cha miezi 24 ya umri wa mtoto 2.Tabia hizi ambazo si za kawaida katika ukuaji wa mtoto ni;
- Kutotamka maneno ya kitoto (no babbling) mpaka anapotimiza umri wa mwaka mmoja
- Kushindwa kuotesha kidole au kumpungia (waving, gesturing etc) mzazi/mtu yoyote mkono mpaka anapotimiza umri wa miezi 12
- Kushindwa kutamka neno lolote mpaka anapotimiza umri wa miezi 16
- Kutotamka maneno mawili kwa pamoja au sentensi mpaka umri wa miezi 24
- Kupoteza uwezo wa kuongea au kutokuwa na tabia ya kutangamana/kuchanganyikana na watu wengine wakati wowote ule katika umri wa mtoto
Matibabu
Familia yenye mtoto mwenye tatizo la usonji huhitaji kuelemishwa jinsi ya kuishi na mtoto huyo pamoja na kusaidiwa katika malezi yake. Kwa kuwa tatizo hili halitibiki ni muhimu mtoto kupata:
- Tiba ya Tabia
- Uchambuzi wa tabia (ABA): Kutumia utaalamu wa kisaikolojia kufundishia na kuwahusisha na jamii, kuboresha mawasiliano, na usimamizi wa kitabia
- Matibabu na elimu ya usonji kwa kuboresha mawasiliano kwa watoto wenye ulemavu (TEACCH)
- Tiba nyingine muhimu ni kuelimisha jamii kuhusu watoto wenye usonji , jinsi ya kuishi nao na kuwaanzishia watoto wenye usonji matibabu mapema.
Marejeo
- Global Burden of Disease Study 2013 Collaborators (2015)."Global, regional, and national incidence, prevalence, and years lived with disability for 301 acute and chronic diseases and injuries in 188 countries, 1990–2013: a systematic analysis for the Global Burden of Disease Study 2013.". Lancet. 386: 743–800. doi:1016/S0140-6736(15)60692-4. PMC 4561509. PMID 26063472.
- Landa RJ (2008). "Diagnosis of autism spectrum disorders in the first 3 years of life". Nat Clin Pract Neurol. 4 (3): 138–47. doi:10.1038/ncpneuro0731. PMID 18253102
Goita (Goiter) ni hali ya kuvimba kwa tezi ya thyroid. Uvimbe huu hautokani na saratani na kwamba goita si saratani. Tezi ya thyroid ipo sehemu ya mbele ya shingo. Kazi kuu za tezi ya thyroid ni kuzalisha homoni mbalimbali ambazo husaidia mwili kuthibiti na kufanya kazi zake mbalimbali.
Aina za goita na visababishi vyake
Kuna aina kadhaa za goita. Goita ya kawaida (simple goiter) inaweza kutokea bila kuwepo kwa chanzo chochote cha kueleweka. Wakati mwingine, yaweza kutokea wakati tezi ya thyroid inaposhindwa kuzalisha homoni/vichocheo vya kutosha vya thyroid kwa ajili ya mahitaji ya mwili. Ili kuweza kuendana na hali hii, tezi ya thyroid huongezeka ukubwa ili kufidia upungufu wa homoni za thyroid.
Kuna aina mbili za goita ya kawaida, Goita inayowapata wakazi wa eneo fulani (endemic goiter). Aina hii pia huitwa colloid goiter, na Goita inayotokea maeneo tofauti (sporadic goiter). Aina hii pia hujulikana kama nontoxic goiter.
Endemic goiter au colloid goiter huwapata makundi ya watu wanaoishi maeneo yenye udongo wenye upungufu mkubwa wa madini ya Iodine. Maeneo ya aina hii mara nyingi ni yale yaliyo mbali kutoka pwani ya bahari au yaliyo katika nyanda za juu kutoka usawa wa bahari kama vile mikoa ya Mbeya, Iringa na Rukwa.
Iodine ni madini muhimu yanayohitajika katika utengenezaji wa homoni mbalimbali zinazozalishwa na tezi ya thyroid. Watu wanaoishi kwenye maeneo kama haya wapo katika hatari ya kupata goita kwa vile hawapati madini ya kutosha ya Iodine katika chakula chao.
Matumizi ya chumvi ziliongezwa madini ya Iodine yamesaidia sana kupunguza matatizo ya upungufu wa Iodine miongoni mwa watu wengi nchini Tanzania na duniani kwa ujumla. Hata hivyo, upungufu wa madini ya Iodine bado umeendelea kuzikumba sehemu nyingi za Afrika ya kati, Amerika ya kusini pamoja na Asia ya kati.
Chanzo cha sporadic goiter au nontoxic goiter bado hakifahamiki vema miongoni mwa wagonjwa wengi. Hata hivyo, matumizi ya baadhi ya dawa kama vile lithium pamoja na aminoglutethimide yameelezwa kuwa chanzo kimojawapo cha aina hii ya goita.
Ugonjwa wa vidonda vya tumbo hutokea iwapo kidonda cha ukubwa wa angalau wa nusu sentimita kitatokea kwenye sehemu yeyote ya ukuta wa tumbo au utumbo wa binadamu.
Kwa kawaida tatizo hili huleta maumivu makali sana ya tumbo ingawa si lazima kila maumivu ayapatayo mgonjwa husababishwa na vidonda vya tumbo. Aidha tafiti zinaonyosha takribani asilimia 70 za madoda ya tumbo hazionyeshi dalili yoyote. mara nyingi aina hii ya tukia (presentation) hupelekea madhara makubwa kwa ghufla kama madonda kutoa damu (bleeding) na matumbo kutoboka (perforation)
Tafiti zimeonesha kwamba karibu asilimia 70 mpaka 90 ya vidonda vya tumbo husababishwa na aina ya vimelea vya bakteria wajulikanao kama Helicobacter pylori. Aidha matumizi ya baadhi ya dawa za kutuliza maumivu za jamii ya Non Steroid Anti-inflamatory Drugs kama aspirin au diclofenac huweza kusababisha au kuongeza uwezekano wa kupata ugonjwa huu.
Kuna dhana iliyozoeleka kuwa vidonda vya tumbo huathiri zaidi mfuko wa kuhifadhia chakula yaani tumbo (stomach). Dhana hii si kweli kwani sehemu inayoathiriwa zaidi na tatizo hili ni sehemu ya kwanza ya utumbo mdogo ijulikanayo kama duodenum.
Ugonjwa wa kisukari ni ugonjwa tishio sana hasa kwa wale wanaougua ugonjwa huu kutokana kuwa na athari nyingi sana kama mgonjwa kupata kiharusi, kupoteza viungo mbalimbali vya mwili kama vile kukatwa mguu/miguu, kidole/vidole na hata kupoteza uwezo wa kuona (diabetes retinopathy), na athari hizi hutokea endapo ugonjwa wa kisukari haujadhibitwa vyema.
Ugonjwa huu wa kisukari unaweza usiwe ugonjwa wa kutisha endapo tu mwenye kisukari ataweza kuishi kwa kujiamini na kujikubali, wataalam wanasema kuwa mtu kuishi na ugonjwa huu wa kisukari anahitaji mambo makuu manne :-
Kujikubali
Kujikubali ni jambo muhimu sana, kutayarisha akili yako na kuikubali hali hiyo ya kuwa na ugonjwa wa kisukari,na kuiambia akili yako kuwa ugonjwa huu hauponi ni hali ambayo itakuwepo katika umri wa maisha yako yote na kuwa tayari kubadili mfumo wako mzima wa maisha.Hii ni sawa na mtu aliyezaliwa upya.
Kubadili mfumo wa Ulaji
Ukijikubali kuwa una ugonjwa wa kisukari ni rahisi sana kubadili mfumo wako mzima wa ulaji, hii inamaanisha kuwa mfumo wako wa ulaji unaweza kusababisha kupanda kwa sukari (glucose level) au kushuka kwa sukari. Ulaji wa vyakula vya wanga kwa wingi husababisha sukari kupanda. Kuacha kabisa ulaji na matumizi ya vitu ama vyakula vyenye sukari, kwa mfano soda, keki, barafu za sukari (ice cream), chokoleti n.k.
Pia kupunguza matumizi ya mafuta wakati wa uandaaji wa chakula na kuacha matumizi ya vyakula vyenye mafuta mengi kwa mafano ulaji wa viazi vya kukaanga (chips), maandazi, vitumbua, n.k. Ulaji wa mboga za majani/salad/kachumbari kwa wingi ni muhimu sana. Sahani ya chakula itawaliwe na mboga za majani,na hii ni kwa kila mlo yaani chakula cha asubuhi,mchana na cha jioni.
Mazoezi ya Viungo
Mazoezi ni muhimu kwa afya, mazoezi huchangamsha mwili,hupunguza mapigo wa moyo na kuyafanya kuwa ya wastani pamoja na kuongeza mzunguko wa damu kwa mtu wenye ugonjwa kisukari (hivyo hupunguza hatari ya kupoteza kiungo cha mwili kwa mgonjwa wa kisukari kutokana kuwa na mzunguko mzuri wa damu kwenye viungo vyake), mazoezi yana nafasi kubwa sana kwa sababu husaidia kuyeyusha lehemu (cholesterol) mwilini na kuondosha hatari ya kupata tatizo la kiharusi (stroke). Mazoezi yanayohitajika hapa ni yale ya kuchoma mafuta na sio ya kupanua misuli, mazoezi hayo ni kama kukimbia, kuruka kamba,kuogelea,kutembea kwa mwendo kasi. Mazoezi haya yafanyike kwa muda wa nusu saa au saa moja kila siku asubuhi au jioni.