Image

Ugonjwa wa kifua kikuu ni kati ya magonjwa matatu yanayotokea sana kwa watu masikini duniani (Disease of poverty). Magonjwa mengine katika jamii ya disease of poverty ni malaria na Ukimwi (AIDS). Ugonjwa wa kifua kikuu huathiri asilimia 98 ya watu katika nchi zinazoendelea, ukimwi asilimia 95 na malaria asilimia 90.

Magonjwa haya matatu husababisha vifo asilimia 10 ya idadi ya watu wote duniani kwa ujumla, ambapo inakisiwa watu wote duniani ni 6.91 bilioni kulingana na kituo cha kuhesabu watu cha Marekani ( US Census Bureau).

Kwa Tanzania, watu 120,191 hukisiwa kuwa na ugonjwa wa kifua kikuu kila mwaka, hii ni kutokana na taarifa ya shirika la USAID ya mwaka 2007. Kati ya watu hawa (120,191), 56,233 ni wale wanaogundulika kuwa na ugonjwa huu kupitia makohozi yaani sputum smear positive (SS+ ). Vifo vinavyotokana na ugonjwa wa kifua kikuu ni 32,000 kila mwaka nchini Tanzania.

Tanzania ni ya 15 kati ya nchi 22 ambazo zimeathiriwa sana na ugonjwa huu. Kati ya asilimia 50 ya wagonjwa wa kifua kikuu waliopimwa virusi vya ukimwi mwaka 2007, inakadiriwa ugonjwa wa ukimwi huathiri asilimia 47 ya wagonjwa wote wa kifua kikuu. Ugonjwa sugu wa kifua kikuu (Multidrug resistant tuberculosis) huathiri watu 1,300 nchini Tanzania kulingana na taarifa ya mwaka 2007.

Je, ugonjwa wa kifua kikuu husababishwa na nini?

Ugonjwa wa kifua kikuu, husababishwa na bakteria wanaojulikana kama Mycobacteria tuberculosis. Kuna aina nyingi za jamii ya Mycobacterium kama Mycobacteria tuberculosis (husababisha kifua kikuu), Mycobacteria leprae (husababisha ugonjwa wa ukoma), Mycobacteria bovis (huathiri ngombe na binadamu), Mycobacteria afrikanum na kadhalika.

Ugonjwa wa kifua kikuu unaweza kuathiri mapafu, mishipa ya fahamu, mifupa, mfumo wa mzunguko wa damu, ngozi, viunganishi vya mifupa (joints) na lymphatic system.

Mycobacteria bovis ambayo huathiri ngombe, inaweza kuambukiza binadamu kama atakula bidhaa zinazotokana na maziwa ya ngombe ambayo yameathirika na bakteria hawa kama vile siagi, mtindi, maziwa yenyewe, cheese, ice cream nk. Aina hii ya bakteria huathiri mapafu, tezi (lymph nodes), tumbo na sehemu nyingine za mwili.

Ni asilimia 10 tu ya watu walio na bakteria wa Mycobacteria tuberculosis ambao hawapati ugonjwa huu wa kifua kikuu.

Kati ya magonjwa yanayoathiri watu wengi sana duniani ni magonjwa ya zinaa. Haya ni magonjwa yanayoambukizwa kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine kupitia vitendo vya ngono. Vitendo hivi vya ngono vinaweza kuwa kujamiana, kupiga denda (kissing), vitendo vya ngono kwa kutumia mdomo (oral genital sex), kujamiana kupitia njia ya haja kubwa (anal sex) iwe kwa mwanamume na mwanamke au kati ya wanaume wenyewe na hata wale wanaotumia vifaa vya kufanyia ngono (vibrators). Magonjwa ya zinaa huathiri sana watu walio katika umri wa miaka 15 – 24 lakini hata kwa watu wengine ambao wana umri chini au zaidi ya huu niliotaja pia yanaonekana kwa wingi.

Kuna magonjwa ya zinaa zaidi ya ishirini yanayotambulika duniani, baadhi ya magonjwa ya zinaa ni

  • Kisonono (Gonorrhoea – “Gono” kama wengi wanavyopenda kuita kwa kifupi).
  • Chlamydia
  • Kaswende (Syphillis)
  • Human papilloma virus (HPV)
  • HIV/AIDS (Ukimwi/Upungufu wa kinga mwilini)
  • Hepatitis B, C, A
  • Herpes virus
  • Trichomoniasis
  • Bacteria Vaginosis
  • Pubic lice (chawa kwenye nywele za kinena)
  • Chancroid

Magonjwa mengi ya zinaa yanatibika lakini kuna baadhi ambayo hayana tiba ya uhakika kama HPV, Hepatitis B na C, na HIV. Mengine yameanza kuwa sugu kutokana na matumizi ya dawa za antibiotics bila mpangilio, magonjwa hayo ni kama gono (gonorrhoea) na nk.

Visababishi vya magonjwa ya zinaa

  • Vitendo vya ngono kama nilivyoeleza hapo awali
  • Kuanza vitendo vya ngono mapema au wakati wa umri mdogo
  • Kuwa na wapenzi wengi
  • Kufanya mapenzi ambao sio salama
  • Maambukizi kupitia michibuko au sehemu zilizokatika kwenye ngozi kwa kugusana na majimaji ya aina yoyote yanayotoka kwa mtu mwenye ugonjwa wa zinaa kama damu, shahawa nk. Hii inaweza kutokea bila mtu kujua kwani mara nyingi dalili za magonjwa ya zinaa zinakuwa hazionekani kwa wanawake na hata baadhi ya wanaume.

Watu wengi huhisi kitendo cha kula denda (kissing) ni salama lakini si kama wanavyofikiria kwani baadhi ya magonjwa kama kaswende, herpes nk, yanaweza kuambukizwa kupitia njia hii. Kondomu husaidia kupunguza maambukizi ya magonjwa ya zinaa kama gono, Chlamydia lakini sio kinga muafaka dhidhi ya magonjwa ya zinaa kama kaswende, genital herpes, genital warts, na magonjwa ya upungufu wa kinga mwilini (AIDS).

Nitaanza kuzungumzia ugonjwa wa gono (gonorrhea) kwa leo na makala zitakazofuata nitakuwa nazungumzia ugonjwa mmoja baada ya mwengine

Kisonono (gonorrhea) ni nini?

Kisonono ni ugonjwa kati ya magonjwa ya zinaa unaosababishwa na bakteria aina ya Neisseria gonorrhoeae, bakteria ambao hukuwa na kuzaliana kwa haraka katika sehemu zenye unyevunyevu na joto mwilini kama kwenye shingo ya kizazi kwa wanawake (cervix), mirija ya kupitisha mkojo au shahawa (urethra), mdomoni na kwenye puru. Maambukizi mengi kwa wanawake hutokea kwenye shingo ya kizazi (cervix). Asilimia 75 ya ugonjwa wa gono hutokea kwa watu wenye umri wa miaka 15 – 29, wanawake walio katika umri wa miaka 15 -19 na wanaume walio katika umri wa miaka 20 – 24 wako kwenye hatari zaidi ya kupata ugonjwa huu.

Ugonjwa huu huambukizwa vipi?

Ugonjwa huu huambukizwa kupitia vitendo vya ngono kupitia uke, njia ya haja kubwa (anus), kupitia mdomoni (oral sex). Ugonjwa unaweza kujitokeza kwenye sehemu za kujamiana, kwenye mdomo na kwenye puru (rectum). Ugonjwa wa gono huonekana sana kwa vijana, watu wenye maisha duni kiuchumi, watu wanaoishi mijini, watu weusi na watumiaji madawa ya kulevya.

Dalili za ugonjwa wa kisonono

Dalili za ugonjwa wa kisonono huanza kujitokeza kuanzia siku ya 2 hadi ya 7 baada ya mtu kupata maambukizi na huweza kuchelewa kwa wanawake. Dalili ni kama zifuatazo

Kwa wanaume

  • Kuhisi kama kichomi wakati wa kukojoa (burning sensation)
  • Kutokwa na majimaji ya njano au meupe au ya kijani kutoka kwenye uume yanayoambatana na maumivu makali sana
  • Wakati mwengine maumivu au kuvimba kwa korodani (swollen testicles)
  • Maambukizi yakiwa kwenye puru (rectum) huambatana na maumivu wakati wa kujisaidia haja kubwa, kuwashwa sehemu za haja kubwa, na hata haja kubwa inaweza kutoka ikiambatana na damu, hii inatokea kwa wanaume na wanawake.

Kwa wanawake

Dalili kwa wanawake huwa si nyingi lakini wanawake wengi hawaonyeshi dalili zozote

  • Maumivu au kuhisi kama kichomi wakati wa kukojoa
  • Kuongezeka kwa kutoka majimaji kutoka kwenye tupu ya mwanamke ambayo ni ya njano au yamechanganyika na damu
  • Kutokwa na damu kupitia tupu ya mwanamke kabla ya hedhi kufika.
  • Kutokwa na damu baada ya kujamiana au baada ya tendo la ndoa
  • Kichefuchefu
  • Homa (fever)
  • Kutapika

Vipimo vya ugonjwa wa kisonono

  • Swab for culture – Kipimo hiki hufanyika maabara kwa kupandikiza bakteria baada ya kufuta sehemu za siri kwa kutumia swab ili kuona kama kuna bakteria wanaosababisha gono.
  • Polymerase Chain Reaction (PCR) – Kipimo cha kuangalia vina saba (DNA) ya bakteria, ni ghali sana.

Tiba ya ugonjwa wa kisonono ni nini?

Tiba ya gono inahusisha na tiba ya ugonjwa wa Chlamydia kwani mara nyingi magonjwa haya huambatana kwa pamoja.Tiba hutegemea na umri wa mgonjwa na kama mtu ni mjamzito au la. Tiba ya gono ambayo sio sugu iliyo kwenye shingo ya kizazi (cervix), urethra na puru, dawa zinazotumika ni aina za cephalosporin dozi moja pamoja na dawa za aina ya macrolide antibiotics (mfano azithromycin) na za jamii ya penicillin (mfano doxycyclin) ili kutibu ugonjwa wa chlamydia. Mara nyingi kwa wale chini ya miaka 18 na wanawake wajawazito, hutibiwa kwa kuchomwa sindano.

Fuata ushauri wa daktari kabla ya kutumia dawa hizi kwani dawa nyingi zina madhara kwa wajawazito (mfano doxycyclin). Ushauri nasaha hutolewa kwa wapenzi wote wawili na ni vizuri wapenzi wote wawili kutibiwa hata kama mmoja hana dalili za ugonjwa huu.

Madhara ya ugonjwa wa kisonono

  • Kutoweza kuzaa kwa mwanamke (tasa) au kutoweza kutungisha mimba kwa mwanamume (infertility)
  • Huweza kuathiri moyo (heart valves), ubongo,ngozi nk ambayo ni hatari sana kwa mtu yoyote.
  • Madhara kwenye sehemu za maungio au jointi (joint inflammation)
  • Kwa wanawake wale ambao hawajatibiwa wanaweza kupata ugonjwa wa PID (Pelvic Inflammatory Disease) ambao huongeza asilimia ya mwanamke kuwa tasa.
  • Wale wanawake ambao ni wajawazito na wameambukizwa gono wako kwenye hatari ya mimba kutoka au kuzaa mapema kabla mimba haijatimiza umri wake (preterm labor).
  • Kwa wale wanaoambukizwa gono kipindi cha kukaribia kujifungua, wanaweza kuwaambukiza watoto wao na hivyo watoto kupata ugonjwa wa uti wa mgongo (meningitis), kuwa kipofu (blindness), homa ya mapafu (pneumonia) na ugonjwa wa mifupa (septic arthritis).

Kinga ya kisonono

  • Kutumia kondomu wakati wa kujamiana
  • Kuwa na mpenzi mmoja mwaminifu
  • Kuacha vitendo vya ngono kama matumizi ya vifaa vya ngono hasa kwa wanawake mfano vibrators nk.
  • Kwa wanawake wajawazito – Hakikisha unahudhuria kliniki mapema ili upate kuchunguzwa na kupatiwa tiba muafaka kama utagundulika na ugonjwa wa gono au ugonjwa mwengine wowote.
  • Wanawake wajawazito wanashauriwa kujifungulia hospitali ili kama mtoto ameathirika na gono apate matibabu ya haraka baada ya kuzaliwa kuepusha kuwa kipofu.
  • Epuka kufanya ngono na mtu aliyeambukizwa gono.

“Kumbuka ya kwamba hakuna kitu kama ngono salama kwani huwezi kujua kama wewe au mwenzako wakati wa kujamiana ameathirika au la, au una michibuko au umekatika kwenye ngozi au la kwani michibuko mengine inaweza isionekane au kugundulika kwa urahisi. Njia pekee na nzuri ni kuacha au kujikinga na vitendo vya ngono”. Mtu aliyepata gono awali anaweza kupata tena.

Usikose mwendelezo wa makala hii.........

 

Daktari mmoja aitwaye Mackod, alipitia makala nyingi za afya ili kuweza  kutambua visababishi vya vifo ambayo havitokani na umri au nasaba ya kiasili (Genetic), na akagundua mambo tisa ambayo yanasabisha vifo ambavyo vingeweza kuzuilika. Mambo hayo tisa ni; uvutaji wa sigara, unywaji wa pombe, kutofanya wa mazoezi, lishe duni, wadudu kama bakteria na virusi, ajali, tabia za ngono za kupita kiasi bila kinga,  vita na madawa ya kulevya.

Katika makala hii ningependa kuzungumzia juu ya ufanyaji wa wazoezi na hasa wakati bora wa kufanya mazoezi. Mazoezi ni muhimu sana kwa ajili ya kupunguza mafuta ya ziada mwilini, tafiti zinaonesha kuwa asiyefanya mazoezi, madhara anayopata ni sawa na mtu anayevuta tumbaku.

Utafiti uliofanywa na Dr. Jason na Nor Farah (2004) wa Chuo kikuu cha Glasgow, umeonesha kuwa unapofanya mazoezi kabla ya kifungua kinywa, wakati tumbo likiwa tupu, ni bora zaidi kuliko unapoweza kufanya mazoezi baada ya mlo wowote. Kufanya mazoezi ni jambo la maana kwa afya kuliko kutokufanya mazoezi ya mwili, lakini unaweza kupata  faida zaidi kama unaweza kufanya kabla hujala chochote.

Mazoezi kwa ujumla wake yana umuhimu mkubwa kwa afya ya binadamu, hasa kama yakiambatana na lishe bora. Mazoezi huweza kuzuia magonjwa sugu kama kisukari, magonjwa ya moyo, kansa na shinikizo la damu, pia kwa kufanya mazoezi unaweza kuongeza kipato kwa kuwa unaweza kufanya kazi muda mrefu kuliko asiyefanya mazoezi.

Familia ambazo hufanya mazoezi huwa na afya bora na kipato kikubwa kwa kuwa fedha kidogo wanazopata hutumika kwenye maendeleo tofauti na familia zisizofanya mazoezi ambazo hujikuta wakitumia kipato hicho kidogo kwa ajili ya kutibu  magonjwa ambayo yangeepukika kwa kufanya mazoezi.

 

Utangulizi

Surua ni mojawapo ya magonjwa ya kuambukiza yanayotisha kwa binadamu. Huu ni ugonjwa ulio na kiwango cha juu cha karibu asilimia 100 cha mashambulizi pindi mtu apatapo vimelea vya ugonjwa huu.

Pamoja na kuwepo chanjo ya ugonjwa huu, bado surua ni miongoni mwa magonjwa yanayosababisha vifo vingi vya watoto walio chini ya umri wa miaka 5 katika baadhi ya maeneo duniani hasa kwa nchi zinazoendelea. Ugonjwa huu ambao ulitoweka katika baadhi ya nchi, umeanza kuonekana tena hivi karibuni miongoni mwa watu ambao hawakupata chanjo katika nchi za Uingereza na nyingine za Ulaya.

Surua husababishwa na nini?

Surua huenezwa na aina ya virusi jamii ya paramyxovirus. Jamii hii ya virusi hupatikana katika mfumo wa njia ya hewa. Hukaa katika kamasi na majimaji yaliyopo katika mfumo wa hewa. Kwa sababu hii basi virusi hawa huenezwa kwa njia ya upumuaji. Virusi hawa wanaweza kuishi hewani kwa muda wa hadi saa moja baada ya kutolewa kwa kupiga chafya au kukohoa au hata mazungumzo na mgonjwa. Hii ina maana kuwa, ili kuambukizwa surua, si lazima mtu akutane uso kwa uso na mgonjwa. Baada ya kuingia ndani ya mfumo wa hewa virusi hushambulia seli za utando wa nje wa njia ya hewa (respiratory tract epithelium) na kuingia katika mzunguko wa wa limfu na kufika kwenye tezi zilizo karibu. Katika tezi huzaliana zaidi na kusambaa mwilini.

Utangulizi

Mada hii ina lengo la kuzungumzia tatizo la kuwa na hofu au wasiwasi uliopita kiasi au kwa kitaalamu Generalized anxiety disorder (GAD). Kwa ajili ya kutofautisha kati ya hofu iliyopitiliza na hofu ya kawaida ambayo yaweza kumkumba mwanadamu yeyote, wakati fulani fulani mwandishi atatumia maneno anxiety au GAD katika kuwasilisha ujumbe wake.

Hofu iliyopitiliza au au anxiety au GAD huambatana na hali ya kuwa na wasiwasi kupita kiasi juu ya maisha ya kila siku pamoja na matukio yake bila hata muhusika kuwa na sababu maalum ya kuwa na hofu hiyo. Kwa maneno mengine ni kuwa, watu wenye anxiety hujihisi hofu kubwa bila ya kuwa na sababu yeyote ya msingi ya kuwafanya wawe hivyo. Mara nyingi watu wenye tatizo hili huwa na tabia ya kuhisi kwamba janga kubwa litawatokea karibuni au maafa yatamkumba katika maisha yake na daima hawaachi kuwa na hofu isiyo na sababu juu ya familia zao, pesa, afya, ajira, masomo au hata biashara zao.

Maisha yao ya kila siku huwa na mchanganyiko wa hofu, wasiwasi na huzuni, kiasi kwamba hatimaye hofu hutawala mawazo  ya muhusika kiasi cha kuingilia utendaji wake wa kila siku ikiwemo kazi, masomo, shughuli zake za kijamii, na hata mahusiano na mwenza wake wa ndoa.

Dalili za hofu iliyopitiliza (anxiety) ni nini?

Katika sehemu hii ya pili ya muendelezo wa makala ya magonjwa ya zinaa tutazungumzia kuhusu ugonjwa wa Chlamydia.

Chlamydia ni nini?

Chlamydia ni aina ya ugonjwa wa zinaa unaosababishwa na bakteria aina ya Chlamydia trachomatis ambao wanaweza kuathiri viungo vya uzazi na pia husababisha aina ya homa ya mapafu ijulikanayo kama atypical pneumonia.

Miongoni mwa magonjwa ya zinaa yasababishwayo na bakteria, Chlamydia unaoongoza kwa maambukizi duniani ambapo kwa nchi ya Marekani pekee inakisiwa watu milioni 4 huambukizwa kila mwaka. Kutokana na ukosefu wa takwimu za nchi nyingi barani Afrika ikiwemo Tanzania, ni vigumu kujua idadi kamili ya maambukizi, ingawa bila shaka ndio ugonjwa wa zinaa utokanao na bakteria unaoongoza kwa maambukizi ukifuatiwa na ugonjwa wa gonorrhea.

Clamydia huambukizwaje?

Chlamydia huambukizwa kupitia njia zifuatazo

  • Kujamiana kwa njia ya mdomo, njia ya haja kubwa na kupitia tupu ya mwanamke
  • Kuambukizwa kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto wakati wa ujauzito
  • Au kupitia manyoya au vinyesi vya wanyama kama ndege walioambukizwa aina ya Chlamydia inayopatikana kwa ndege kama vile kuku, bata, kasuku nk. Aina hii ya clamydia husababisha aina ya homa ya mapafu ijulikanayo kama psittacosis ambayo huambatana na homa kali yenye nyuzi joto kati ya 39.4 - 41.1 celsius

Chlamydia huathiri sehemu tofauti za mwili wa binadamu kama vile macho, mfumo mzima wa kupumua, sehemu za siri, viungo vya uzazi na tezi (lymph nodes). Chlamydia na gonorrhea huwa na tabia ya kuambatana kwa pamoja (rejea makala ya magonjwa ya zinaa sehemu ya kwanza).

Dalili na viashiria vya ugonjwa wa Chlamydia

Asilimia 75 ya wanawake na asilimia 50 ya wanaume wanaopata maambukizi ya ugonjwa huu huwa hawaoneshi dalili zozote za ugonjwa wa Chlamydia. Dalili hutokea wiki 1 hadi 3 baada ya mtu kupata maambukizi.

Dalili kwa wanawake zinaweza kuwa

  • Kutokwa na majimaji ya rangi ya njano yenye harufu kali na mbaya sehemu za siri
  • Maumivu wakati wa kukojoa (haja ndogo)
  • Kuhisi kama kuwaka moto wakati wa kukojoa
  • Kutokwa na damu katikati ya kipindi cha hedhi yaani baada ya kumaliza mzunguko wa hedhi na kabla ya kuanza mzunguko mwengine wa hedhi
  • Maumivu sehemu ya chini ya tumbo
  • Maumivu wakati wa kujamiana
  • Kutokwa na damu wakati wa kujamiana
  • Kuvimba na maumivu kwenye tezi zilizopo sehemu za siri

Dalili kwa wanaume zinaweza kuwa

  • Maumivu wakati wa kukojoa
  • Kuhisi kama kuwaka moto wakati wa kukojoa
  • Kutokwa na majimaji kwenye uume yanayoweza kuwa ya rangi nyeupe kama maziwa, kijivu au ya njano
  • Sehemu ya tundu la uume huwa jekundu, huvimba na kuwasha
  • Maumivu kwenye korodani
  • Tezi zilizopo sehemu za siri huvimba na huambatana na maumivu

Mara nyingi dalili hizi kwa wanaume zinakuja na kupotea au zinaweza kuonekana tu wakati anaenda kukojoa asubuhi baada ya kuamka kutoka usingizini

Dalili za ugonjwa huu kama umeathiri puru (rectum) ni kama ifuatavyo (kwa wanawake na wanaume)

  • Kuwashwa na kutokwa na damu kwenye puru
  • Maumivu wakati wa kujisaidia haja kubwa
  • Kutokwa na uchafu kama kamasi kwenye puru

Dalili za chlaymdia iliyoathiri macho (kwa wanawake na wanaume)

  • Kuvimba sehemu za macho
  • Macho kuwa mekundu, kuwasha na hata kutokwa na majimaji

Chlamydia inayoambukiza kwenye macho (Chlamydia conjunctivitis or trachoma) ndio inayoongoza kwa kusababisha upofu duniani.

Vipimo vya uchunguzi

  • Urethral swab for culture – Majimaji kutoka kwenye uume au uke huchukuliwa kwa kutumia swab maalum ambapo hupelekwa maabara ili kuotesha na kuangalia aina ya uoto wa bakteria
  • Urinalysis (urine test) – Vipimo vya mkojo
  • Polymerase Chain Reaction (PCR) – Kipimo cha kuangalia vinasaba vya bakteria na hufanyika maabara.

Tiba ya ugonjwa wa Chlamydia

Chlamydia ni kati ya magonjwa ya zinaa yanayotibika. Ugonjwa huu hutibiwa kwa dawa aina ya antibiotics zilizopo kwenye makundi ya ;

  • Macrolide antibiotics
  • Quinolones antibiotics
  • Polyketides antibiotics

Madhara ya ugonjwa huu

  • Kwa wanaume, Chlamydia huathiri korodani na kusababisha mwanamume kukosa uwezo wa kutia mimba mwanamke (infertility) na maambukizi
  • Maambukizi kwenye tezi dume (prostatitis)
  • Kwa wanawake, husababisha maambukizi kwenye mirija ya uzazi, mfuko wa uzazi, na mayai ya uzazi hivyo kusababisha ugonjwa aina ya Pelvic inflammatory disease (PID). Pia huongeza asilimia ya mwanamke kupata mimba zinazotunga nje ya mfuko wa uzazi (Ectopic pregnancy). Mbali na hilo, mwanamke hupata maumivu sugu ya kwenye nyonga, ugonjwa wa mifupa arthritis aina ya Reiters syndrome. Vilevile, Chlamydia huweza kusababisha ugumba kwa mwanamke kama hatapata tiba.
  • Kwa wajawazito, Chlamydia husababisha wanawake kujifungua kabla wakati. Mtoto anaweza kuzaliwa na maambukizi kwenye masikio, sehemu za siri, macho na kwenye mapafu (homa ya mapafu). Kama mtoto hatapata tiba ya haraka ya macho basi anaweza kuwa kipofu.

Dalili za Chlamydia kwa watoto wachanga hutokea ndani wiki mbili kwenye macho na homa ya mapafu (pneumonia) ndani ya wiki 2 hadi miezi 3 baada ya kuzaliwa.

Jinsi ya kujikinga na ugonjwa wa Chlamydia

  • Kama ilivyoelezwa kwenye makala iliyopita, njia sahihi ya kujikinga na magonjwa ya zinaa ni kuacha au kuepuka kufanya ngono au kujamiana.
  • Kwa wanawake wajawazito, ni vizuri kuhudhuria kliniki mapema wakati wa ujauzito
  • Wale wenye maambukizi wanashauriwa kuchukua tahadhari ya kutowaambukiza wapenzi wao kwa kufanya ngono salama (kutumia mipira), kuepuka kushika macho kwa kutumia mikono na hata ikiwezekana kuwaepuka wapenzi wao ili kuwalinda na maambukizi.
  • Kwa wale ambao wapenzi wao wameambukizwa au wameonyesha dalili za ugonjwa huu, wanashauriwa na wao kupata tiba hata kama hawana dalili zozote.
 

Madhara ya ugonjwa wa kaswende katika mfumo wa mishipa ya fahamu hutokea miaka 10-20 baada ya mtu kuugua ugonjwa wa kaswende na ambaye hakupata tiba yoyote hapo awali. Madhara haya huonekana kwenye uti wa mgongo na kwenye ubongo.

Kuna aina nne ya neurosyphilis kama ifuatavyo

  • Isiyo na dalili (Asymptomatic) – Katika aina hii mgonjwa anakuwa hana dalili zozote. Aina hii ndio huonekana sana kwa wagonjwa ambao hawakupata tiba hapo awali.
  • Ulemavu wa jumla (General paresis)
  • Inayoshambulia tando za ubongo na mishipa ya damu (Meningovascular)
  • Inayoshambulia sehemu za chini za uti wa mgongo (Tabes dorsalis)

General paresis hutokana na kuathirika kwa ubongo na hivyo kuleta upungufu katika ufanyaji kazi wa ubongo (impairement of mental function). Aina hii pia huweza kutokea kwa wagonjwa wa kisonono (gonorrhoea).

Dalili za general paresis

  • Kupungua uwezo wa kuzungumza (aphasia)
  • Kupungua uwezo wa kufanya maamuzi (impaired judgement)
  • Kutokuwa na uwezo wa kuhesabu kitu chochote
  • Kupungua kuhamasishika (impaired motivation)

Ugonjwa wa matende ni aina ya ugonjwa unaosababisha ngozi na  tishu zilizo chini ya ngozi ya  mwanadamu kuwa nene (thickening of skin and underlying tissue).Ugonjwa huu  huathiri  miguu, mikono, figo,  korodani  na kusababisha korodani  kuvimba na kuwa kubwa sana.Inakisiwa watu milioni 120 duniani wana maambukizi ya ugonjwa huu ambapo kati yao milioni 40 wamepata madhara makubwa kutokana na ugonjwa huu.Kati ya hawa walioathirika theluthi moja huapatikana katika bara la Afrika, theluthi moja nyingine hupatikana India, na kiwango kilichobakia hupatikana katika  visiwa vya Pacific, Marekani na Asia ya kusini.

Ugonjwa wa matende husababishwa  na vimelea aina ya minyoo (parasitic worm) vinajulikana kama Wuchereria bancrofti, Brugia malayi, B. timori ambavyo huenezwa na mbu jike aina ya  culex quinquefasciatus mosquitoes na jamii fulani ya mbu dume (Anopheles species) wakati minyoo aina ya  Brugia roundworms huenezwa mbu wanaojulikana kama  Mansonia mosquitoes. Mbu hawa hueneza ugonjwa huu kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwengine.
 
Aina nyingine ya ugonjwa wa matende inayojulikana kama nonparasitic elephantiasis au podoconiosis ambayo haisababishwi na vimelea vyovyote hupatikana katika nchi za Afrika Mashariki (Kenya, Uganda, Tanzania, Rwanda, Burundi) Sudan, Egypt na Ethiopia. Asilimia 6 ya maambukizi ya aina hii ya podoconiosis hupatikana nchini Ethiopia.

Nini hutokea baada ya maambukizi?

Kwa kawaida mtu aliyeambukizwa ugonjwa huu huwa na mabuu (larvae) kwenye mfumo wa damu mwilini mwake wanaojulikana kama microfilariae. Mabuu haya husafiri kutoka kwenye mfumo wa damu hadi kwenye mfumo mwingine unaojulikana kama mfumo wa limfu (lymphatic system) na kukua kuwa minyoo kamili (adult worms) ambayo huziba mfumo huu wa limfu ambao unategemewa sana katika kuweka uwiano sawa  wa maji (fluid balance) kati ya mfumo wa damu na tishu ndani ya mwili na husaidia kuupa mwili kinga dhidhi ya magonjwa mbalimbali. Minyoo hii huishi kwa miaka minne hadi sita na katika uhai wake huzaa mamilioni ya mabuu (microfilariae)  mengine wakati ikiwa kwenye mfumo wa damu.

Mbu huenezaje ugonjwa huu?

Mtu ambaye ameambukizwa ugonjwa huu huwa na mabuu kwenye mfumo wake wa damu na anapongatwa na mbu ambawo wanauwezo wa kuchukua mabuu haya  ambayo  huendelea kukua na kufikia hatua ya kuambukiza mtu mwingine ndani ya mwili wa mbu.Kwa kawaida, ukuaji huu wa mabuu ndani ya mwili wa mbu huchukua wiki moja hadi tatu na baada ya kukua na kufikia hatua ya kuambukiza mtu mwingine, mabuu haya husogea mpaka kwenye sehemu ya mdomo wa mbu ambayo ndio huwa humng'ata mtu wakati mbu anapofyonza damu kutoka kwa mtu. Mbu mweye mabuu kwenye mdomo wake anapomngata mtu ili kufyonza damu, ndipo mabuu haya yanapoingia kwenye mwili wa mtu na hivyo kusababisha maambukizi ya ugonjwa huu.

Dalili za ugonjwa huu ni zipi?

• Dalili kubwa ya ugonjwa huu ni kuvimba sehemu ya chini ya mwili yaani kwenye miguu na vidole.Pia mtu anaweza kuvimba sehemu ya mikono au mkono wote pamoja na vidole vya mkononi. Wengine huvimba kwenye korodani (wanaume).
• Kuhisi uzito na kukamaa kwa mikono au miguu kutokana na uvimbe uliopo.
• Kutoweza kutumia kiungo husika kilichovimba.
• Maumivu au kutohisi vizuri kwenye mikono au miguu.
• Kupata maambukizi ya mara kwa mara kwenye sehemu iliyovimba.
• Ngozi kuwa nene na ngumu kwenye mikono au miguu.

Dalili nyingine ni pamoja na

  • Homa
  • Maumivu ya kichwa
  • Maumivu kwenye jointi na mifupa 
  • Kutapika
  • Vidonda kwenye mikono au miguu
  • Mistari ya rangi nyekundu inayoonekana kwenye mikono au miguu (red streaks)

Vipimo vya uchunguzi

• Blood examination under microscope - Kipimo cha kuangalia damu kwenye hadubini  ili kuangalia kama kuna mabuu ya ugonjwa huu wa matende.Kwa wale ambao wana ugonjwa huu kwa muda mrefu, mabuu hayaonekani kwenye damu kwani tayari yatakuwa yameshaingia kwenye mfumo wa limfu. Hivyo, kutoonekana kwa mabuu kwenye damu kwa kutumia hadubini si kigezo cha kusema kwamba mgonjwa hana ugonjwa huu wa matende.
• Vipimo vyengine vinavyoweza kutumika ni pamoja na CT Scan, MRI, Doppler Ultrasound, Radionuclide Imaging ili kuweza kutofautisha ugonjwa huu na magonjwa mengine yanayosababisha kuvimba kwa miguu au mikono kama saratani za  aina mbalimbali, kuganda kwa damu kwenye mishipa ya damu (blood clot) na kadhalika.
• Kwa wale wenye kuvimba korodani, ni muhimu kwa daktari  kuchukua kipimo kwa kukwangua sehemu husika kisha kuchanganya na potassium hydroxide na kutazama kwenye hadubini kama kuna dalili (Meddler bodies, sclerotic bodies)  za ugonjwa wa fangasi unaojulikana kama chromobalstomycosis  (unaosababishwa na fangasi aina ya Fonsecaea pedrosoi, Phialophora verrucosa, Cladosporium carrionii, au Fonsecaea compacta). Pia ukungu huu huweza kuoteshwa maabara ili kuangalia kama kuna fangasi aina yoyote ile niliyotaja hapo juu watakaota.

Tiba ya ugonjwa wa matende ni nini?

Tiba ya ugonjwa wa matende hutegemea na sehemu husika. Kwa wagonjwa walio katika jangwa la sahara, tiba ni dawa aina ya albendazole pamoja na ivermectin. Kwa wagonjwa waliopo sehemu nyingine duniani tiba huusisha matumizi ya albendazole pamoja na diethylcarbamazine.
 
Kusafisha sehemu iliyoathiriwa na ugonjwa wa matende mara kwa mara husaidia kupunguza dalili na viashiria vya ugonjwa huu.
 
Kwa wale waliovimba korodani kutokana na ugonjwa wa matende, tiba yake ni upasuaji.Wakati mwingine, kama mgonjwa atakuwa amevimba sana korodani, basi baada ya kufanyiwa  upasuaji wa kawaida, atahitaji kufanyiwa upasuaji kurekebishwa ngozi yake (plastic surgery).
 
Katika utafiti uliofanywa na chuo cha Liverpool school of tropical medicine mwaka 2005, umeonyesha dawa ya antibiotiki hususan doxycyline inaweza kutumika kutibu ugonjwa huu wa matende kutokana na  minyoo (adult worms) kuwa na bakteria aina ya wolbachia wanaoishi ndani ya minyoo hii, hivyo dawa hii hutibu kwa kuua bakteria hawa na kusababisha minyoo hii kufa, na kuondosha kabisa microfilariae kwenye damu ya mgonjwa na  hivyo mgonjwa kupona. Dawa hii hutumika kwa muda wa wiki 8. Hata hivyo, kama mgonjwa atakuwa na mabuu ndani ya mfumo wake wa limfu, basi itakuwa vigumu kwake kupona. Utafiti zaidi unahitajika ili kuwa na uhakika zaidi juu ya dawa hii kutibu ugonjwa huu.

Kinga ya ugonjwa wa matende ni nini?

• Shirika la afya duniani (WHO) limeanzisha jitihada za kutokomeza ugonjwa huu wa matende ifikapo mwaka 2020.
• Matumizi ya  dawa aina ya albendazole kwa wale walio katika hatari kupata ugonjwa wa matende unaosababishwa na vimelea.
• Kuvaa viatu wakati wa kutembea nje ili kujikinga kupata maambukizi ya aina ya podoconiosis.
• Kuosha miguu na mikono kwa kutumia maji na sabuni
• Kuosha miguu kila siku kwa kutumia antiseptic (bleach).

Marejeo

1. Nidhi Sharma, Y.S.Marfatia: Genital elephantiasis as a complication of chromoblastomycosis: A diagnosis overlooked, Indian J Sex Transm Dis. 2009 Jan-Jun; 30(1): 43–45.  
2. McNeil, Donald (2006-04-09). "Beyond Swollen Limbs, a Disease's Hidden Agony". New York Times. Retrieved 2008-07-17.
3. Davey, Gail (2008). "Podoconiosis: let Ethiopia lead the way". The Ethiopian Journal of Health Development 22 (1): 1–2.
 
 

Katika tafiti mpya zilizofanywa hivi karibuni zinaonyesha kuwa unyongovu na jaribio la kujiua ni viashiria hatari ambavyo huleteleza vijana kufa kwa magonjwa ya moyo.

Katika utafiti mkubwa uliohusisha washiriki zaidi ya 7000 walio chini ya miaka 40 ulionyesha kuwa kwa wale waliokuwa na historia ya unyongovu au jaribio la kujiua walikuwa na hatari kubwa zaidi ya kufa kutokana na magonjwa ya moyo hasa yale ambayo moyo hukosa oksijeni ya kutosha (ischemic heart disease) ukilinganisha na wale ambao hawakuwa na historia hiyo.

Ingawa jinsia zote zilikuwa kwenye hatari zaidi ya kufa kutokana na magonjwa ya moyo, lakini wanawake wenye unyongovu au waliofanya jaribio la kujiua walikuwa na hatari mara 14 zaidi ya kufa kwa magonjwa ya moyo yatokanayo na kukosa oksijeni ya kutosha (ischemic heart disease) kulinganisha na wale ambao hawakuwa na unyongovu au jaribio la kujiua.

Katika utafiti huu uliofanywa na Profesa Viola Vaccarino kutoka chuo kikuu cha Emory, Atlanta, Georgia aligundua jinsi matatizo ya kisaikolojia yanavyopelekea kuongeza hatari ya kufa mapema na magonjwa ya moyo katika idadi ya vijana.

Taarifa nyingi zilizopo za magonjwa ya moyo ambazo zilizokwisha tolewa huwa za umri wa kati na wazee, maana imekuwa ikizoeleka magonjwa haya huathiri zaidi rika hiyo, ambayo ni kweli kabisa hasa katika magonjwa yanao athiri zaidi mishipa ya damu ya moyo (CHD).

Naitwa Kissu K. Mpini, ni mwenyeji wa wilaya ya Ifakara,mkoa wa Morogoro, Tanzania, utakumbuka mara ya mwisho nilivyotoa ushuhuda wangu kuhusu shida ya kusigina/kusaga meno-bruxism ilivyonitatiza kwa muda mrefu bila kupata nafuu, kwa kifupi baada ya kupata huduma pale kwenye hospitali ya Taifa Muhimbili, Kitengo cha Meno, ninaendelea vizuri sana kwa sasa, ninalala usingizi vema, na kazi zangu nazifanya vizuri, hakika nimekuwa mwenye furaha kama wenzangu.

Utakumbuka nilijiuliza sana kama watoto pia hupata tatizo la kusigina meno kama inavyotokea kwa watu wazima, hivyo ili kukata mzizi wa fitina, nilimwandikia barua daktari aliyenihudumia pale Muhimbili siku ile, nimeona ni vema pia elimu aliyonipatia daktari nishirikishe wadau wengine, maana sio wote tunaweza kufika Muhimbili kirahisi, vilevile ninaamini kuwa yeyote atayeweza kusoma maelekezo haya ya daktari itakuwa ni msaada mkubwa sana kwake binafsi, familia na rafiki zake. Majibu ya daktari yamebainisha kwa kirefu kuhusu tatizo la kusigina meno linavyoathiri watoto, ifuatayo ni barua ya daktari kama alivyoniandikia.

Tafiti zinaonesha kuwa asilimia 20 ya watoto kati ya mwaka 1 hadi miaka 11 husumbuliwa na kusigina/kusaga meno tatizo ambalo kwa kitaalamu linajulikana kama Bruxism. Ingawa takwimu hii inakadiriwa kuwa chini ya hali halisi kwa vile wazazi wengi wanashindwa kutambua tatizo hili kwa watoto wao.

Kama ilivyo kwa watu wazima kwa vyanzo mbalimbali vinavyosababisha kusigina meno, kwa watoto dalili za tatizo hili zinafanana sana na matatizo mengine ya watoto hivyo inawawia vigumu wazazi ama walezi kutambua tatizo hili na hata kupuuzia.

Ukurasa 5 ya 12