Image

Fangasi wapo kila mahali, kwenye miti, mimea, mchanga, ndani majumbani mwetu na hata kwenye ngozi ya binadamu.Aina nyingi ya fangasi hawasababishi madhara yoyote kwa binadamu isipokuwa wachache tu. Kuna aina milioni moja na nusu za wadudu aina ya fangasi wanaotambulika duniani, kati yao ni fangasi 300 tu wanaojulikana kusababisha maambukizi kwa binadamu .1,2 Uvutaji wa hewa iliyochanganyika na  mazalia ya fangasi yanayojulikana kama fungal spores pamoja na uwepo wa uvamizi au ukuaji wa fangasi kwenye ngozi ya binadamu husababisha maambukizi ya fangasi, hivyo basi maambukizi mengi ya fangasi huanza kwenye  mapafu au kwenye ngozi ya mtu.

Takribani watu milioni 984 walipata maambukizi ya fangasi kwenye ngozi  mwaka 2010 na hivyo kufanya maambukizi haya kuwa ugonjwa namba nne katika magonjwa yote kwa mwaka huo 3.

Watu walio kwenye hatari ya kupata maambukizi ya fangasi ni kama wafuatavyo;

  • Wagonjwa wanaotumia dawa za kuua vimelea vya wadudu bila kufuata masharti ya daktari -Dawa aina ya antibayotiki (antibiotics)
  • Wale wenye kinga dhaifu - Wagonjwa wa ukimwi,wagonjwa wa kisukari, wagonjwa wanaotumia dawa za jamii ya steroid, wagonjwa wanaotumia dawa za kutibu saratani (chemotherapy drugs), immunosuppressive drugs, wagonjwa wanaotibiwa kwa mionzi na  wajawazito
  • Watoto wadogo na wazee - Ingawa watu wote wapo kwenye hatari ya kupata maambukizi ya fangasi, hatari kubwa ipo kwenye kundi hili la wazee na watoto kutokana kuwa na kinga dhaifu

Aina za maambukizi ya fangasi

  1. Maambukizi ya fangasi nje ya mwili (Superficial mycoses) - Ni fangasi ambao husababisha maambukizi kwenye ngozi, nywele, kucha na hawaishi kwenye tishu mwilini. Fangasi aina hii hujulikana kama Dermatophytes.Fangasi hawa hushambulia sehemu tajwa hapo juu kwa kutoa vimengenyo (Extracellular enzymes) vinavyolainisha protini aina ya keratin inayopatikana katika maeneo hayo.Maambukizi haya ya fangasi yamegawanyika katika
  2. Tinea Corporis - Maambukizi ya fangasi yanayopatikana katika sehemu yoyote ile mwilini.
  3. Tinea Pedis (Athlete’s foot)-Maambukizi ya fangasi katikati ya vidole vya miguuni na kwenye nyao za miguu
  4. Tinea Unguium (Onchomycosis) - Maambukizi haya yanapatikana kwenye kucha za vidole vya miguuni na vya mikononi
  5. Tinea Capitis – Huonekana kwenye kichwa hasa kwa watoto wadogo.Husababisha mapunye kwenye kichwa, nywele kunyofoka, mabaka meusi kwenye kichwa yaliyoambatana na mcharuko (Inflammation), kutokwa na magamba kichwani, kuwashwa na kuvimba vimba  kwenye kichwa
  6. Tinea Cruris – Maambukizi ya fangasi sehemu za siri
  7. Tinea Barbae – Huonekana maeneo yenye ndevu kwenye uso na shingoni
  8. Tinea Vesicolor – Maambukizi ya fangasi kwenye ngozi ya watu wazima.Maambukizi haya hayaonekani kwenye uso ila husababisha ngozi kuwa na mabaka yenye rangi ya kahawia iliyochanganyika na rangi nyekundu (reddish brown).Tinea vesicolor huonekana sana kwenye ngozi ya watu wanaoishi sehemu zenye joto kali au wenye matatizo kwenye vichocheo vya miili yao (hormonal abnormalities) ingawa wote wanaopata maambukizi haya huwa ni watu wenye afya njema.
  9. Subcutaneous Mycoses- Maambukizi ya fangasi kwenye tishu chini ya ngozi zinazojulikana kama dermis, subcutaneous tissue, fascia na kwenye misuli.Fangasi wanaosababisha maambukizi haya hupatikana kwenye mchanga na mimea.Maambukizi haya sugu hutokea pale mtu anapokuwa na kidonda na hivyo kurahisisha fangasi kuvamia mwili.Magonjwa yanayosababishwa na fangasi kwenye tishu chini ya ngozi ni kama yafuatayo;
  • Sporotrichosis
  • Chromoblastomycosus
  • Mycetoma
  • Phaeohypomycosis 

Sporotrichosis

Husababishwa na fangasi aina ya Sporothrix schenckii.Fangasi hawa hupatikana kwenye mimea, miti, nyasi na kwenye maua aina ya waridi. Maambukizi yanayotokea kwenye mikono na miguu ingawa kwa watoto huonekana sana sehemu za usoni.Pia huweza kusambaa kwenye damu kwa watu wenye upungufu wa kinga mwilini. 

Ugonjwa wa kaswende ni ugonjwa wa zinaa unaosababishwa na bakteria aina ya Treponema pallidum.  Ugonjwa wa huu ni kati ya magonjwa ya zinaa yanayoongoza kwa kusababisha madhara mengi.

Maambukizi ya kaswende wakati wa ujauzito huleta madhara mengi sana kama kujifungua kiumbe ambacho kimeshakufa, mtoto kuathirika na ugonjwa huu wakati wa kuzaliwa, mtoto kupata matatizo wakati wa   ukuaji wake, degedege na kuongezeka kwa vifo vya watoto wachanga nchini. 

Ugonjwa wa kaswende huathiri zaidi ya mimba millioni moja duniani kote kila mwaka na huchangia theluthi mbili ya vifo vya watoto wale wanaozaliwa tayari wameshakufa katika nchi za maeneo ya jangwa la sahara. Asilimia 30 ya mimba zinazoathiriwa na kaswende huishia watoto kufariki wakati wa kuzaliwa. Asilimia nyengine 30 ya mimba zinazoathiriwa na kaswende husababisha watoto kuzaliwa na ugonjwa huu wa kaswende, kupata matatizo ya ukuaji wao, degedege na kuongeza vifo vya watoto kwa asilimia 50.

Taasisi ya  kudhibiti Ugonjwa wa Ukimwi Tanzania (Tanzania National AIDS Control Programme) au NACP imesema maambukizi yote ya kaswende wakati wa ujauzito Tanzania bara kati ya mwaka 2003 hadi 2004 ni asilimia 6.7, kutoka asilimia 0.4 kwa mkoa wa Kilimanjaro hadi asilimia 32 kwa mkoa wa Tabora katika ripoti yake ya utafiti uliofanywa chini ya Wizara ya afya na ustawi wa jamii. Maambukizi yalionekana yako juu zaidi kwa wanawake walio na umri wa miaka 35 na zaidi (7%) na kiwango cha maambukizi kuwa chini zaidi kwa wanawake walio na umri kati ya miaka 15 – 24 (6.5%).

Ugonjwa wa ukimwi na kaswende mara nyingi huambatana pamoja. Ugonjwa wa kaswende huongeza uwezekano wa mtu kupata ugonjwa wa ukimwi.

Makala ya leo ni muendelezo wa magonjwa ya moyo ya kuzaliwa nayo, na ugonjwa wa leo hujulikana kama Tundu katika moyo, au Tundu katika kuta za ventrikali za moyo, ni ugonjwa ambao hutokea mara nyingi zaidi.

Watoto wenye tundu dogo katika moyo, huweza kukua bila matatizo yoyote, wakati wale wenye tundu kubwa huanza kuonesha dalili mapema

Vifuatavyo ni vihatarishi ambavyo vinaweza kupelekea kupata tundu katika kuta za chini za moyo

  • Maambukizi ya Rubella katika kipindi cha ujauzito
  • Ugonjwa wa kisukari ambao haujadhibitiwa kwa mama mjamzito
  • Matumizi ya pombe au madawa ya kulevya na baadhi ya dawa za hospitali katika kipindi cha ujauzito

Dalili

  • Rangi ya ngozi, midomo na kucha hubadilika na kuwa bluu
  • Kunyonya au kula kwa shida sana, na ukuaji wa shida
  • Kupumua kwa shida
  • Kuchoka haraka
  • Kujaa miguu na kuvimba tumbo
  • Mapigo ya moyo ya haraka
  • Kwa mtaalamu anaweza kusikia ishara ya ongezeko la sauti ya ziada ya mapigo ya moyo ya mtoto hali ambayo wataalamu huiita holosystolic murmur kwa kutumia kifaa kitaalamu stethoscope

Moja ya madhara ya ugonjwa wa kisukari katika mwili wa binadamu ni ugonjwa wa figo (diabetic nephropathy). Ugonjwa huu ambao huwapata watu wenye kisukari, hutokea muda mrefu baada ya mtu kugunduliwa kuwa na kisukari.

Kinachotokea (Pathofiziolojia)

Figo zinaundwa na mamia kwa maelfu ya vijiumbo vidogo vidogo viitwavyo nefroni (nephrons). Kazi ya hizi nefroni ni kuchuja damu na kutoa uchafu mwilini mwako kwa njia ya mkojo.

Kwa watu wenye kisukari, nefroni huwa na tabia ya kukakamaa, kuzeeka na kuwa na makovu kadiri miaka inavyopita. Baada ya muda fulani, hushindwa kabisa kazi yake ya kuchuja uchafu, matokeo yake protini ambazo kwa kawaida huwa haziwezi kuchujwa, huchujwa na kutoka katika mkojo.

Chanzo hasa cha kuzeeka, kukamaa na kuwa makovu huku kwa nefroni hakijulikani. Hata hivyo inadhaniwa kuwa uthibiti mbaya wa sukari husababisha uharibifu wa figo, na madhara huongezeka maradufu kwa watu wenye shinikizo la damu lisilothibitiwa na kisukari kwa pamoja.

Kuharibika kwa chujio ama Glomerulonephritis ni aina ya ugonjwa wa figo unaoathiri sehemu maalum ya figo (chujio) inayohusika na uchujaji wa maji pamoja na uchafu kutoka katika damu. Sehemu hii huitwa glomelurus au chujio kama tutakavyokuwa tukitumia katika mada hii. 

Visababishi

Mara nyingi chanzo halisi cha kuharibika kwa chujio za figo (glomerulonephritis) huwa hakijulikani. Hata hivyo wakati mwingine uharibifu huu unaweza kusababishwa na kushambuliwa na mfumo wa kinga ya mwili. Uharibifu katika chujio husababisha damu pamoja na protini kuingia katika mkojo. 

Tatizo hili hukua kwa haraka na figo linaweza kupoteza uwezo wake wa kuchuja maji na uchafu kwa kasi ndani ya muda mfupi wa kati wiki chache mpaka miezi kadhaa. Aina hii ya kuharibika kwa chujio za figo kwa haraka hujulikana kitalaamu kama rapidly progressive glomerulonephritis. 

.

Ukubwa wa tatizo na vihatarishi vyake

Takribani robo ya watu wanaopatwa na tatizo sugu la glomerulonephritis huwa hawana historia ya kuwa na ugonjwa wowote wa  figo hapo kabla. 

Kuna mambo kadhaa yanayoweza kumfanya mtu awe katika hatari ya kupata glomerulonephritis. Mambo hayo ni pamoja na:

  • Matatizo katika mfumo wake wa damu au lymph
  • Kuwahi kutumia vimiminika vilivyotengenezwa kwa kemikali za hydrocarbon
  • Wenye historia ya saratani
  • Maambukizi ya bakteria aina ya streptococcus, virusi, majipu au maambukizi katika moyo 
  • Mambo mengine yanayoweza kuongeza hatari ya kupatwa na glomerulonephritis ni pamoja na:
  • Magonjwa ya mishipa ya damu kama vile vasculitis au polyarteritis
  • Matumizi yaliyopitiliza ya dawa za kutuliza maumivu za jamii ya Non steroidal anti-inflammatory drugs kama vile aspirin na diclofenac
  • Magonjwa ya mfumo wa kinga ya mwili kama vile Anti-glomerular basement membrane antibody disease na IgA nephropathy
  • Makovu katika chujio (Focal segmental glomerulosclerosis) au hali ya chujio kuwa na kuta nene kuliko kawaida (Membranoproliferative GN)
  • Magonjwa yanayoathiri viungo mbalimbali vya mwili kama vile Henoch-Schonlein purpura, IgA nephropathy, Goodpasture’s syndrome au Lupus nephritis 
  • Ugonjwa wa kimetaboliki wa Amyloidosis

 Dalili

Dalili kuu za glomerulonephritis ni kuwa na damu katika mkojo (hali inayoufanya mkojo kuwa na rangi kama nyeusi, kutu au samawati; mkojo kuwa kama wenye povu jingi (kwa sababu ya kuwa na protini nyingi kuliko kawaida) na kuvimba uso, macho, miguu au tumbo (hali inayojulikana kama edema) 

Baada ya kujifungua mtoto wangu wa kwanza, daktari wangu wa meno alinilalamikia kuwa situnzi vema afya yangu ya kinywa na meno. Kiukweli sikuwa nikifanya jambo lolote la ziada kuhakikisha afya yangu ya kinywa na meno iko katika hali nzuri.

Daktari wangu wa meno aliendelea kunieleza kuwa wanawake wajawazito wote na mama watarajiwa mara nyingi hupuuzia usafi wa kinywa na meno wakati wa ujauzito. Kiukweli, sikumuamini kabisa pale aliposema kuwa ujauzito husababisha mama wajawazito kubadili tabia zao za usafi wa kinywa na meno, lakini alikuwa sahihi kwa kiasi kikubwa kwa kunieleza kuwa wakati wa ujauzito vichocheo (hormones) vya mwili wa mwanamke hubadilika kwa kiwango kikubwa sana na mara nyingi huathiri afya ya fizi, hivyo ikiwa afya ya fizi ni dhaifu haiyumkini hali hii ikaathiri ukuaji wa kichanga tumboni mwa mama.

Tafiti zimethibitisha kuwa afya duni ya kinywa na meno hususani ugonjwa wa fizi unasababisha kuharibika kwa ujauzito. Tafiti iliyofanyika huko Marekani, Karolina ya Kaskazini kuangalia hali ya afya ya kinywa na meno kwa wamama watarajiwa 812, uchunguzi ulifanyika kwa kila mwanamama kwa kipindi cha majuma 26, na kisha masaa 48 baada ya kujifungua.

Watafitii walihakiki kiwango cha kuharibika mimba (chini ya majuma 28) na uzito mdogo wa kuzaliwa (chini ya 1000 gms), takwimu zilizingatia rangi ya mama (race), namba ya watoto wanaozaliwa, na jinsia ya mtoto. Asilimia 1.1 ya wamama waliokuwa na afya bora ya kinywa na meno (wamama 201) walipjifungua watoto njiti.

Kiwango hiki kiliongezeka zaid miongoni mwa wamama 566 waliokuwa na afya dhaifu ya kinywa na meno kutoka asilimia 3.5 mpaka asilimia 11.1 miongoni mwa wamama 45 waliokuwa na afya mbaya na afya mbaya zaidi ya kinywa na meno hususani magonjwa ya fizi.

Upungufu wa damu mwilini au Anemia ni miongoni mwa magonjwa yanayosumbua watu wengi duniani. Anemia humaanisha kupungua kwa kiwango cha chembechembe nyekundu za damu (RBC’s) katika mzunguko wake, au kupungua kwa wingi wa hemoglobin kwenye damu.

Kazi ya hemoglobin ambayo hupatikana ndani ya chembechembe nyekundu za damu ni kubeba gesi ya oksijeni kutoka katika mapafu na kusambaza kwenye tishu. Kwa sababu hiyo upungufu wa damu husababisha ukosefu wa hewa muhimu ya oksijeni katika viungo au hypoxia.

Kwa mujibu wa shirika la Afya duniani (WHO), viwango vya hemoglobini hutofautiana kati ya jinsia moja na nyingine, na kati ya nchi au eneo na eneo. Hata hivyo, iwapo nchi zote zitazingatia viwango hivi vya WHO, kunaweza kutokea mkanganyiko hususani kwa nchi zinazoendelea kama za Afrika hivyo basi ili kuepuka hali hiyo Wizara za afya za nchi husika zimejiwekea viwango vyao kutokana na mazingira ya nchi zao.

Kwa mujibu wa takwimu za WHO, na kulingana na jinsia, mtu aliye na chini ya viwango vifuatavyo huhesabika kuwa na upungufu wa damu, kwa wanaume chini ya 13g/dl, wanawake wasio wajawazito chini ya 12g/dl wakati wanawake wajawazito na watoto ni chini ya 11g/dl.

Upungufu wa damu husababishwa na nini?

Mambo yanayoweza kusababisha upungufu wa damu yanaweza kugawanywa katika makundi makuu matatu, ambayo ni:

  • Kupungua kwa uzalishwaji wa chembe nyekundu za damu yaani impaired production of rbcs kunakoweza kutokea iwapo kuna upungufu wa madini muhimu ya chuma (iron deficiency) hali ambayo husababishwa na mtu kuwa na minyoo aina ya hookworms au mtu kuwa na vidonda vya tumbo; upungufu wa vitamin hasa vitamin B12 pamoja na upungufu wa folic acid; na magonjwa sugu ya figo (chronic renal failure)
  • Kuongezeka uharibifu wa chembe nyekundu za damu kuliko kawaida yaani increased destruction of rbcs. Hali hii huitwa hemolytic anemia ambayo inaweza kutokea iwapo mtu ana kasoro katika umbo la chembe zake nyekundu za damu kwa mfano iwapo ana magonjwa ya hereditary spherocytosis au sickle cell; aliongezewa damu isiyoendana na kundi lake yaani blood transfusion reaction; ana malaria, au saratani ya damu kama vile chronic lymphocytic leukemia.
  • Kupoteza damu yaani blood loss ambayo yaweza kusababishwa na mambo kama ajali; kupoteza damu wakati wa upasuaji; na kupoteza damu kunakotokea kwa wanawake mara baada ya kujifungua au postpartum hemorrhage (PPH).
  • Sababu nyingine zinazoweza kusababisha upungufu wa damu mwilini ni pamoja na kuungua (burns); matumizi ya dawa au kemikali zinazoathiri sehemu laini ya mifupa inayohusika na uzalishaji wa chembe nyekundu za damu (bone marrow); magonjwa yanayosababisha kuharibika kwa chembe nyekundu za damu kabla ya muda wake kama vile thrombocytopenic purpura na hemolytic uremic syndrome

Dalili za Anemia ni zipi?

Kwa ujumla dalili za upungufu wa damu ni pamoja na

  • Mwili kuwa mchovu au mlegevu
  • Kupungua na kukosekana kwa umakini
  • Mgonjwa kushindwa kupumua vizuri hasa baada ya kutoka kufanya kazi nzito au mazoezi
  • Mapigo ya moyo kwenda haraka
  • Kucha kuwa na umbo la kijiko (Koilonchyia) na kukatika kirahisi. Hali hii hutokea kwa wenye upungufu wa madini ya chuma.
  • Kuwa na manjano (jaundice) kwenye macho, ngozi na sehemu nyingine za mwili kutokana na kuongezeka kwa uharibifu wa chembe nyekundu za damu.
  • Wakati mwingine, iwapo anemia ni kali, mgonjwa anaweza pia kuwa na dalili za moyo kushindwa kufanya kazi (heart failure) kama vile kuvimba miguu, au kushindwa kupumua wakati wa kulala bila kuinua kitanda (flat)
  • Baadhi ya wagonjwa wenye anemia inayotokana na upungufu wa madini ya chuma mwilini hupendelea kula vitu kama udongo, chaki, penseli, mchele mbichi, au vipande vya barafu, hali ambayo kitaalamu huitwa PICA.

Vipimo na Uchunguzi:

Vipimo kwa ajili ya tatizo hili vimelenga kutambua iwapo mgonjwa ana upungufu wa damu pamoja na kutambua chanzo chake. Vipimo hivyo ni

  • Kupima damu na viainishi vyake (complete blood count/full blood picture with red cell indices) kama vile MVC, MCH na MCHC.
  • Kuchunguza damu kwenye darubini (peripheral blood smear) ambayo husaidia kugundua iwapo kuna tatizo kwenye umbo la chembe nyekundu za damu.
  • Hemoglobin electrophoresis
  • Sickling test iwapo mgonjwa anahisiwa kuwa na ugonjwa wa sickle cell
  • Kuchunguza choo (stool examination) husaidia kugundua uwepo wa minyoo (hookworms)
  • Kuchunguza mkojo (urine examination)
  • Kucuhunguza uwepo wa vidonda vya tumbo kwa kutumia Endoscopy na vipimo vya barium
  • Kuchunguza sehemu ya mifupa inayozalisha chembe nyekundu za damu (bone marrow examination)

Matibabu ya Upungufu wa damu

Matibabu ya upungufu wa damu hutegemea kiwango cha upungufu (ukubwa wa tatizo) na chanzo chake. Kulingana na chanzo, matibabu yanaweza kujumuisha

  • Lishe yenye virutubisho muhimu kwa ajili ya wenye upungufu wa madini ya chuma, vitamin B12, na folic acid. Vyakula kama mboga za majani, nyama, na matunda hushauriwa sana.
  • Matumizi ya dawa za corticosteroids hasa kwa wagonjwa wenye autoimmune hemolytic anemia
  • Kuacha matumizi ya dawa au kemikali zenye kuathiri sehemu za mifupa zinazohusika na uzalishaji chembe za damu
  • Kuongezewa damu kwa wale walio poteza kiasi kikubwa cha damu au wale wenye dalili za moyo kushindwa kufanya kazi.
  • Kwa wenye minyoo ya hookworms hupewa dawa za kuua na kuondoa minyoo mwilini.
  • Kutibu malaria ipasavyo
  • Kutibu vidonda vya tumbo kwa wenye tatizo hili

Jinsi ya kuzuia upungufu wa damu: Namna ya kuzuia upungufu wa damu ni pamoja na kujitahidi kula mlo kamili wenye mchanganyiko wa nyama, mboga za majani, maziwa na matunda; kutambua dalili na kutibu haraka magonjwa yawezayo kuleta upungu wa damu; pamoja na kuwapa mama wajawazito vidonge vyenye madini ya chuma na folic acid

Ni ugonjwa unaoshambulia ini na husababishwa na virusi au bacteria wa aina za A, B, C, D

Na vile vile huweza kusababishwa na :

  • Fangasi
  • Unywaji wa pombe (alcoholic hepatitis)
  • Dawa
  • Magonjwa yanayosababishwa na kinga ya mwili kuushambulia mwili (autoimmune)
  • Magonjwa ya kimetaboliki

Magonjwa yanayosababiswa na virusi au bacteria husambazwa kutokana na aina zake:

Homa ya Ini isababishwao na aina A (Hepatitis A), E

  • Kwa kula kinyesi kilichochanganyika na aina hii ya vimelea kwenye Maji, chakula

Homa ya Ini isababishwao na aina B (hepatitis B), C, D, G

  • Mchanganyiko wa damu ambao hutokana na:
    • Ngono zembe
    • Kutumia Sindano zilikwishatumika wakati wa matumizi ya madawa ya kulevya
    • Wakati wa kuwekewa damu
    • Kwenye kusafisha figo kwa wenye shida za figo

Mwaka 2013 virusi vya homa ya ini vilishika nafasi ya saba kwenye sababu ya vifo duniani,  mara nyingi homa ya Ini husababishwa na virusi zaidi ya hizo sababu nyingine.

Na homa ya ini imeganwanyika kama ifuatavyo

  • Ya hapo kwa papo kitaalamu acute hepatitis
  • Sugu kitaalamu chronic hepatitis

Dalili za Homa ya Ini

Kwa wagonjwa wengine wanaweza kukaa bila dalili mpaka madhara ya ugonjwa huu yanapoathiri ini.

Dalili ambazo hutokea ni:

  • Kichefuchefu
  • Kutapika
  • Ladha kubadilika mdomoni
  • Kupoteza hamu ya kula
  • Uchovu
  • Kuwashwa
  • Kukojoa mkojo mweusi
  • Maumivu ya tumbo upande wa juu wa kulia
  • Manjano kuonekana kwenye viganja vya mkono na machoni
  • Maumivu ya misuli na viungo
  • Homa

Madhara ambayo yanaweza kutokea baada ya kuugua homa ya Ini

  • Ini kuoza (hepatic necrosis)
  • Ini kukakamaa na kuota vinundunundu (cirrhosis)
  • Ini kushindwa kufanya kazi (hepatic failure)
  • Saratani ya Ini (hepatocellular carcinoma)

Vipimo

  1. Maabara
  • Kipimo cha damu kujua aina ya homa ya ini
  • Kipimo cha kuangalia ufanyaji kazi wa ini, kupitia kuangalia vimenge’nyo vya kwenye ini
  1. Picha
  • Kipimo cha kuangalia ini kitaalamu ultrasound

Tiba

Ni vyema kwenda hospitali na kufanyiwa uchunguzi kusudi upewe dawa na matibabu muhimu.

Baadhi ya wagonjwa huweza kunufaika na matibabu ya dawa, na madhumuni ya dawa ni kuzuia kuendelea kuathirika kwa ini

Dawa ambazo mgonjwa hupewa kitaalamu ni: ( interferons [IFNs], antivirals, and corticosteroids)

Lamivudine na Adenofir zimeonyesha matokeo ya kuaminika kwenye matibabu ya homa ya ini aina B.

 

 

Ushawishi wa kuandika makala hii ya tatizo la kutokwa usaha wakati wa kukojoa umetokana na swali la msomaji wetu ambaye aliuliza hivi kwenye tovuti hii na hapa na mnukuu,

 " Dr khamisi samahani sana mi nasumbuliwa nikikojoa mwisho wa mkojo unatoka kama usaha na sina dalili ya kaswende ambazo umezizungumzia nakuomba unisaidie’’.

Bila shaka wapo wengi ambao wana tatizo kama hili na ambao wamewakilishwa kupitia swali hili lililoulizwa na msomaji wetu huyu. Naomba tuwe pamoja kwenye makala hii ili ujifunze kuhusu tatizo la mtu kutokwa usaha wakati wa kukojoa.

Tatizo la Kuwepo kwa chembechembe za usaha au usaha kwenye mkojo hujulikana kama pyuria ambapo linaweza kuonekana kwa kutumia hadubini (microscope) au kama tatizo ni kubwa linaweza kuonekana kwa macho.

Visababishi vya tatizo la Kutokwa Usaha Wakati wa Kukojoa ni nini?

Visababishi vya tatizo hili ni kama vifuatavyo;

  • Ugonjwa wa mfumo wa mkojo (UTI)-Maambukizi kwenye figo, kwenye mrija wa mkojo na kwenye kibofu cha mkojo (cystitis- amabayo huonekana sana)
  • Magonjwa ya Zinaa-Kama ugonjwa wa kisonono au ‘’gono’’ kama wengi wanavyoita, ugonjwa wa Chlamydia na Trichomoniasis
  • Sumu inayotokana na kemikali (Chemical poisoning) kama 4-Aminodiphenyl inayotumika kwenye maabara na kwa ajili ya tafiti
  • Tatizo linajulikana kama Reiter’s syndrome
  • Pyelonephritis-Maambukizi ya bakteria kwenye sehemu za figo zinazojulikana kama calyces, renal pelvis na tishu za figo
  • Madhara ya pyelonephritis ambayo husabababisha ugonjwa unaojulikana kama renal abscess
  • Maambukizi kwenye tezi dume-Prostatitis (Kwa wanaume)
  • Upungufu wa kinga mwilini
  • Mcharuko (Inflammation) kutokana kuwa na mawe kwenye kibofu cha mkojo au kwenye figo
  • Mzio (Allergy) au kuota uvimbe sehemu yoyote ya mfumo wa mkojo

Viashiria vya tatizo hili ni;

  • Maumivu makali ya kuchoma (Painful burning sensation) wakati wa kukojoa
  • Maumivu chini ya kitovu
  • Homa
  • Kutapika

Tatizo hii likidumu kwa muda mrefu husababisha kupungua uzito kwa mgonjwa

Ni ugonjwa unaowaathiri sana watoto mpaka kufananishwa kuwa ni moja ya hatua za ukuaji wa mtoto. Mgonjwa wa tetekuwanga hutokewa na vijipele vyenye majimaji mwili mzima. Vijipele hivi huwa vinawasha kitendo kinachomfanya mgonjwa wa tetekuwanga kutojisikia vizuri huku akishinda anajikuna mwili mzima. Tetekuwanga husababishwa na virusi kwa kitaalamu hujulikana kama Varicella Zoster (VZV).

Mara nyingi ugonjwa huu wa tetekuwanga huwa haujirudii, hii ndiyo sababu imezoeleka sana kwa wengi kusema kama haujawahi kuugua basi usikae karibu na mgonjwa wa tetekuwanga. Ikumbukwe kuwa, ugonjwa wa tetekuwanga unayo kinga ingawa hapa kwetu upatikanaji wake bado haujasambaa sehemu zote.

Dalili za ugonjwa wa tetekuwanga

Dalili kuu za ugonjwa wa tetekuwanga ni vijipele (kama malengelenge) vinavyowasha. Ugonjwa huu huchukua muda mpaka kuanza kujitokeza kwa dalili zake, mgonjwa wa tetekuwanga ataanza kuona dalili hizi baada ya siku 21 tangu virusi vya ugonjwa huu kuingia kwenye mwili wake (baada ya maambukizi). Ukiachana na vijipele vinavyowashwa, dalili nyingine za ugonjwa wa tetekuwanga ni kama;

  • Kuumwa kwa kichwa
  • Homa
  • Kupungukiwa kwa hamu ya kula

Hizi ni dalili za awali ambazo huanza kujitokeza kabla ya vipele kuanza kuchomoza, mara nyingi huchukua siku moja au mbili mara baada ya kuanza kusikia dalili hizi mpaka kuanza kujitokeza kwa vijipele. Vijipele vya tetekuwanga hupitia hatua kadhaa;

  • Vijipele vyekundu au pinki hujitokeza mwili mzima
  • Vijipele huiva na kuanza kutoa majimaji
  • Vijipele vinavywea na kuanza kukauka

Kumbuka, vijipele hivi havijitokezi kwa wakati mmmoja, hivyo wakati vingine vinapona, kuna vingine vitakuwa ndiyo vinatokeza.

Mgonjwa huendelea kujisikia vibaya mpaka vijipele vikauke, na hatua hii huweza kuchukua hadi wiki mbili mpaka kupotea kabisa.

Nini husababisha Tetekuwanga?

Kama tulivyoeleza hapo juu, tetekuwanga husababishwa na virusi ambavyo kwa kitaalamu hujulikana kama Varicella Zoster (VZV). Mara nyingi ugonjwa wa tetekuwanga huambukizwa kutokana na kugusana na mtu mwenye ugonjwa wa tetekuwanga. Virusi vya tetekuwanga huendelea kuwa na uwezo wa kuambukiza mpaka malengelenge (vijipele) viwe vimetumbuka na kukauka. Hivyo epuka makutano na mgonjwa wa tetekuwanga mpaka vipele vitakapokauka kabisa. Virusi hivi huweza kuambukizwa kwa njia zifuatazo;

Ukurasa 6 ya 12